Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa limepoteza udhibiti wa mji muhimu wa Bor ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Jonglei huku kukiwa na wasi wasi mkubwa kuwa mapigano baina ya mirengo hasimu jeshini itapelekea kuibuka vita vya ndani nchini humo.
Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer amenukuliwa akisema Jumatano kuwa, ‘hatuudhibiti tena mji wa Bor’. Mji Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuna ishara kuwa machafuko ambayo yamepelekea mamia ya watu kuuawa katika mji mkuu Juba sasa yanaenea kote Sudan Kusini.
Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Balozi Gerard Araud wa Ufaransa ameonya kuwa makabila mawili makubwa ya Dinka na Nuer yamkini yakaitumbukiza nchi hiyo katika vita vya ndani. Mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba yalianza pale wanajeshi wanaoaminika kuwa watiifu kwa Riek Machar makamu wa zamani wa rais, walipojaribu kuipindua serikali ya Rais Salva Kiir. Katika taarifa aliyoitoa Jumatatu Rais Kiir alisema mapinduzi hayo yamezimwa. Uhasama wa kisiasa nchini Sudan Kusini ulianza mwezi Julai pale Kiir alipomfuta kazi Machar. Kiir ni wa kabila la Dinka ambalo ndio lenye nguvu zaidi na Machar ni wa kabila la Nuer.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!