Leo ni Jumapili tarehe 29 Desemba mwaka 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1835 iliyopita, mji wa Izmir ulioko
magharibi mwa Uturuki ya leo, uliharibiwa na kubomolewa vibaya kufuatia
mtetemeko mkubwa wa ardhi. Janga hilo lilipelekea nusu ya wakazi wa mji
huo wa Izmir kupoteza maisha na wengine wengi kubaki bila makazi. Katika
wakati huo mji wa Izmir ulikuwa chini ya utawala wa Roma na ulihesabiwa
kuwa moja ya vituo muhimu vya utawala huo katika Asia Ndogo. Hatimaye
mji huo ulijengwa upya kwa amri ya Marcus Aurelius mtawala wa wakati huo
wa Roma.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, mkataba wa kupata
uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania
Jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza. Hata hivyo
kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza
ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949,
Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa
mkoloni Muingereza. Uhuru wa Ireland ilikuwa ni natija ya mapambano ya
karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.
Na siku kama ya leo miaka 1147 iliyopita alifariki dunia
Thabit bin Qarrah Harrani, mwanahesabati na mnajimu wa Kiislamu wa Iraq.
Harrani alizaliwa mwaka 211 Hijria na alikuwa miongoni mwa wanazuoni
wakubwa wa zama zake. Thabit Harrani pia alikuwa hodari katika kutarjumu
vitabu vya sayansi kutoka lugha za Kigiriki na Kisiriani kwenda lugha
ya Kiarabu. Vitabu vingi vya Kigiriki vilitarjumiwa kwa lugha ya Kiarabu
na Thabit bin Qarrah au chini ya usimamizi wake. Baadhi ya wanahistoria
wanasema, mwanazuoni huyo alitarjumu vitabu 130 kwa lugha ya Kiarabu.
Mbali na kutarjumu, Harrani ameandika pia vitabu kadhaa kama "Kitabul
Raudha fi Tibb" na Masailul Handasa wal A'adad".
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!