PATI la mastaa watupu. Fikiria hapa kuna Eden Hazard, Robin van Persie, Wayne Rooney, Andres Iniesta, Lionel Messi, Radamel Falcao kule kuna Alexis Sanchez, Jozy Altidore, Shinji Kagawa, Mesut Ozil, Xherdan Shaqiri, Claudio Marchisio; hao ni baadhi tu. Halafu wataandamana na mademu wao.
Unadhani patakuwaje hapo Brazil mwakani, nchi
yenye fukwe za maana. Hii ni kwenye fainali za Kombe la Dunia
zitakazoanza Juni 12 mwakani. Supastaa Neymar atakuwa mwenyeji wao
kwenye fainali hizo wakati atakapovaa jezi ya Brazil. Kwa mastaa kama
Iniesta, Kagawa na Marchisio wameonja mazingira ya Brazil yalivyo baada
ya miezi michache iliyopita kuwapo kwenye ardhi hiyo katika michuano ya
Kombe la Mabara.
England baada ya kwenda Brazil kucheza mechi ya
kirafiki na timu ya nchi hiyo, iliporudi kwao hadithi zilikuwa kile
walichokiona kwenye fukwe za Kibrazili na baada ya kufuzu fainali za
Kombe la Dunia za mwakani, kitu cha kwanza mashabiki wao kuulizia ni
gharama za kuishi Copacabana.
Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil
mwakani zimepata mvuto wa aina yake baada ya mataifa mengi makubwa na
yenye nguvu kisoka kufuzu. Jambo hilo litavuta watazamaji wengi
kushuhudia mikiki mikiki hiyo.Uwepo wa mataifa makubwa kwenye fainali
hizo ndicho kitu kinachotoa imani kwamba ushindani utakuwa mkubwa na
mashabiki duniani kote watapata fursa ya kushuhudia soka yenye hadhi
kubwa.
Nchi zilizofuzu kwenda Brazil
Timu 32 ndizo zitakazoshiriki michuano hiyo,
lakini hadi sasa ni 21 tu ndizo zilizofuzu. Kwenye Bara la Ulaya, tayari
nchi tisa zimeshafuzu moja kwa moja na nne zinasubiri kucheza mchujo
ili kupata idadi ya timu 13 zitakazofuzu kutoka barani humo.
Ubelgiji, Italia, Ujerumani, Uholanzi, Uswisi,
Urusi, Bosnia, England na Hispania. Timu hizo zitaungana na timu nne
nyingine zitakazopatikana baada ya mechi ya mchujo utakazohusisha timu
za Croatia, Sweden, Romania, Iceland, Ureno, Ukraine, Ugiriki na
Ufaransa.
Amerika Kusini; Brazil wamefuzu
moja kwa moja kwa sababu ya kuwa wenyeji, wakati nchini nyingine kutoka
bara hilo ni pamoja na Argentina, Colombia, Ecuador na Chile. Kwenye
orodha hiyo kuna timu moja hapo imekosekana ambayo itasubiri kucheza
mchujo wa mechi itakayohusisha na bara lingine.
Ili kukamilisha idadi kamili ya timu zitakazofuzu
kupitia bara hilo, Uruguay italazimika kucheza mechi na Jordan kutoka
Bara la Asia ili kupata tiketi moja iliyobaki.
Kwa upande wa Amerika Kaskazini na Kati; Marekani,
Costa Rica na Honduras zimefuzu moja kwa moja, wakati Mexico
italazimika kucheza na New Zealand ili kufuzu, kinyume cha hilo, basi
mastaa kama Javier Hernandez ‘Chicharito’ na Giovani Dos Santos watakuwa
miongoni mwa wachezaji watakaokosekana.
Japan, Australia, Iran na Korea Kusini zenyewe
muda mrefu tayari zilishafuzu fainali hizo, wakati Bara la Afrika hadi
kufika mwishoni mwa Novemba timu tano zitakazowakilisha bara zitakuwa
zimepatikana.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!