LONDON, ENGLAND.JOSE Mourinho alipokwenda Old
Trafford msimu huu na kikosi chake cha Chelsea kucheza na Manchester
United kwenye Ligi Kuu England alichokifanya ni kupanga viungo na mabeki
tu, huku timu yake ikicheza kwa kujihami zaidi. Sifa yake kubwa Mreno
huyo kwenye soka ni mtindo wa kupaki basi.
Lakini, wakati ligi hiyo ikiingia kwenye mzunguko
wa pili, Jumatano iliyopita Chelsea ilimenyana na West Ham United na
kocha Sam Allardyce akaiga mtindo wa mwenyeji wake wa Stamford Bridge
kwa kucheza kwa kujilinda zaidi jambo lililomfanya Mourinho kung’aka na
kudai kwamba wapinzani wao walicheza soka la karne ya 19.
Mourinho amesahau mtindo wake huo wa kucheza kwa
kupaki basi jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa sana kwamba anatibua
mchezo wa soka. Lakini, kwa unafiki wake, Mourinho akaishambulia West
Ham United kwamba ilicheza kwa kubaki langoni kwao tu na kwamba
walihitaji sururu au shoka ili kuvunja ngome hiyo.
Hasira za Mourinho zilikuja baada ya mechi hiyo
kumalizika kwa sare ya bila kufungana na kikosi chake kikipoteza nafasi
ya kupanda juu kwa nafasi moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Wataalamu wa soka wanasubiri kuona Jumatatu ijayo
kama Mourinho hatapaki basi uwanjani Etihad atakapokwenda kumenyana na
Manchester City.
Makala haya yanazungumzia kauli za kinafiki za
Mourinho alizowahi kuzitamka katika mchezo huo wa soka na kuzua kasheshe
kubwa kwenye vyombo vya habari. Mourinho tabia zake ni kutaka
kuwadhihaki makocha wenzake na kutaka waanze kupambana kwa kurushiana
maneno.
Aliwahi kumtibua Arsene Wenger, Sir Alex Ferguson, Barcelona na hata watu wa Real Madrid wakati alipokuwa kocha wa kikosi hicho.
Kutoka kumwita Wenger kuwa ‘mpiga chabo’ hadi
kudai West Ham ‘walipaki basi’ langoni, hayo ni baadhi ya mambo yenye
utata mkubwa yaliyowahi kufanywa na kocha huyo.
Soka la karne ya 19
Alipozungumza baada ya mechi dhidi ya Arsenal
kwenye Uwanja wa Emirates iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana
mapema msimu huu, Mourinho alisema: “Nadhani inakera sana kwa timu
inayocheza nyumbani na kisha haifungi mabao. Inakera. Kwa sababu unajaza
uwanja na wengi wanataka kuona ushindi.”
Kwa tukio la hivi karibuni, Chelsea baada ya
kufanya mashambulizi 39 langoni kwa West Ham bila kufunga, Mourinho
akamjia juu na kuitaka timu hiyo inayonolewa na Allardyce kuacha kucheza
soka lililopitwa na wakati na kusema walihitaji kuwa na sururu kuvunja
ukuta uliokuwa umejengwa na wachezaji wa timu hiyo wakiwa wamejazana tu
langoni kwao ili wasifungwe.
Mreno huyo alianza kutambulika kimataifa baada ya klabu yake ya
FC Porto kuitupa nje Manchester United kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya
mwaka 2004 baada ya bao la dakika ya tisini la Costinha lililokuwa la
kusawazisha Old Trafford na baada ya mechi Mourinho alikimbia uwanja
mzima na kuburuzika.
Baada ya tukio hilo akaanza kutupa maneno makali
kwa kocha wa Manchester United wa kipindi hicho, Ferguson, alipodai:
“Najua kwa nini (Ferguson) amepagawa. Ana wachezaji wazuri duniani na
wangeweza kufanya vizuri zaidi. Ni lazima uchukie kwa timu yao
kutawaliwa na mpinzani uwanjani ambaye bajeti yake ni asilimia 10 ya
kwako.”
Staili ya kupaki basi
Huu si unafiki? Mourinho hakuchezesha straika
yeyote kwenye mchezo dhidi ya Manchester United uliofanyika Old Trafford
mapema msimu huu.
Baada ya sare ya bila kufungana, Mourinho alisema:
“Timu yangu ilipaswa kufanya hivi kwa sababu ina wachezaji wenye vipaji
vikubwa sana, lakini wakati mwingine inapaswa kucheza kwenye mazingira
magumu. Wawe na fikira za kiufundi, kufikiria matokeo ambayo si rahisi
kupatikana.
“Kwangu ilikuwa safi tu. Andre Schurrle alicheza dhidi ya Patrice Evra, Oscar alicheza nafasi tofauti kabisa. Ilikuwa safi.’
Lakini, alipokwama kuwafunga Tottenham Stamford
Bridge mwaka 2004, Mourinho aliishambulia timu hiyo na kusema: “Nadhani
hawa Tottenham walikuwa wamepaki basi la timu yao langoni,” na
kusisitiza Tottenham walipata pointi wasiyostahili kujaa golini kwao na
wao walitumia washambuliaji wao wote bila mafanikio.
Asema Wenger mpiga chabo
Akiwa na hasira baada ya kauli ya Wenger kuhusu
matokeo ya mechi, Mourinho alimshambulia kocha huyo wa Arsenal kwa kutoa
kauli iliyoibua utata mkubwa mwaka 2005.
Mourinho alisema: “Nadhani yeye ni mmoja wa wapiga
chabo. Anapenda kutazama mambo yasiyomhusu. Hawa ni watu ambao
unapokuwa nyumbani kwao, wanatumia darubini kuchunguza mambo ya familia
za wenzake. Anasemasema tu mambo ya Chelsea. Anatuogopa, yeye akiamka tu
Chelsea, Chelsea, Chelsea, Chelsea. Sijui kama anataka kibarua changu.
Atakuwa anaipenda Chelsea.”
Asababisha refa kujiuzulu
Mwaka 2005, Mourinho aliibua utata mkubwa sana
wakati Chelsea ilipomenyana na Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwenye mchezo wa kwanza, baada ya straika Didier Drogba kuonyeshwa kadi
nyekundu na mwamuzi Anders Frisk, Mourinho alimshutumu kocha wa
Barcelona wa wakati huo, Frank Rijkaard kwamba alimfuata mwamuzi kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo.
Shutuma hizo zilikuwa nzito sana na kumfanya mwamuzi Frisk
kujiuzulu. Mourinho alisema: “Didier Drogba alipotolewa kwa kadi
nyekundu baada ya kipindi cha kwanza sikushangazwa. “Nilipenda Frisk
achezeshe pia mechi ya marudiano pengine angetupendelea na sisi kama
alivyofanya kwa Barcelona.”
Amkomoa Gallas
Mourinho amekuwa hataki mzaha na wachezaji wake.
Wakati mwingine anaweza kutetea wachezaji wake kwa mambo ya kijinga,
lakini wakati mwingine anakuwa tofauti sana kama alivyombadilikia beki
Mfaransa William Gallas baada ya kupitiliza likizo yake na kuchelewa
kurudi kikosi Chelsea mwaka 2005.
“Kama mnavyoona, Gallas amekuwa na likizo ya aina
yake. Nadhani alifurahia safari yake ya Guadeloupe, palikuwa pazuri kwa
likizo yake na akaamua kubaki huko kwa muda mrefu.”
Amshambulia Ranieri
Wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Inter Milan,
Mourinho alikerwa na maneno yaliyotolewa na kocha wa Juventus wa wakati
huo, Claudio Ranieri baada ya Mtaliano huyo kuhoji mbinu za ukocha
zinazotumiwa na Mreno huyo.
Kwenye kujibu mapigo, Mourinho alisema:
“Nilijifunza Kitaliano saa tano kila siku kwa miezi mingi sana ili
kuweza kuwasiliana vizuri na wachezaji wangu, vyombo vya habari na
mashabiki. (Claudio) Ranieri alikuwa England kwa miaka mitano, lakini
bado alishindwa kusema ‘habari za asubuhi’ na ‘habari za jioni’.
“Ameshinda Super Cup, kombe dogo sana. Hajawahi
kutwaa taji kubwa. Pengine anahitaji mabadiliko ya kiakili, lakini pia
ni mzee sasa.”
Kadi za Camp Nou
Wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid,
Mourinho aliendeleza bifu dhidi ya Barcelona baada ya sasa kumenyana nao
kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwaka 2011, Mourinho alidai kwamba kikosi chake
cha Real Madrid kinafanya mazoezi ya kucheza wachezaji 10 uwanjani kwa
sababu wanafahamu wazi watakapokwenda Nou Camp lazima nyota wao mmoja
ataonyeshwa kadi nyekundu.
“Nafanya mazoezi na wachezaji 10 kujiandaa na
mechi ya Barcelona ili tufahamu tutachezaje pungufu, kwa sababu
niliwafuata Nou Camp nilipokuwa Chelsea tukamaliza mechi tukiwa 10,
nikaenda tena na Inter Milan tukamaliza 10, hivyo nafanya mazoezi ya
wachezaji 10 kujiandaa na hilo.”
Amponda Drogba
Si kitu ambacho ungeamini kingeweza kutoka kwenye
kinywa cha Mourinho kuhusu straika Didier Drogba. Mwaka 2010 wakati
alipoachana na Chelsea, Mourinho aliibuka na kumponda Drogba kwamba
alikuwa mchezaji muongo sana uwanjani kwa sababu alikuwa akijiangusha.
“Mimi si kocha tena wa Chelsea na hivyo simtetei
yeyote. Nadhani nitakuwa sahihi nikisema Drogba anajiangusha sana”
Anasema Mourinho.
“Drogba, Ronaldo, Torres na Van Persie wote
wanajiangusha. Nani amejirusha mara nyingi? Nani ameshinda penalti
nyingi kwa miaka ya hivi karibuni? Lakini, kwenye soka la England
wanaojirusha wanakosolewa sana.”
Amkandia Benitez
Mourinho anaweza sana kucheza na akili ya
mashabiki wa Chelsea baada ya kumkandia Rafael Benitez, aliyekuwa kocha
wa muda kwenye klabu hiyo.
Akizungumza baada ya Chelsea kuifunga Manchester
City 2-1 uwanjani Stamford Bridge, Oktoba mwaka jana, Mourinho
hakuchukua muda na kuanza kumshambulia Benitez na mbinu zake katika
klabu hiyo.
“Nilikuwa nazitazama sana mechi za Chelsea
ilizocheza dhidi ya Manchester City mwaka jana. Nilitazama mechi yao
Wembley, mechi ya nyumbani na mechi ya ugenini. Nilitazama pia mechi zao
za kirafiki kule Marekani. Kiakili, si kiufundi, Chelsea walikuwa
wameharibiwa sana.
“Alikuwa mwoga, wachezaji wakawa wanaogopa kusema
kwamba tunataka kushinda, tunaweza kushinda. Lakini, kitu muhimu kwa
sasa kwamba tumeanza kuiondoa hofu hiyo.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!