Wakuu wa nchi kadhaa za Mashariki
mwa Afrika wanakutana leo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba kwa
lengo la kutafuta njia za kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Baada ya hapo, siku ya Ijumaa, mji mkuu
wa Kenya, Nairobi utakuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa Halmashauri
ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD), ambayo ni jumuiya ya baadhi ya nchi
za Mashariki mwa Afrika. Hayo yamedokezwa na afisa wa Wizara ya Mambo ya
Nje ya Kenya Karanja Kibicho ambaye ameongeza kuwa Rais Salva Kiir wa
Sudan Kusini anatazamiwa kuhudhuria mkutano huo ambao utajadili mgogoro
wa nchi yake.
Tayari wakuu wa Umoja wa Afrika na IGAD
wametoa wito kwa pande husika katika mgogoro wa Sudan Kusini kuanza
mazungumzo kwa lengo la kumaliza vita vya ndani nchini humo. Rais wa
Sudan Kusini amesema yuko tayari kufanya mazungumzo ya kumaliza vita vya
ndani nchini humo ambavyo vimepelekea mamia ya watu kuuawa katika
kipindi cha siku 10 zilizopita. Naye kiongozi wa uasi mpya Sudan Kusini
Riek Machar, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais, amesema yuko tayari kwa
mazungumzo lakini anataka Kiir aondoke madarakani kutokana na kile
anachodai kuwa ni udikteta.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!