STRAIKA wa Simba, Amissi Tambwe, amesema sasa anajua ujanja wa
kocha mpya wa Simba, Mcroatia Zdravko Logarusic, baada ya kuangalia
staili yake ya ufundishaji kwenye ‘You Tube’ kwa takribani saa sita.
Tambwe anasema aliziangalia video hizo kwa lengo
la kujua ni vipi ataweza kuendana na staili ya ufundishaji wa kocha huyo
na pia kujua atawezaje kupata nafasi ya kufunga mabao.
Mshambuliaji huyo ambaye yupo hapa nchini mapumzikoni, alisema anatarajia kutua Tanzania wiki ijayo kwani anangoja
viongozi wa klabu yake wamtumie tiketi.
“Nataka kuwa mfungaji bora na kuisaidia timu yangu
kutwaa ubingwa, lakini ni lazima ujue kocha anataka nini, pia inabidi
ucheze kuendana na staili anayoitaka. Hivyo mimi niliona ni bora nianze
kumtizama mapema kabla hatujakutana,” alisema.
“Kwa mtazamo wangu baada ya kuangalia video zake
akiwa na Gor Mahia ya Kenya na timu nyingine za Ghana, niligundua kuwa
katika timu yake amekuwa akiwatumia washambuliaji ipasavyo, hivyo kwa
staili hiyo bila shaka nitailetea Simba mafanikio.
“Huyo kocha mpya anaonekana anapenda mabao mengi
na anataka straika asiwe na masihara anapokuwa karibu na lango. Lakini
pia anataka viungo wanaopandisha mashambulizi, kocha atafurahia mambo
yangu.”
Straika huyo aliongeza: “Itakuwa wakati wa Simba
kurudi kileleni, falsafa na staili ya ufundishaji ya mwalimu
itaturudisha juu kama timu.”
Naye Logarusic alisema: “Bado sijawajua mastraika
wangu vizuri, wakianza mazoezi nina uhakika tutajua tusaidiana vipi na
wapi watanifaa.
“Najua kuwa straika wa Simba (Tambwe) ndiye
anayeongoza kwa magoli, nafikiri ni kitu kizuri cha kuanzia. Hivyo
nitahakikisha anazidi kuisaidia timu akishirikiana na wenzake.”
Kwa upande wake, mshambuliaji, Betram Mwombeki,
alisema: “Mimi nitahakikisha nakuwa kikazi zaidi, timu itakayokuja mbele
yangu lazima ijue mimi nafanya kazi gani Simba. Sitaki kuongea sana
kwani mikakati yangu ya sasa ni kufanya kazi.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!