KOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amempa pole mwenzake wa
Yanga, Ernest Brandts, kwa kupewa notisi na uongozi wa timu hiyo, lakini
akasema angekuwa anaifundisha Yanga angewatimua mabeki wanne wa kikosi
hicho wakiwamo nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
Logarusic ameliambia Mwanaspoti kuwa safu ya
ulinzi ya timu hiyo ndiyo tatizo kubwa na ndio maana akaichapa Yanga
mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe wiki iliyopita. Amesisitiza
kuwa tatizo si kocha Brandts.
Mabeki waliokuwa kwenye ukuta wa Yanga katika
mechi hiyo, kulia alicheza Mbuyu Twite, kushoto alikuwa David Luhende na
katikati walisimama Cannavaro na Yondani.
Logarusic alisema mabeki hao pamoja na kiungo
mkabaji wa siku hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’, walishindwa kutekeleza
majukumu yao ambapo waliruhusu washambuliaji wa Simba kuuona uso wa
goli, tofauti na kazi waliyofanya mabeki wake, Mkenya Donald Musoti na
Joseph Owino raia wa Uganda.
Mcroatia huyo aliongeza kuwa yeye hana tabia ya
kuwavumilia wachezaji wanaofanya masihara ya wazi uwanjani ambayo
yanaweza kuhatarisha ulaji wake na ndio maana anapogundua mchezaji
anakosa umakini, hakawii kumrudisha benchi au jukwaani.
“Nimesikia wamemfukuza (Brandts) nampa pole kwa
hilo, lakini haya ndio maisha yetu makocha, hakuna cha ajabu. Sasa
imetokea kwake na siku nyingine unaweza kusikia kwangu,” alisema.
“Lakini najua ni kutokana na matokeo dhidi ya
Simba. Ningekuwa naifundisha Yanga ningewafukuza mabeki wote waliocheza
katika mchezo ule. Ukiangalia kwa makini walivyokuwa wakicheza huwezi
kuamini kama kweli wale ni mabeki, walikuwa wakifanya makosa mengi ya
kushangaza.
“Wewe ni beki unaruhusu vipi mshambuliaji kupata
nafasi ya kuuona uso wa goli? Sipendi kuona beki anafanya makosa kama
yale unaona jinsi Musoti na Owino walichokuwa wakikifanya? Ndivyo mabeki
wanavyotakiwa kufanya.
“Ikitokea beki wangu anafanya uzembe kama ule wa
wale wa Yanga naweza kuwaondoa haraka na kama nikikasirika zaidi naweza
hata kuwatimua kabisa.”
Katika hatua nyingine, juzi Jumanne wachezaji wa
Yanga walikabidhiwa kitita cha Sh50 milioni zikiwa ni salio lililokuwa
limebakia kwenye zawadi ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita.
Habari ambazo Mwanaspoti imepata, zinasema kuwa
wachezaji hao walikabidhiwa fedha hizo ikiwa ni ahadi ya Mwenyekiti,
Yusuf Manji, ambaye aliwaahidi Sh100 milioni endapo watashinda mechi
tano za mwishoni mwa msimu huo na kutwaa ubingwa, jambo ambalo
walilitimiza.
Mwishoni mwa msimu uliopita, wachezaji hao
walipewa Sh50 milioni wagawane jambo ambalo halikuwafurahisha sana kwani
walihisi viongozi wao ni wababaishaji.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!