Msanii wa muziki wa kizazi kipya Tunda Man hivi karibu alizungumzia kwa namna alivyokuwa akimtungia nyimbo msanii wenzake wa muziki huo aitwa Matonya na fadhila alizozipata.
Akizungumza kwenye kipindi cha The Takeover kinachorushwa na kituo cha TBC fm, Tunda Man alisema, yeye ndiye ambaye alitunga na kuandika nyimbo mbili zilizompa jina Matonya, yaani Vaileth na Dunia mapito, "mimi ndiye ambaye nilitunga na kumuandikia Matonya zile nyimbo, yaani ule wa Vaileth na Dunia mapito". Alisema Tunda Man a.k.a Captain Tunda.
"Unajua ni hivi, Vaileth ni jina la dada yangu na nililitumia jina lile kwa sababu hiyo, nilimtungia na kumpa kama mshikaji ila kwa sasa siwezi kufanya hivyo kwa sasa sababu Matonya hana shukurani, japo juzi kati aliniomba nimtungie wimbo".
"Unajua binadamu tunatofautiana, hebu fikiria jamaa alishindwa japo kurudisha fadhila hata kwa mama yangu mzazi ambaye kwa kipindi kile alikuwa anatusaidia mimi na mshkaji japo kwa hela ndogo ndogo kama nauli nk. ila baada ya kutoka yote hayo aliyasahau na kuendelea na maisha yake, kweli tenda wema uende zako," alisema Tunda Man huku akiendelea. "Hii wala sio siri na muulize hata yeye na kama atabisha niambie".
Mtangazaji wa kipindi Dan Chibo alipomuuliza kwa nini hukuziimba wewe mwenyewe, Tunda Man alijibu, " kwa kipindi kile mimi nilikuwa siimbi sababu nilikuwa siamini kama kwa sauti yangu ningeweza kuwa ni muimbaji, niliamua kumtungia yeye kwa sababu hiyo".
Aliendelea kwa kusema "Siku moja nilikutana na mtaalamu mmoja kule Bagamoyo kwenye Chuo cha Sanaa na kunieleza kwamba sauti niliyo nayo ni sauti nzuri na inafaa kwa kuimba, na nikifanya hivyo nitakuja kuwa mwanamuziki mkubwa mwenye sauti ya kipekee, jamaa sitomsahau sababu yeye ndiye aliyenifungua kwenye hili, namshukuru sana".
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!