Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe |
Nchi hiyo wa Kusini mwa Afrika
ilitia saini Mkataba wa Roma, ambao uliibuni ICC, lakini haijauidhinisha
kisheria, hali inayomaanisha kuwa haidhibitiwi na maamuzi ya mahakama
hiyo.
Waziri wa Haki Bw Emmerson Mnangagwa
mnamo Alhamisi aliilaumu ICC kwa kuwalenga viongozi wa Kiafrika, huku
ikikosa kuwachukulia hatua viongozi wa Kimagharibi.
“Historia imetufunza kuwa ukoloni
ulikuwa mataifa ya bara Uropa kututawala,” akasema. “Sasa inatuhitaji
tena kwenda katika nchi zizo hizo kushtakiwa huko, na waliokuwa wakoloni
wetu. Hilo haliwezekani,” akaeleza waziri huyo.
“Hatujadiliani hata kuhusu Mkataba huo (wa ICC). Sidhani kuwa unaweza kupata uungwaji mkono wowote nchini humu,” akaeleza.
Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wa
Rais Mugabe wamekuwa wakisema amekuwa akikataa kung’atuka uongozini
kutokana na hofu kuwa huenda akatolewa kibali cha kukamatwa na mahakama
hiyo kutokana na madai ya dhuluma za haki za kibinadamu.
Bw Mnangagwa alisema kuwa Zimbabwe ilitaka Afrika 'kusimama kidete na kupinga’ ubaguzi wa ICC dhidi ya bara la Afrika.
“Viongozi wa Kimagharibi huwa
hawaulizwi, hali iliyo kinyume barani Afrika, angalia nchini Kenya,
wanawachukua Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, ambao walichaguliwa na
Wakenya, na kuwataka kuskizwa kwa kesi (Mjini The Hague),” akasema.
Rais Kenyatta na naibu wake William
Ruto wanakabiliwa na kesi katika mahakama hiyo kwa madai ya kuhusika
katika ufadhili wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, ambapo watu
zaidi ya 1,000 waliuawa.
Kongamano hilo la AU linaanza mnamo Ijumaa, ambapo Rais Mugabe, ambaye amekuwa akiipinga ICC anatarajiwa kuhudhuria.
Bush
“Kwa sasa tumegundua kuwa hicho
ndicho chombo ambacho kimekuwa kikitumiwa dhidi ya viongozi wa Kiafrika
kinyume na wahalifu kama George Bush (aliyekuwa Rais wa Amerika) na Tony
Blair (aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza),” akaeleza waziri huyo.
“George Bush aliivamia Iraq kwa
visingizio vya kuwepo kwa silaha za maangamizi ya halaiki, na ningali
siamini kuwa mashirika ya kijasusi ya CIA na FBI hayakujua kuwa hakukuwa
na silaha hizo. Walitumia hilo kama hadaa ya kuhalalisha uvamizi wao,”
akasema.
“Walimnyonga Saddam Hussein
baadaye…tukio sawia na lililomfanyikia aliyekuwa kiongozi wa Libya,
Muammar Gaddaffi, aliyeuawa na magenge yayo hayo kwa sababu tu mataifa
hayo yana mafuta na hakuna yeyote anawachukulia hatua za kisheria George
Bush au Tony Blair, ama viongozi wengine walioendesha dhuluma kama
hizo,” akaeleza.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!