Nelson
Rolihlahla Mandela ni Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini ya
kidemokrasia. Ni mtu aliyejijengea heshima kubwa duniani kutokana na
jitihada zake kubwa zilizofanikisha uhuru wa nchi hiyo na nyinginezo
katika Bara la Afrika.
Mzee Mandela anayefahamika pia kwa jina la Mzee Madiba amelazwa
hospitalini mjini Pretoria, Afrika Kusini kwa zaidi ya mwezi sasa akiwa
mahututi. Anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu.
Kutokana na umaarufu wa Rais huyo mstaafu wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 95, Ismailniyonkuru.info tumeona vema kuchapisha historia fupi ya maisha yake kama ifuatavyo:
Nelson
Mandela ni mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati aliyepambana na sera za
ubaguzi za makaburu wa Afrika Kusini na hatimaye kuwa Rais wa kwanza
Mwafrika nchini humo. Ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Pia amepata
kutunukiwa zaidi ya tuzo 250 katika miongo minne iliyopita.
Ni
rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini.
Alikuwa mwanasheria na mwanachama wa Chama cha African National Congress
(ANC) aliyepinga utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Nelson
Mandela alizaliwa Julai 18, 1918. Baba yake mzazi alifariki wakati
Mandela akiwa na umri wa miaka tisa. Tangu kipindi hicho alilelewa na
Jonintaba hadi alipoitoroka familia hiyo baada ya kutakiwa aoe mwanamke
aliyepangiwa.
Mwaka 1943 Mandela alijiunga ANC. Aliiongoza Afrika ya Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na kuibuka kiongozi shujaa duniani.
Alipoanza
mapambano ya kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi na kutafuta usawa kwa
wote, ilitegemewa kuwa mke wake ndiye angekuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Mandela
alipata kuoa wake watatu katika historia ya maisha yake. Alimuoa mke wa
mwisho siku alipokuwa akiadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Madiba
anatajwa kuwa katika kipindi chote cha historia yake amekuwa akiwaunga
mkono watoto na upatikanaji wa elimu. Mfuko wa Nelson Mandela wa
kusaidia watoto ni sehemu tu ya ushahidi wa mafanikio ya Mandela
kuwasaidia watoto.
Mandela
ni baba wa watoto sita. Watoto wanne aliwazaa na mke wake wa kwanza,
Evelyn Mase na watoto wawili aliwazaa na mke wake wa pili, Winnie
Madikizela.
Inaelezwa kuwa baadhi ya watoto wake hawakupata kwenda kumwona Madela alipokuwa gerezani.
Watoto wake wote wawili wa kike aliowazaa na mke wa kwanza walikuwa wakitumia jina la Makazawie.
Mtoto
wake wa kwanza alifariki akiwa na umri wa miezi tisa na mtoto wa pili
aliyejulikana kwa jina la Madiba Thembikile (Thembi) alifariki katika
ajali ya gari mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 25. Mandela alikuwa
gerezani na hakuruhusiwa kwenda kuhudhuria mazishi ya mwanaye.
Mtoto
mwingine, Makgatho alifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi mwaka 2005. Mandela
amekuwa mstari wa mbele kupiga vita virus vya Ukimwi na Ukimwi akitumia
namba 46664 ambayo ni namba yake alipokuwa gerezani kupiga kampeni.
Mandela
na Evelyn walidumu katika ndoa yao kwa miaka 13 kabla haijavunjika
mwaka 1957. Evelyn alikuwa muumini wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova
lililokuwa haliruhusu waumini wake kushiriki kwenye siasa, hivyo muda
wote hakujihusisha na siasa. Alifariki mwaka 2004.
Mandela
alimuoa Winnie Madikizela mwaka 1958, ingawa muda mwingi hawakuishi
pamoja kwa sababu alikuwa kifungoni huku Winnie akijijengea umaarufu
katika majukwaa ya siasa.
Kutokana
na misuguano iliyoibuka ndani ya umaarufu wa kisiasa ya Mandela na
Winnie walijikuta wakipeana talaka mwaka 1994. Mwaka 1998 Mandela
alimuoa Graca Machel ambaye alikuwa mke wa kwanza wa Rais wa Msumbiji,
Samora Machel.
Rais
wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ameendelea kutoa wito kwa
wananchi wa nchi hiyo wamwombee heri wakati huu anapougua. Maombi
yamekuwa yakifanywa makanisani kote nchini Afrika Kusini kumwombea
Mandela apone maradhi yanayomsumbua.
Hata
hivyo, Mandela ameshaandika wosia wake na kuelekeza kwamba kama atakufa
azikwe kwenye milima iliyojitenga nyumbani kwa mababu zake huko Qunu,
Afrika Kusini.
Mandela
alikuwa Rais wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 1994 hadi 1999. Alifungwa
jela miaka 27 kuanzia mwaka 1962 hadi mwaka 1990. Anaelezwa kuwa
alikumbwa na ugonjwa wa mapafu alipokuwa akifanyishwa kazi ngumu katika
machimbo ya mawe akiwa gerezani.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!