Novemba 29, 1987, Kocha Alex Ferguson alipiga hodi
nyumbani kwao Ryan Giggs ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 14. Kazi
ilikuwa ni moja tu, kumshawishi mzazi wa mchezaji huyo.
Giggs amepewa ukocha wa muda, anayetarajiwa kuchukua
nafasi hiyo ni Louis van Gaal raia wa Uholanzi. Lakini mjadala uko hivi, kwamba
Giggs anaweza kuendelea kuwa kocha wa Manchester na kuifanya iendelee kushinda?
Ferguson alitaka kumshawishi mama Giggs kwamba mwanaye
ahame kutoka katika timu ya watoto ya Manchester City na kujiunga na ile ya
Manchester United ambayo ndiyo alikuwa ameifundisha kwa mwaka mmoja tu tangu
ajiunge nayo akitokea Aberdeen.
Uamuzi huo ulitokana na Giggs kufunga mabao matatu
‘hat trick’ katika mechi ya timu yake ya watoto chini ya miaka 15 ya Salford
Boys dhidi ya Manchester United. Ferguson akamchukua mtaalamu wa vipaji Joe
Brown na kuongozana naye hadi kwao kumshawishi mama yake.
Wakati Ferguson akifanya kazi ya kumshawishi mama
Giggs, mshambuliaji nyota wa Manchester United, Wayne Rooney alikuwa na umri wa
miaka miwili. Sasa wawili hao wamepita hatua mbili za maisha, mchezaji na
mwenzake na sasa mchezaji na kocha wake!
Hii inaonyesha dunia ya soka ina mengi lakini kivutio
zaidi, kwani Giggs leo amechukua nafasi ya Ferguson ambaye wakati huo alivutiwa
naye kama mchezaji na kwenda kumshawishi ajiunge na Man United ambayo
ameichezea mechi 962, si mchezo.
Gumzo ni kufukuzwa kwa Kocha David Moyes aliyerithi
nafasi ya Ferguson halafu akaboronga kupindukia, sasa amepewa Giggs ambaye ni
kocha wa muda lakini ameanza kazi vizuri kwa ushindi wa mabao 4-0 na Rooney
akipiga mabao mawili.
Maana anaweza kuifanya icheze kwa staili ile ya
Ferguson ambayo Wa-man United wanaona ndiyo sahihi, tena kitu kizuri kwenye
benchi la ufundi yuko na Manchester wa kweli waliopewa jina la “Class of 92”
ambao ni Paul Scholes, Phil Neville na Nicky Butt.
Class of 92 kuiongoza Man United, unaweza kusema
inaongozwa na vijana au watoto wa Ferguson ambao hakuna ubishi kwa asilimia
zaidi ya 60, watatumia mbinu au mifumo iliyokuwa akiitumia kocha huyo wakati akiwafundisha
tokea timu za chini hadi timu kubwa wakiwa makinda hadi walipofikia kuitwa
wakongwe na wengine wakaondoka.
Kumbuka Ferguson aliwahi kumtandika Giggs kofi mbele
ya mpenzi wake pamoja na wenzake wakiwemo Scholes, Neville, Butt na David
Beckham, Giggs alipowaalika wenzake hao kwake na kelele za muziki zikawaudhi
majirani ambao walimpigia kocha huyo na kumueleza “watoto wako wanatubughudhi”.
Maana yake Giggs anaijua zaidi kazi ya Ferguson ambaye
amefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka 20, lakini ana watu wanaomsaidia na
wanaoijua Man United. Wanaoweza kufanya mambo yaende vizuri.
Sahihi kumuacha Giggs aendelee baada ya kushinda mechi
moja iliyozaa mabao manne na pointi tatu? Kama wakimuachia timu, litakuwa ni
kosa moja, tena kubwa, hilo ndilo jibu.
Si kwamba Norwich ni dhaifu hapana, lakini Man United
ni kubwa kumuachia Giggs katika kipindi hiki. Badala yake anatakiwa kocha mwenye
jina kubwa, uwezo na uzoefu zaidi mfano wa van Gaal.
Kuwa na mtu kama van Gaal, bado kutaongeza heshima na
mvuto wa Man United na kusaidia wachezaji wengine nyota kutoka sehemu
mbalimbali kuamini Man United ni sehemu sahihi ya kwenda ambayo wanaweza kufanya
kazi.
Kumuacha Giggs awe kocha kutajenga hofu na ikitokea
akakosea na kutimuliwa, pia kutajenga hofu kwa wenzake hasa Class of 92 ambao
kuwapunguza morali kipindi hiki ni sawa na kuitupia United kaburini. Lakini ni
vizuri kutomuondoa Giggs katika nafasi ya kocha msaidizi.
Moyes alikosea kuliondoa benchi lote la ufundi
lililokuwa chini ya Ferguson na kuleta watu wake, kama van Gaal akipata kazi,
asifanye kosa kama hilo kwa kuwa anamhitaji Giggs na Class of 92. Hawawezi
kumshinda kwa kuwa aliwahi kuwa bosi wa Jose Mourinho wakiwa Barcelona na
wakafanya kazi vizuri kabisa.
Giggs amekuwa kocha ambaye ameweka rekodi mbili za
haraka siku chache tu baada ya kuchukua nafasi yake hiyo kwa muda.
Moja ni kuonyesha anapendwa zaidi kuliko kocha
mwingine yeyote baada ya makocha wawili waliokaa muda mrefu zaidi ambao ni
Ferguson na Matt Busby aliyeifundisha Man United kuanzia Oktoba Mosi 1945 hadi
Juni 4, 1969, kabla ya kurudi na kuinoa kwa mwaka mmoja na ukawa ndiyo mwisho
wake na United.
Rekodi ya pili aliyoweka Giggs ni kuwa mtu wa kwanza
mwenye asili ya Bara la Afrika kuinoa klabu hiyo, haijawahi kutokea.
Asili ya Giggs ni nchini Sierra Leone barani Afrika
ingawa mama yake ni raia wa Wales na kwa kuwa alizaliwa nchini humo, moja kwa
moja amekuwa raia wa huko.
Wakati akiwa mwanafunzi, Giggs ni kati ya wachezaji
ambao wamesimulia mengi mabaya waliyokutana nayo kutokana na ubaguzi wa rangi
ingawa umaarufu na muonekano wake umekuwa si rahisi watu wengi kugundua kuwa
ana asili ya Afrika ambako mpira umezaliwa.
Kombe la Dunia la Klabu (1): 2008
REKODI ZA GIGGS NA PREMIER LEAGUE:
•Ana rekodi ya kubeba makombe yote 13 iliyoshinda Man
United wakati wa Ferguson.
•Amecheza mechi nyingi zaidi za ligi hiyo kuliko
mwingine, amecheza mechi 611.
•Ndiye mchezaji aliyetoa pasi nyingi zaidi zilizozaa
mabao katika ligi hiyo.
•Mchezaji pekee aliyecheza misimu 22 mfululizo ya ligi
hiyo bila kukosa hata mmoja.
•Mchezaji pekee aliyefunga mabao katika ligi ya
Premiership kwa misimu 21 mfululizo.
•Mchezaji aliyeanza mechi 794 za kikosi cha kwanza cha
United.
•Mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 kwa Man United.
•Kiungo wa pili kufunga mabao 100 Premiership baada ya
Matt Le Tissier.
REKODI ZA GIGGS NA LIGI YA MABINGWA:
•Amecheza misimu 17 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia
akiwa amecheza misimu 11 mfululizo. Anazidiwa na Raul Gonzalez tu aliyecheza
mfululizo mara 14.
•Mwingereza aliyecheza mechi nyingi zaidi za Ligi ya
Mabingwa Ulaya.
•Akiwa na umri wa miaka 37 na siku 289, aliweka rekodi
ya kuwa mkongwe kufunga bao Ligi ya Mabingwa Ulaya, Man United ilipocheza na
Benfica, Septemba 14, 2011.
MAKOMBE YA GIGGS NA UNITED:
Premier League (13): 1992–93, 1993–94, 1995–96,
1996–97, 1998–99, 1999–2000, 2000–01, 2002–03, 2006–07, 2007–08, 2008–09,
2010–11, 2012–13
Kombe FA (4): 1993–94, 1995–96, 1998–99, 2003–04
Kombe la Ligi: (4): 1991–92, 2005–06, 2008–09, 2009–10
Ngao ya Jamii ya (9): 1993, 1994, 1996, 1997, 2003,
2007, 2008, 2010, 2013
Ligi ya Mabingwa Ulaya (2): 1998–99, 2007–08
Super Cup ya Uefa (1): 1991
Kombe la Intercontinental (1): 1999
Rekodi ya Class of 92 wanaoiongoza Man United sasa
Phil Neville – Alijiunga United 1992
Mechi: 386
Makombe:
Ligi ya Mabingwa (1)
Premier League (6)
Kombe la FA (3)
Nicky Butt - Alijiunga United 1991
Mechi: 387
Makombe:
Ligi ya Mabingwa (1)
Premier League (6)
Kombe la FA (3)
Paul Scholes - Alijiunga United 1991
Mechi: 718
Makombe:
Ligi ya Mabingwa (2)
Premier League (11)
Kombe la FA (3)
Kombe la Ligi (2)
Ryan Giggs - Alijiunga United 1987
Mechi: 962
Makombe:
Ligi ya Mabingwa (2)
Premier League (13)
Kombe la FA (4)
Kombe la Ligi (4)
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!