HISIA mbalimbali zimezidi kuibuka miongoni mwa
Wakenya kufuatia picha zenye utata za mwakilishi wa wanawake pamoja na
seneta wa kaunti ya Nairobi, zinazoendelea kusambazwa kupitia mitandao
ya kijamii.
Wakenya walitumia umahiri wao wa
kimtandao kwa kutuma jumbe na hata kutumia vibonzo vinavyowasawiri
viongozi hao kwa njia ya kuwakebehi na kuwasuta Huku hayo yakijiri, mwakilishi wa
wanawake katika kaunti ya Nairobi na ambaye amekuwa akigonga vichwa vya
habari huku akiandamwa na kashfa moja baada ya nyingine, ameendelea
kusalia kimya huku picha zake zinazolenga kumuumbua zikizidi kusambazwa
kupitia mitandao ya kijamii katika siku za hivi majuzi.
Kusambazwa kwa picha kupitia ulingo wa mitandao ya kijamii kumeibua kashfa mpya dhidi ya viongozi hao wawili wa Nairobi.
Picha hizo ambazo zimekuwa
zikienezwa kupitia mitandao ya kijamii zinawasawiri Bi Shebesh na Mike
Mbuvi kama walio zaidi ya wandani wa kisiasa.
Katika mahojiano yaliyofanyika hivi
majuzi, Mike Mbuvi, ambaye ni seneta wa Nairobi na aliye maarufu kama
'Sonko’, alidai kuwa picha hizo si za kweli na kwamba zilikuwa
zimefanyiwa ukarabati kielektroniki.
Alipoulizwa iwapo picha hizo
zitazua hoja ya uadilifu dhidi ya wawili hao, seneta alisema picha hizo
hazingewaathiri kwa vyovyote kama viongozi wa Nairobi.
Hata hivyo, alikiri kwamba wawili hao wamekuwa na tofauti za kibinafsi.
Kofi
Katika kisa cha kwanza, Gavana wa
Nairobi, Evans Kidero alidaiwa kumzaba kofi Shebesh katika malumbano
kuhusiana na wafanyakazi wa kaunti walikuwa katika mgomo.
Siku chache baadaye, Sonko na Bi
Shebesh wanadaiwa kukabiliana katika hoteli mojawapo Nairobi na pia
katika majengo ya bunge ambapo Sonko anadaiwa vilevile kumzaba kofi Bi
Shebesh.
Alikijibu kuhusiana na mafarakano
yake na Bi Shebesh, Sonko alinukuliwa kusema kwamba matukio hayo ni
sehemu ya “changamoto nyingi” zinazoambatana na maisha na uongozi.
“Hata wewe wakati mmoja au mwingine
umewahi kutofautiana na dadako. Kutofautiana ni changamoto ambalo
halikumbi magari au miti; huwakumba binadamu na lilinikabili mimi,”
Sonko alinukuliwa akisema.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!