Wiki hii maonesho ya bidhaa za China yanafanyika katika maeneo ya viwanja vya Jubilee Jijini Dar es Salaam. Kwenye maonesho haya makampuni makubwa ya China yataonyesha bidhaa mbalimbali zaidi ya 197, za makundi manne – Ya mashine na magari, vifaa vya nyumbani, vifaa vya umeme na vifaa vinavyotumia umeme wa jua. Maonesho haya yamefanya baadhi ya watu waanze kuzungumzia tena suala la bidhaa feki, kwa kuwa kwa sasa China inajulikana kama kiwanda cha dunia, tena China na Tanzania zinafanya biashara kubwa ya bidhaa, na baadhi ya bidhaa hizo zinatajwa kuwa “feki”.
Kwenye maonesho hayo yanayohusisha makampuni makubwa kutoka China, si rahisi kuwa na bidhaa feki. Kwa kuwa bidhaa zinazotengenezwa na makampuni hayo makubwa zinatumiwa na mamilioni ya wachina kila siku, na kama zingekuwa na matatizo basi zisingeoneshwa. Aidha hii si mara ya kwanza kwa maonesho kama haya kufanyika, huko nyuma kwenye maonesho kama haya hakukuwa na tatizo la bidhaa feki. Lakini uzuri ni kuwa yamerudisha tena mjadala kuhusu suala la bidhaa “feki”.
Tatizo la bidhaa “feki” nchini Tanzania kwa sasa limekuwa wazi, karibu kila mtu anajua tatizo hilo na huenda ameguswa kwa namna moja au nyingine. Pamoja na kuwa bidhaa zinazotajwa kuwa “feki” zinatoka katika nchi mbalimbali na nyingine zinatengenezwa Tanzania, China ndio inalalamikiwa zaidi kwa kuwa bidhaa nyingi zinazotumiwa na watu nchini Tanzania zinatoka China. Hili kwa kweli ni jambo linaloeleweka.
Lakini kumekuwa na kitu kama upotoshaji kuhusu jambo hili, na kuwafanya baadhi ya watu waamini kuwa China ndiyo inaleta bidhaa hizo “feki” na zenye ubora wa chini, kana kwamba imeamua kufanya hivyo makusudi kwa nchi yetu, na wananchi tumekuwa tunaelekeza lawama kwa China na kuonesha kuwa sisi ni wahanga wa tatizo hilo, bila kuangalia undani wa tatizo hilo.
Nchini China wana viwanda na wanatengeneza bidhaa kwa kuangalia hali ya mahitaji na soko. Pamoja na kwamba wachina wengi wana uwezo wa kununua bidhaa za bei kubwa au za chapa maarufu, si kila mmoja ana uwezo huo. Kwa hiyo wanaotengeneza bidhaa wanalenga wanunuzi wote. Kuna siku nilikwenda kwenye kiwanda kimoja cha kutengeneza T-shirts za Polo (maarufu kama form six), nilipewa machaguo manne, bei ya chaguo la kwanza ilikuwa kama shilingi elfu 13 na ya chaguo la mwisho ilikuwa kama shilingi elfu 5. Lakini ukiangalia kwa macho T-shirt zote zina mwonekano sawa. Niliambiwa nichague kwa mujibu wa uwezo wa mfuko wangu. Siku nyingine niliwasindikiza wageni kutoka Tanzania kununua nguo za chapa maarufu, muuzaji aliniambia ana nguo za chapa moja lakini za aina mbili, moja ni bei poa na nyingine ni bei mbaya, lakini zote zinafanana kwa ubora. Ya bei mbaya ilikuwa bei mbaya kwa kuwa ilifuata taratibu halisi za haki miliki, ya bei poa ilikuwa poa kwa sababu haikuwa na nembo yoyote. Wenzangu wakaamua kununua ya bei poa, na mwuzaji akasema tuweke kwenye begi hadi tutakapoondoka.
Ukiangalia mifano hiyo miwili unaweza kuona kuwa hata watu wanapozungumzia suala la bidhaa “feki” kuna wakati hawaelezi vizuri, bidhaa “feki” ni ipi na isiyo na ubora ni ipi. Kuna bidhaa “feki” lakini zina ubora mzuri, tatizo sio bidhaa hizi, tatizo ni bidhaa zenye ubora wa chini. Lakini tatizo hili halipo Tanzania peke yake lipo China pia, miaka ya nyuma kuna wakati wachina walilalamika sana na serikali yao ilitumia nguvu nyingi sana kupambana na tatizo hilo.
Tukiangalia kwa upande wa Tanzania, tunaweza kuona kuwa kwenye tatizo hili la bidhaa “feki” kuna pande mbili zinazohusika, muuzaji na mnunuaji. Wafanyabiashara wa Tanzania wanaokuja hapa China kununua bidhaa, kwanza huwa wanaangalia uwezo wao kifedha, pili huwa wanaangalia ni bidhaa ipi inahitajika nyumbani na tatu huwa wanaangalia uwezo wa wateja kununua bidhaa hiyo. Kuna wakati wauzaji wanawaambia bidhaa hizi hazifai kwenda kuuzwa kwenye masoko ya nje, lakini wao wanang’ang’ania kuwa hizi ndio zinafaa soko letu na wateja wetu. Kwa hiyo linapokuja suala la biashara, mfanyabiashara huwa anaangalia soko na faida tu, mengine atafikiria baada ya kupata faida.
Tunachotakiwa kuangalia ni vipi bidhaa hizo zinaingia Tanzania. Bidhaa nyingi zinazoingia Tanzania zinapitia bandarini au kwenye viwanja vya ndege, ingekuwa vizuri tukafahamu kuna utaratibu gani katika sehemu hizo unaohakikisha kuwa bidhaa “feki” na hafifu haziingii Tanzania. Tunatakiwa tujue kama kweli tuna vigezo maalum vya bidhaa zinazoingia, au tunaruhusu bidhaa yoyote inayoingia. Kama wanaoruhusu bidhaa kutoka nje wanajua kuwa wanaruhusu bidhaa hafifu, basi kuna sababu inayowafanya waruhusu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!