ARSENE Wenger ametoa kali ya mwaka baada ya kudai kwamba
alifahamu mchezaji mpya waliyemsajili mwezi Januari, Kim Kallstrom ni
mgonjwa na kwamba kwake si kitu muhimu sana hata kama atashindwa kucheza
mechi yoyote Arsenal.
Mchezaji huyo aligundulika kuvunjika mfupa wa
mgongo, lakini kwa presha ya siku ya mwisho ya kufunga usajili, Wenger
aliamua kufanya usajili wa kiungo huyo licha ya kwamba madaktari
walimwambia kuwa ni mgonjwa.
Madaktari wa Arsenal waliompima staa huyo walimpa
taarifa Wenger kwamba staa huyo amevunjika moja ya mifupa mgongoni
wakati walipomfanyia uchunguzi huo Ijumaa iliyopita.
Lakini, Wenger aliyepitisha usajili wake na juzi
Jumapili alikiri kwamba ameamua kumnasa mchezaji huyo mwenye umri wa
miaka 31 na atakuwa kikosini kwake hata kama hatacheza mechi yoyote
Arsenal hadi mwisho wa msimu.
Kallstrom atakakuwa nje ya uwanja kwa kipindi
ambacho kinatajwa kuwa ni wiki sita, klabu yake ya zamani ya Spartak
Moscow ndiyo itakayokuwa ikimlipa mshahara na baada ya hapo litakuwa
jukumu la Arsenal.
Wenger alisema: “Nina hakika kama umewahi kucheza
mpira, lazima uliwahi kucheza huku sehemu moja ya mfupa ikiwa imevunjika
kidogo. Huwezi kujijua. Mimi nililiwaza hilo lakini nilifikiria zaidi
kumaliza dili. Hawa Spartak watamlipa mshahara wake kwa wiki sita,
lakini matarajio yangu atakuwa nje kwa wiki nne hadi sita. Acha hili
lipite tutajua mwisho wa msimu kama tulikuwa sahihi au tulikosea.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!