KIUNGO veterani wa Manchester United, Ryan Giggs, amesema kuna
ulazima wa Ligi Kuu England kupumzishwa kwa wiki mbili Januari mwakani
ili kuzisaidia klabu za nchi hiyo kufanya vyema kwenye michuano ya Ulaya
na timu ya taifa itakayocheza fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Giggs, ambaye ni mzoefu wa kipindi kigumu cha
mechi nyingi kwenye Ligi Kuu England inapofika mwisho wa mwaka, alisema
jambo hilo linawafanya wachezaji kuchoka na hivyo kushindwa kutamba
kwenye michuano ya Ulaya wanapomenyana na wenzao ambao walipata muda wa
kupumzika.
Kwingineko kwenye ligi kubwa Ulaya kama Ujerumani, Italia, Hispania na hata Ufaransa, ligi zinasimama unapoingia Mwaka Mpya.
Ujerumani, ligi zinapumzika kwa wiki tano, wakati
Ufaransa wachezaji wanapewa mapumziko ya wiki tatu ili kujipanga vyema,
huku Hispania na Italia kumekuwa na mapumziko kwa kipindi cha Mwaka
Mpya.
Giggs alisema: “Kwa mapato ya televisheni ni
mazuri kwa sababu viwanja huwa vinajaa sana. Lakini hilo linaweza
kuiathiri timu ya taifa.
“Unapokuwa mapumziko inasaidia sana na hata kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya utakwenda ukiwa fiti. Nadhani kuna ulazima wa
ligi kuwa na mapumziko kinapofika kipindi cha majira ya baridi.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!