SIKU chache baada ya Fifa kuitaka Klabu ya TP Mazembe iwaruhusu wachezaji watatu wa Zambia kuiwakilisha timu yao ya Taifa, Mazembe wameonyesha jeuri ya fedha kwa kuwatumia ndege wachezaji hao.
Awali Fifa walitoa onyo kwa klabu hiyo ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwataka iwaruhusu, Rainford Kalaba,
Stopilla Sunzu na Nathan Sinkala kujiunga na timu ya Taifa ya Zambia kwa
ajili ya mechi yao na Brazil hapo kesho Jumanne.
Jeuri hiyo ya fedha imekuja baada ya Mazembe kudai
kuwa isingewaruhusu wachezaji hao kwenda Brazil kwa kuwa walikuwa
wagonjwa na hivyo wasingeweza kuiwakilisha Zambia.
Alhamisi iliyopita, Daktari wa Mazembe, Tahar
Messaoud, alisema kwamba Kalaba na Sinkala wanasumbuliwa na malaria
wakati, Sunzu ana matatizo ya goti aliyoyapata wakati akiiwakilisha timu
hiyo katika mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la CAF dhidi ya
Stade Malien ya Mali. Taarifa za daktari huyo zilisababisha Chama cha
Soka Zambia (FAZ) kuomba Fifa waingilie kati suala hilo na kuwashutumu
Mazembe kwa taarifa za uwongo kuhusu maradhi ya wachezaji hao.
“Tungependa kuwaarifu wadau wa soka kwamba
tumepata taarifa kutoka Fifa ambao wamewaonya TP Mazembe kwa kupuuza
taratibu zinazohusu kuwaruhusu wachezaji kushiriki mechi za
kimataifa,’’ alisema Meneja Uhusiano wa FAZ, Erick Mwanza.
Mazembe walikuwa na mechi muhimu dhidi ya Malien
na inadhaniwa kwamba hiyo ndiyo sababu ya kutunga habari hiyo ya
kuwazuia wachezaji hao. Katika hatua nyingine, beki wa Morocco,
Abderrahim Achchakir aliyefungiwa mwaka mmoja na Fifa kwa kosa la
kumzonga mwamuzi katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2014 dhidi ya
Tanzania amekata rufaa katika mahakama ya masuala ya kimichezo.
Mahakama ya michezo ilibainisha Alhamisi iliyopita
kwamba rufaa ya beki huyo itasikilizwa Novemba 5 mwaka huu. Achchakir
alimzonga mwamuzi Helder Martins de Carvalho kutoka Angola na
kusababisha kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliomalizika kwa
Tanzania kushinda mabao 3-1 jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!