MATAJIRI wawili wenye hamasa kubwa kwa mashabiki wa Simba na Yanga, Zacharia Hanspoppe (Simba) na Yusuph Manji (Yanga) jana Jumapili walionyesha ubabe kwa muda kwa kucheza na akili za mashabiki wao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea wakati wa kuanza kwa mchezo,
mapumziko na dakika za mwisho lakini kishabiki Hanspoppe alionekana
kumzidi kete Manji kwavile timu yake ilimkomboa kwa kuchomoa mabao na
kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Wakati mpira unaanza Manji ambaye ni Mwenyekiti wa
Yanga aliingia uwanjani hapo akiambatana na makamu wake, Clement Sanga
na kabla hawajakaa, Manji alizunguka akihamasisha mashabiki kuhesabu
vidole vitano akimaanisha Yanga ingeshinda kwa mabao matano kitendo
ambacho kilishangiliwa na mashabiki wa Yanga.
Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Usajili wa
Simba, alipoona hivyo alisimama na kuwahamasisha mashabiki wa Simba na
kuwaonyesha ishara ya mabao matatu na kuwaambia watulie.
Hata hivyo hadi mapumziko Yanga walikuwa
wanaongoza kwa mabao 3-0 jambo ambalo lilimpa kiburi Manji na wakati wa
mapumziko akahamasisha tena mashabiki wake akimaanisha goli zilezile
tano.
Lakini upepo ukambadilikia kipindi cha pili timu
yake iliporuhusu mabao yote matatu yakarudi ndipo Hanspoppe akainuka na
kuanza kutamba tena huku Manji na Yanga wote wakanywea kwa kutoamini
kilichotokea.
Mpaka mchezo unamalizika Yanga walikuwa wamenywea
huku Simba wakiongozwa na Hanspoppe walikuwa wakishangilia sare hiyo
ambayo ni kama ushindi kwa vile walichomoa bao zote na kuwaacha Yanga
midomo wazi.
Baada ya mchezo huo Yanga walinywea mitaani huku Simba wakizunguka wakipiga kelele kwa mbwembwe nyingi kama wametwaa ubingwa.
Jijini la Dar es Salaam lilikuwa limezizima kwa
kelele za mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakishangilia kwa kutumia
honi za magari, mavuvuzela na maneno ya kebehi.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!