DUH! Imeshakuwa noma. Hii inaweza kuwa kauli ya mashabiki wa Manchester United baada ya straika wao aliyekwenda kiwango cha juu msimu huu, Wayne Rooney, kugomea mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na klabu hiyo.
Licha ya straika huyo kudaiwa kufurahia maisha
ndani ya Old Trafford kwa sasa, bado dhamira yake ya kuihama Manchester
United ipo palepale baada ya kushindwa kuondoka katika uhamisho wa
majira ya kiangazi.
Ripoti iliyopatikana ni kwamba kambi ya Rooney
imekataa ofa ya mabosi wa Manchester United wanaotaka mazungumzo ya
kumbakiza fowadi huyo baada ya mkataba wake wa sasa kufikia tamati
mwisho wa msimu huu.
Rooney ambaye baadaye mwezi huu atafikisha umri wa
miaka 28, ameanza msimu akiwa kwenye kiwango bora kabisa, lakini
amejipanga kuibua upya sakata la kuwahama mabingwa hao wa Ligi Kuu
England na pengine ikiwezekana kwenye usajili wa Januari mwakani.
Mipango yake ni kwenda kupata changamoto mpya kwa
kujiunga na klabu inayoshiri Ligi ya Mabingwa Ulaya, mahali ambapo
atakuwa na uhakika wa kucheza kama straika wa kati. Kwa sasa tofauti na
alivyokuwa chini ya Sir Alex Ferguson, Rooney anatumika akiwa
mshambuliaji wa pili katika kikosi cha Manchester United kinachonolewa
na kocha David Moyes.
Jumatano iliyopita akiwa kwenye kambi ya timu ya
taifa ya England iliyokuwa ikijiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia
dhidi ya Montenegro iliyochezwa jana Ijumaa, Rooney aliulizwa kama
atabaki kwenye kikosi cha Manchester United na alisema: “Kama unavyoona,
kwa sasa nacheza na nafurahia soka langu. Nitakuwa na mazungumzo mazito
na klabu na hado tutatazama kitakachotokea.”
Mabosi wa Manchester United bado hawana uhakika
juu ya mchezaji huyo kubaki kwenye timu yao, huku wakala wake, Paul
Stretford, akionekana kupiga chapuo ya kumhamisha kutoka Old Trafford.
Manchester United iligoma kumuuza Rooney kwenda Chelsea, lakini sasa
amekataa kuongeza mkataba mpya baada ya ule wa sasa unaomshuhudia
akilipwa Euro 295,000 kwa wiki.
Julai mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu mpya wa
Manchester United, Ed Woodward, alidai hakuna haraka ya kufanya
mazungumzo ya mkataba mpya wa Rooney, jambo ambalo kwa sasa tayari
limeanza kuwashtua na kuona kwamba staa huyo ataondoka Old Trafford.
Arsenal na Paris Saint-Germain nazo zinafukuzia saini ya straika huyo wa kimataifa wa England.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!