Jose Mourinho tena! Kwa mara nyingine katika ubora wake wa
kuzungumza, amejaribu kuiaminisha dunia kile ambacho ni vigumu kwa watu
wengine kukiamini na kukifikiria.
Bosi huyo wa Chelsea amesisitiza kwamba wapinzani
wake katika Ligi Kuu England, Manchester City na Arsenal, wana nafasi
kubwa ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuziondoa
Barcelona ya Hispania na Bayern Munich ya Ujerumani.
Arsenal ilichapwa 2-0 na Bayern Munich katika
uwanja wao wa nyumbani, Emirates, wiki mbili zilizopita huku Manchester
City nao wakipoteza kwa idadi hiyo hiyo ya mabao pia nyumbani kwao,
Etihad.
Hata hivyo, huku mashabiki wa timu hizo pengine na
mashabiki wengine wa soka duniani wakiamini kwamba Arsenal na Man City
hazina nafasi ya kusonga mbele, Mourinho anaamini kuwa timu hizo zina
nafasi nzuri ya kutinga robo fainali.
“Man City haiwezi kuishinda Barcelona? Barcelona
mbona ilipoteza kwa Valladolid, ilipoteza nyumbani pia mbele ya
Valencia. Sasa kwanini isiweze kufungwa tena?” Alihoji Mourinho kwa
kujiamini.
“Arsenal kwa Bayern inaweza kushinda 2-0 na kwenda dakika za nyongeza. Ngumu. Inaonekana ngumu sana, lakini nakwambia wanaweza.”
Wakati Mourinho, kocha mwenye maneno mengi,
akiwapa moyo Arsenal na Man City, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger,
amedai kwamba mchezaji wake ghali zaidi katika historia ya Arsenal,
Mesut Ozil, amerudi upya na ataonyesha ubora wake katika pambano dhidi
ya Bayern.
Ozil alifunga bao moja na kupika mengine mawili
wakati Arsenal ilipoichapa Everton Jumamosi na kutinga nusu fainali ya
Kombe la FA.
“Alikuwa na hisia kwamba ameiangusha timu katika
mechi muhimu, hilo liliathiri sana kiwango chake. Maumivu ya
kisaikolojia ni makali kama yalivyo maumivu ya mwili. Inahitaji muda
kuweza kuyaponya,” alisema.
Wakati Arsenal ikiwa wageni wa Bayern, katika
mechi nyingine za leo Jumanne, Atletico Madrid itaikaribisha AC Milan
baada ya pambano lao la awali kumalizika kwa sare ya 1-1 jijini Milan,
Italia.
Kesho Jumatano achilia mbali pambano la Barcelona
na Man City, Paris St Germain itakuwa nyumbani kuikaribisha Bayer
Leverkusen baada ya kuwapiga Wajerumani hao mabao 4-0 wakiwa ugenini
wiki mbili zilizopita.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!