ITALIA kumeibuka mjadala mzito kwamba AC Milan imemwajiri mrembo
kwenye jopo la madaktari wa timu hiyo ili kuwa kama Chelsea. Kwenye
mitandao ya kijamii kunasambazwa picha ya mrembo, akitajwa kuwa ni
daktari mpya wa AC Milan, licha ya mabosi wake kuwa hawajathibitisha
bado.
Wakati jina la mrembo huyo likisakwa, mjadala huo
ulivuka mipaka hadi kwenye Ligi Kuu England, Stamford Bridge ambako kuna
daktari wa kike anayetesa kwenye ligi hiyo.
Chelsea inatesa na daktari wake mrembo, Eva
Carneiro. Wenye kejeli wanadai kwamba uwepo wa daktari Eva ndio chanzo
cha Ashley Cole na John Terry kuugua mara kwa mara. Lakini, hayo ni
masihara tu.
Tangu alipotua Stamford Bridge, Eva amekuwa
maarufu kwa kuwa daktari wa kike kufanya huduma kwenye klabu kubwa kama
Chelsea na kuweza kuhimili mikikimikiki ndani ya klabu hiyo.
Hakikuwa kitu kinachotarajiwa kufanywa na Chelsea
au na mmiliki wake bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich, lakini mara
baada ya kuchaguliwa kuinoa timu hiyo mwaka 2011, Andre Villas-Boas
alifanya usajili wa nguvu kwa kumnasa Eva ili kuwa daktari wa kikosi cha
kwanza cha timu hiyo.
Uwepo wa Eva kwenye benchi la Chelsea kulianza
kuwavuta wengi na kuifanya timu hiyo kutikisa England kwa kuwa daktari
wa kike, ambaye amekuwa akiwapa burudani mashabiki pia wakati
anapokimbia kuingia ndani ya uwanja kutoa huduma endapo kama kuna
mchezaji wa Chelsea aliyeumia.
Kwa mujibu wa wasifu wake kwenye tovuti ya
Chelsea, Eva aliwahi pia kufanya kazi katika kikosi timu ya Olimpiki ya
Uingereza kama daktari wa timu ya wanawake.
Cole asahau Chelsea imefungwa
Uwanja wa Hawthorns kwenye mechi ya Ligi Kuu,
dakika 90+4, Chelsea ikiwa nyuma 1-0 nyumbani kwa West Bromwich Albion,
Machi 3, 2012, Cole alianguka chini kuugulia kwamba ameumia.
Lakini, beki huyo wa kushoto baada ya Eva kuingia
uwanjani kumpatia huduma, alipoinama kumuuliza tatizo linalomsumbua huku
mikono yake ikiwa imemshika mgongoni mchezaji huyo, Cole alizubaa chini
na kushindwa kutambua kwamba alipaswa kunyanyuka haraka kwa kuwa tayari
timu yake ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Imedaiwa huduma ya mrembo huyo ilimzubaisha Cole na kushindwa
kutambua kwamba Chelsea ilipaswa kupambana walau kusawazisha bao hilo
ili kunusuru kibarua cha aliyekuwa kocha wao kwa kipindi hicho,
Villas-Boas.
Aanzia kikosi cha akiba
Daktari Eva anayeripotiwa kuwa na uzoefu mkubwa
kutokana na kufanya kazi katika taasisi kubwa tofauti, alianzia kwenye
kuwatibu wachezaji wa kikosi cha akiba kabla ya kupandishwa kwenye
kikosi cha kwanza katika msimu wa 2011-2012 na kocha AVB.
Haijafahamika sababu ya AVB kumpandisha mrembo
huyo na kumtaka awe daktari wa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza na
watangulizi wake hawakuwa wakifikiria mpango huo.
Moja ya wachezaji wa kikosi cha kwanza waliowahi
kufurahia huduma ya mchezaji huyo ni Terry wakati alipokuwa akisumbuliwa
na maumivu ya goti.
Ashabikia Chelsea
Japo kumekuwa na ugumu kidogo wa kufahamu mambo
yake binafsi, lakini taarifa zilizopatika Septemba 2009 ni kwamba mrembo
huyo ni shabiki mkubwa wa Real Madrid. Lakini, hivi karibuni alidaiwa
kuwa ni shabiki mkubwa wa Chelsea na hilo lilijionyesha dhahiri wakati
timu hiyo iliponyakua ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anachodai mwenyewe ni kwamba alianza kujihusisha
na mambo ya soka katika fainali za Kombe la Dunia 1998 na hasa
alipotazama mechi ya Brazil na Mexico. Wazazi wa Eva wana asili ya
Uingereza na Hispania, lakini anaonekana kuwahusudu sana Wabrazili.
Kazi nyingine ya mrembo huyo kwenye kikosi cha
Chelsea ni kuhakikisha anawasaidia wachezaji kupata usingizi hasa
wanapokuwa kwenye nchi ambayo majira yake yana tofauti kubwa na England.
Nesta alipata mke
Kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998
zilizofanyika Ufaransa, beki wa kati wa zamani wa Italia, Alessandro
Nesta ndiko alipompata mkewe Gabriela Pagnozzi.
Nesta, ambaye alifunga ndoa na Gabriela, Mei 7,
2007, alisema mapenzi na mrembo huyo yalianza baada ya kuumia kwenye
fainali hizo na kisha huduma zote alikuwa akizipata kutoka kwake.
Gabriela alikuwa mfanyakazi tu katika kambi ya Italia katika
fainali hizo na alipewa jukumu la kumhudumia Nesta alipopata majeruhi
kwenye mechi dhidi ya Austria.
“Ninachoweza kusema, niliumia kule Ufaransa na kisha yeye akawepo jirani yangu kwa ajili ya kunihudumia.
Maumivu yangu yamekwisha na yeye ameendelea kubaki
na mimi,” alisema Nesta ambaye amezaa watoto Sofia na Tommaso katika
uhusiano huo.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!