STRAIKA wa Simba, Amissi Tambwe, amewaambia mashabiki wa timu hiyo waachane na blaa blaa za Yanga na kuwasisitizia kwamba soka ni uwanjani.
Yanga inawatambia Simba baada ya kumnasa straika wa zamani wa Msimbazi, Emmanuel Okwi ambaye Mwanasheria wake ameisisitizia vyombo vya habari kwamba mchezaji huyo ni mali halali ya Yanga na si SC Villa ya Uganda wala Etoile du Sahel ya Tunisia.
Yanga na Simba zitapambana siku hiyo kwenye mechi maalumu ijulikanayo kwa jina la Nani Mtani Jembe iliyoandaliwa na wadhamini wao bia ya Kilimanjaro.
Lakini Tambwe anaamini ubora wa kikosi cha Yanga hauwatishi kwani mpira uwanjani hivyo dakika 90 ndio zitaamua nani zaidi ya mwenzake.
“Sisi tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo na hatuihofii kabisa Yanga kwani hata sisi tuko vizuri, wachezaji wote wa Simba wana viwango vya uhakika, hivyo waache hao Yanga wajitape kuwa wana kikosi bora siku hiyo ndiyo tutajua,” alisema Tambwe mchezaji kutoka hapa nchini
“Nasikia tu Yanga wanajitapa wana timu bora, lakini hatuwaogopi hayo ni maneno tu watu wasubiri mpira dakika 90, kama mechi iliyopita dhidi yetu wengi walikuwa hawatupi nafasi na tukawashangaza na ndicho kitakachotokea tena Jumamosi, tutawashangaza tena.”
Kambi ya Simba iliyopo mjini Unguja, Zanzibar imepamba moto ambapo kocha wao mkuu, Zdravko Logarusic, anawapa dozi ya mara mbili kwa siku kwenye Uwanja wa Fuoni na jana Jumatano beki kutoka hapa nchini,Gilbert Kaze aliwasili Dar es Salaam na anatarajiwa kuungana na wenzake leo Alhamisi.
Akizungumza na vyombo vya habari za michezo,kocha Logarusic ambaye ni raia wa Mcroatia alisema: “Maandalizi yetu yanaendelea kama kawaida, tunafanya mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni na kila kitu kinakwenda sawa, naamini tutashinda mechi hiyo.
“Kwa ujumla, hadi sasa bado sijapata kikosi cha kwanza na tunafanya kazi kwa pamoja. Naendelea kuwajua wachezaji, kama hawa waliokuwa na timu za taifa ndiyo nimeanza nao sasa na bado sijawajua vizuri nafikiri hadi Jumamosi kila kitu kitakuwa wazi.”
Akiwazunguzia kipa Mtanzania, Ivo Mapunda na beki wa kati, Donald Musoti raia wa Kenya ambao wote wamesajiliwa kutoka klabu ya Gor Mahia ya Kenya, Logarusic, alisema: “Bado wanatakiwa kupewa muda. Ivo na Musoti ndiyo wamejiunga kwenye timu mpya na sasa ni mapema mno kwao, wanahitaji muda kidogo ili wawe vizuri zaidi.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!