MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Wayne Rooney amekubali
kusaini mkataba mpya utakaomweka Old Trafford zaidi ya mwaka 2015 huku
akiwa mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo.
Rooney amesuasua kusaini mkataba mpya Old Trafford
na ilidaiwa kwamba alikuwa anajiandaa kuondoka mwishoni mwa msimu kwa
ajili ya kupata changamoto mpya ya soka nje ya Man United.
Mkataba wa Rooney unatarajiwa kumalizika mwishoni
mwa msimu ujao Juni 2015 na kulikuwa na wasiwasi kwamba staa huyo wa
zamani wa Everton alikuwa anataka kuondoka bure mwishoni mwa msimu ujao
hili apate fedha nyingi zaidi.
Hata hivyo, kocha David Moyes amefanikiwa
kumshawishi nyota huyo kubaki lakini kwa gharama za kumlipa mshahara wa
Pauni 300,000 (Sh.750 milioni) kwa wiki ambao unaweza kuwa wa mwisho
kwake klabuni hapo.
Wakati huohuo, licha kumnasa kiungo mchezeshaji wa
Chelsea, Juan Mata na kufanikiwa kumbakiza Rooney, Moyes amekumbana na
pigo baada ya kiungo wa Juventus aliyekuwa anamwinda, Arturo Vidal
kusisitiza kwamba atabaki klabuni hapo.
Moyes ameshasafiri mpaka Italia kwa ajili ya
kumwangalia nyota huyo wa kimataifa wa Chile ambaye yupo katika kiwango
cha juu na alikuwa anataka kumchukua katika kikosi chake kwa ajili ya
kukitia makali na kukirudisha katika ushindani.
Moyes atalazimika kuongeza juhudi zake kwa kiungo wa Bayern Munich, Toni Kroos ambaye anaweza kuuzwa.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!