MANCHESTER United imeitia adabu Arsenal kwa kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford jana Jumapili, shukrani kwa bao la kichwa na straika Robin van Persie katika kipindi cha kwanza.
Mdachi huyo alifunga katika dakika 27 na kuzima
tambo za Arsenal huku Kocha David Moyes akimtambia mpinzani wake Arsene
Wenger kutokana na kushindwa kumaliza uteja wa kuchapwa na Mashetani
Wekundu.
Kichapo hicho kimeipunguza kasi Arsenal na sasa pengo la pointi dhidi yake na Manchester United limekuwa pointi tano.
Ushindi huo sasa umeifanya Manchester United
kupanda kutoka nafasi ya nane hadi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada
ya kufikisha pointi 20 na sasa kuwa na uhakika wa kuendelea kuwamo
kwenye mbio za kutetea ubingwa wao, huku Van Persie akiiua tena timu
yake ya zamani baada ya kufanya hivyo msimu uliopita kwenye ushindi wa
2-1 kwenye uwanja huo huo wa Old Trafford.
Kwenye kipindi cha kwanza, Arsenal ilionekana
kubanwa na kuchapwa bao hilo kabla ya kipindi cha pili kuingia kwa kasi
kusaka bao la kusawazisha, huku Manchester United ikipata pigo mwishoni
mwa kipindi cha kwanza baada ya beki na nahodha wake Nemanja Vidic kugongwa kichwani na hivyo kulazimika kukimbizwa hospitali.
Kwenye kipindi cha kwanza kipa wa Arsenal,
Wojciech Szczesny ndiye aliyepata misukosuko baada ya kuokoa shuti la
umbali wa mita 25 lililopigwa na Wayne Rooney, licha ya kwamba shuti hilo lilipunguzwa makali kidogo kwa kumgonga mchezaji mmoja wa Arsenal.
Dakika za mwanzo, Manchester United iliyokuwa
nyumbani Old Trafford ilimiliki mpira kwa asilimia 66 licha kwamba
ilishindwa kutengeneza nafasi za maana za kufunga.
Mechi nyingine za ligi hiyo, Tottenham Hotspur ikiwa nyumbani White Hart Lane ilikubali kipigo kutoka kwa Newcastle United cha bao 1-0, huku Sunderland ikiiduwaza Manchester City kwa kuichapa 1-0 na Swansea City ikitoka sare na Stoke City kwa kufungana mabao 3 - 3.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!