Henry Joseph |
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata,
zinasema Henry ambaye amesajiliwa na Simba msimu huu huku akilipwa
mshahara wa Sh1.5 milioni, alikorofishana na kocha wake, Abdallah
Kibadeni, Jumatatu wiki hii katika mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika
katika Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
Henry anayemudu kucheza nafasi ya ulinzi na
kiungo, alirudi nchini mwaka huu akitokea klabu ya Kongsvinger ya Norway
iliyoshuka daraja. Kurejea kwake kumetokana na kukataa mkataba mpya wa
klabu hiyo wenye pesa kiduchu baada ya timu kuyumba kiuchumi.
Jumatatu wiki hii, wakati Simba ikiwa katika
mazoezi ya asubuhi kabla ya kuondoka jioni yake kwenda kambini Bamba
Beach, Henry alifanya mazoezi ya kukimbia pekee yake na baadaye
wachezaji wote walipofika uwanjani Kibadeni aliwataka wakimbie kwa
pamoja, lakini Henry inadaiwa aligoma kwa madai kuwa alikuwa tayari
ameshafanya mazoezi ya peke yake.
Hata hivyo, Henry alipozungumza na Mwanaspoti jana
Jumatano, alikanusha vikali madai hayo na kusema kuwa hawezi kufanya
kitendo kama hicho maishani mwake kwani anaheshimu wajibu wake.
“Sijawahi kufanya utovu wa nidhamu kwa kocha.
Nilifika pale saa 11 alfajiri, nilikuwa wa kwanza. Nikafanya mazoezi ya
kukimbia pekee yangu ili kujiweka fiti kwa sababu muda mwingi nilikuwa
majeruhi. Baadaye wenzangu walipofika nikajumuika nao, lakini Julio
(Jamhuri Kihwelu) akaniambia nipumzike kwani nimechoka,” alisema Henry.
Alisema alivyoambiwa hivyo alimfuata Kibadeni
kumwambia kuwa ameambiwa na Julio apumzike na baada ya hapo akawa amekaa
nje ya uwanja huku wenzake wakiendelea na mazoezi.
“Nilishangaa wakati Kibadeni anatangaza kikosi cha
kuingia kambini Bamba Beach, alisema sitakwenda na timu, badala yake
nikafanye mazoezi ninayoyajua mimi na kwamba akinihitaji ataniita,”
alisema Henry.
Alisema anamheshimu kila mtu na kwamba katika
maisha yake amejitahidi kufuata misingi na nidhamu ya soka na ndio maana
bado haelewi kisa kilichotokea mpaka Kibadeni kuamua kumuacha.
Henry alisema ili kujiweka fiti, ameendelea
kufanya mazoezi asubuhi na jioni na wakati mwingine amekuwa akienda gym,
lakini kwa sasa hayupo katika mazoezi ya Simba.
Mwanaspoti ilimtafuta Kibadeni kuzungumzia hilo na
alilisukuma suala hilo kwa Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’
ambaye majibu yake hayakuwa ya moja kwa moja, lakini yalitosha
kuthibitisha.
Julio alisema kila mchezaji anatakiwa kuwa na
nidhamu na kujituma katika mazoezi na kwenye mechi na asiyefanya hivyo
hurudishwa kikosi cha pili.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!