BAADA ya mechi kumalizika, David
Moyes, aliulizwa swali moja tu linalomhusu, Shinji Kagawa. Ni mahali
gani Mjapani huyo amecheza kwa ubora wake, kushoto au katikati?
Sikia alichojibu kocha huyo wa Manchester United: “Nadhani anakuwa bora mpira unapokuwa kwenye miguu yake.”
Hakika, kiungo huyo mchezeshaji alilithibitisha
hilo usiku wa juzi Jumanne. Huyu ndiye Kagawa ambaye Manchester United
inayomtaka.
Kagawa alipokosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi
hicho kuliibuka uvumi kwamba staa huyo anaweza kurejea katika klabu yake
ya zamani, Borussia Dortmund.
Lakini katika mechi dhidi ya Real Sociedad,
Mjapani huyo alicheza kwa ubora mkubwa utakaowafanya Manchester United
wawe na sababu ya kumbakiza Old Trafford kiungo huyo.
Alivyotawala uwanja
Alianzishwa upande wa kushoto kwenye safu ya
washambuliaji watatu na kucheza nyuma ya straika Javier Hernandez,
lakini huduma yake ilikuwa ya uwanja mzima.
Kagawa alimfanya beki wa kushoto, Patrice Evra,
kutopata usumbufu wowote kutoka kwa wapinzani na mara kadhaa
alimrahisishia kazi Mfaransa huyo kwa kupandisha mashambulizi bila ya
wasiwasi.
Katika kipindi cha pili, Wayne Rooney,
alipotolewa, Kagawa alipata nafasi ya kuingia kati na kucheza nyuma ya
straika. Mahali hapo aliichambua ngome ya Sociedad mara kadhaa na pasi
zake zingeweza kuipa bao Manchester United kama si washambuliaji wake
kukosa umakini.
Mfano mzuri ni kwenye dakika ya 69, Kagawa alipiga pasi kali ya kisigino kwa Ashley Young iliyosababisha hatari huku Robin Van Persie akikosa nafasi kadhaa zilizopikwa na staa huyo.
Hakika Kagawa alikuwa kwenye ubora wake usiku huo na kwamba wachezaji wenzake ndio waliomwangusha.
Kagawa na Evra waligongeana pasi 20, pasi 12 zilitoka kwa Evra kwenda kwa Kagawa na nane zilitoka kwa Mjapani hadi kwa Mfaransa.
Moyes apata ujumbe
Kitendo cha kupata namba katika mchezo huo, Kagawa
alitumia nafasi hiyo kuonyesha ubora ambao utamfanya kocha wake kuona
kitu ambacho Mjapani huyo anaweza kukifanya kwenye kikosi chake.
Kagawa alicheza kwa kiwango kikubwa, aliing’arisha Manchester United wakati mastaa wengine wa timu hiyo; Rooney, Hernandez na Van Persie wakiwa kwenye kiwango kibovu uwanjani.
Kwa kiwango alichocheza Kagawa dhidi ya Sociedad,
hakika kitakuwa kimetuma ujumbe muhimu kwa Moyes na huenda kocha huyo
akafikiria kumjumuisha kwenye kikosi chake cha Jumapili ijayo kwenye
Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal.
Moyes ni kama alivyokuwa mtangulizi wake wa Old Trafford,
Sir Alex Ferguson, kwamba anapenda kumtumia Rooney nyuma ya
mshambuliaji wa kati, lakini sasa anaweza kukoshwa na kile
kilichoonyeshwa na Kagawa.
Staa huyo wa zamani wa Borussia Dortmund
ameonyesha jinsi anavyoweza kuutawala uwanja na soka lake si kwamba tu
limemkosha Moyes, bali limewaburudisha wafuasi wengine wa soka la kushambulia.
Kiwango cha kiuchezaji kilichoonyeshwa na Kagawa
ni viungo wachache sana wanaweza kufanya kutawala sehemu kubwa ya uwanja
na hakuna shaka kwamba Moyes hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya
kumuanzisha staa huyo kwenye mechi isiyotumia nguvu nyingi kama Arsenal.
Uwepo wa Kagawa uwanjani unaifanya Manchester
United kuwa na wigo mpana wa kubadili aina ya mchezo wake na jinsi ya
kupanga mashambulizi na itakuwa faida kubwa kwa Moyes kama atamuanzisha
nyuma ya mshambuliaji wa kati na Rooney akashambulia kutokea kushoto.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!