Bunge la waakilishi nchini Burundi,limepitisha mswada unaodhamiria kupunguza ongezeko la makanisa nchini humo.
Utafiti wa serikali uliofanywa mwaka jana, ulipata madhehebu 557 ya waumini wa kikristo wanaofanya ibada zao nchini humo.Sheria hiyo mpya itahitaji makanisa kuwa tu na waumini 500 pamoja na jengo nzuri linalotumiwa kama kanisa.
Makanisa ya kiivanjelisti, yalianza kuongezeka kabla na baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilimalizika 2005 ambapo karibu watu 300,000 waliuawa.
Mswada huo uliungwa mkono na wabunge wote katika bunge la waakilishi na huenda usipingwe utakapowasilishwa kwa baraza la Senate.
Ikiwa hautafanyiwa mabadiliko yoyote, mswada huo utahitajika kutiwa saini na Rais ishara ya kuudhinisha na kuufanya sheria mpya katika siku 30, la sivyo urejeshwe kwa bunge la waakilishi kurekebishwa.
Pindi itakapotiwa saini, makanisa yatapewa mwaka mmoja kufuata sheria hiyo na masharti mapya.
Kwa kanisa la kigeni kusajiliwa , lazima wamiliki kuonyesha kuwa iliwahi kuwa na waumini 1,000.
Ni jambo la kawaida kuona waumini wakiwa wamepiga kambi kando ya barabara katika mahema wakifanya ibada siku za Jumapili.
Mtu yeyote anaweza kujitangaza kama muhubiri na kumekuwa na kashfa kadhaa zikihusisha kanisa ndogo ndogo.
Baadhi ya wahubiri wametuhumiwa kwa kuwanyanyasa waumini.
Kuna kisa kimoja ambapo muhubiri aliwaambia wanawake wasio na uwezo wa kushika mimba kulala naye ili awazalishe.
Idadi kubwa ya watu nchini Burundi ni wakristo, wakati wengine wanafuata itikadi za kitamaduni.
Wakati wa mjadala kuhusu swala hilo bungeni, mbunge mmoja kwa jina Jean Minani, aliwatakia waumini wenye imani ambazo sio za kidini kuruhusia kuabudu watakavyo.
Lakini waziri wa mambo ya ndani alipuuza imani hizo na kuzitaja kama za kijadi na zisizokubalika.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alichaguliwa kama Rais mwaka 2005 na ni mlokole huku mkewe akiwa muhubiri katika kanisa la kiivanjelisti.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!