Siku kama ya leo miaka 1430 iliyopita
alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na
Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa
watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la
Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za
watawala dhalimu na jahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya
kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na
mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya
Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi
ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko
Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji
wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume
walivyodhulumiwa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran ya Kiislamu
siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekea kama 'Siku ya Wauguzi'.
************************************************************
Siku kama hii ya leo miaka 740 iliyopita
alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas. Alizaliwa
mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo
hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua
kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za
kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama
alivyo kuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu
kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile
aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya
viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli. Itikadi za Aquinas na
misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa
vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.
************************************************************
Na siku kama ya leo miaka 63 iliyopita
inayosadifiana na tarehe 16 Esfand 1329 Hijria Shamsia, aliuawa Ali
Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara
aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na
mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi.
Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi,
ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na
kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!