UKIFUNGUA simu ya Mesut Ozil utakutana na meseji za Jose Mourinho. Zipo nyingi, japo Ozil ameamua kuiweka hadharani meseji moja, inayosomeka kwa kimombo ‘Welcome to London’ kwa maana ya ‘karibu London’.
Meseji nyingine walizotumiana wawili hao ni siri
yao. Ozil amesema hivyo. Haijulikani kama Mourinho anatuma meseji za
aina gani kwa Ozil hasa kwa kipindi hiki anachoonyesha uwezo mkubwa wa
soka katika klabu yake mpya ya Arsenal.
Kiungo huyo Mjerumani, Ozil msimu huu ameuanza kwa
kasi kubwa akiwa ndani ya jezi za Arsenal baada ya kujiunga katika
dakika za mwisho za siku ya kufunga usajili akitokea Real Madrid, mahali
ambako alikuwa pamoja na kocha Mreno, Mourinho.
Mourinho mambo yake hayapo vizuri sana katika
klabu yake ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England na huwezi kujua nini
mpango wake wa Januari mwakani baada ya mwaka huu kumkosa straika
aliyekuwa akimwinda kwa nguvu zote, Wayne Rooney.
Ozil amesaini mkataba mrefu ndani ya Arsenal,
lakini kwa mchezaji wa kariba yake ni lazima kikosi hicho cha Arsene
Wenger kihakikishe kwamba hakitoki kapa kwenye kutwaa mataji kwa misimu
isiyozidi miwili, vinginevyo kila kitu kitakuwa tofauti.
Mourinho ni kocha mwenye nguvu sana na si mtu
anayemtakia mema Wenger baada ya kuzuia uhamisho wa straika Demba Ba
katika dakika za mwisho, alipogundua Mfaransa huyo amemnasa kiungo mkali
wa pasi fupi za mwisho, Ozil.
Jose amtumia meseji, Ozil afanya siri
Kuna kitu kinatia wasiwasi juu ya meseji
wanazotumiana Mourinho na Ozil kwa sababu staa huyo wa Ujerumani
anafanya siri licha ya kwamba si jambo zuri kutaka kufahamu ni kitu gani
wanachozungumza wawili kwa sababu ni mambo binafsi.
Mourinho kiukweli ana wivu kwa kumwona Ozil
akifanya mambo kwenye kikosi cha Arsenal, inayonolewa na kocha ambaye
daima hawakuwa na uhusiano mzuri tangu awamu ile ya kwanza aliyokuwa
Chelsea hadi sasa aliporejea tena kwenye klabu hiyo ya Stamford Bridge.
“Ndiyo, kuna mambo tunawasiliana. Alinitumia SMS
akisema ‘karibu London’,” alisema Ozil alipozungumza na gazeti la Bild
la Ujerumani.
Hata hivyo, baadaye akasema “mengine yanatuhusu
wenyewe,” wakati alipoulizwa swali ni meseji za aina gani anazotumiwa na
kocha wake huyo wa zamani katika Uwanja wa Santiago Bernabeu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!