WACHEZAJI wa Manchester United wamedhamiria kuachana na mwaka wa
tabu! Sasa wameanza kukesha mazoezini ili warejee njia zao za ushindi
na kuepuka msimu wa aibu.
Hata hivyo, itaendelea kukosa huduma ya mastraika
wake makini, Wayne Rooney na Robin van Persie kwa kuwa bado hawapo fiti
kutokana na kuugua.
Rooney amepelekwa Marekani kwenye hali ya hewa ya
joto ili kufanya mazoezi ya kumaliza tatizo la majeruhi ya nyonga,
wakati Van Persie bado hajapona maumivu ya paja.
Man United imepokea vipigo vitatu mfululizo kutoka
kwa Tottenham katika mechi ya Ligi Kuu England, Swansea City katika
mechi ya Kombe la FA na Sunderland katika pambano la Kombe la Ligi, leo
Jumamosi itacheza tena na Swansea uwanjani Old Trafford. Katika mechi
hizo tatu imefungwa 2-1 kila mchezo.
Katika msimamo wa Ligi Kuu England, Manchester
United ipo nafasi ya saba ikiwa imeachwa nyuma kwa pointi 11 na vinara
Arsenal pia ipo katika hatihati ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa
Ulaya msimu ujao.
Hata hivyo, sasa kipa namba moja wa timu hiyo,
David de Gea, amedai wachezaji wa timu hiyo wamepagawa na vipigo hivyo
na huwa wanabakia mazoezini kwa ajili ya kujifanyisha mazoezi ya ziada
kuokoa msimu wao mbovu.
“Mara nyingi tunabaki mazoezini baada ya programu
tukifanya mazoezi ya krosi na kumalizia. Tunafanya sana hasa wakati
ambapo hakuna mechi katika siku zinazofuata nadhani inanisaidia mimi na
wachezaji wengine kuimarika,” alisema kipa huyo.
Dea Gea ameongeza kuwa amekuwa akifanya mazoezi ya
ziada mara kwa mara na mshambuliaji Javier Hernandez ‘Chicharito’ kwa
ajili ya kuonyeshana ubabe na kuimarishana.
“Tunajaribu kusaidiana. Anajaribu kuniweka katika
wakati mgumu na mimi namweka katika wakati mgumu. Siku zote tunajaribu
kufanya kila tunaloweza na Chicharito ni mchezaji anayejituma kwa kila
kitu mazoezini.
“Ni mmoja kati ya wachezaji wa ukweli wa kulipwa
ambao nimewahi kuwaona katika maisha yangu ya soka. Ni mchezaji mahiri
sana na rafiki bora pia.”
Kuhusu Rooney, ambaye awali alidai ana uhakika
timu yao itarekebisha mambo licha ya vipigo vitatu mfululizo ataendelea
kukosekana jambo linaloiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu zaidi.“Tunahitaji sapoti wakati huu. Tutakuwa bora tu na tutarudi tena,” alisema Rooney.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!