Askari watatu wa vikois vya kulinda amani nchini Sudan Kusini wameuawa kwenye shambulio lililotekelezwa na vijana wa kabila la Nuer ambao walivamia kambi ya vikosi hivyo kwenye mji wa Akobo kwenye jimbo la Jonglei.Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kuongeza kuwa mpaka sasa ofisi yake inaendelea kufanya mawasiliano na viongozi wa kambi hiyo kubaini chanzo cha wapiganaji hao wa kijadi kuwashambulia.
Hili ni shambulio la kwanza kutekelezwa na wapiganaji wanaodaiwa kuasi Serikali na kuingia msituni kwa lengo la kutaka kuipindua Serikali ya rais Salva Kiir.
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuendelea wa vita hivi na kwamba sasa vimechukua mrengo wa kikabila kati ya makabila mawili makubwa nchini humo ambayo yamekuwa yakipigana kuwania madaraka kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon amelaani shambulio hilo na kuagiza kuongezwa askari zaidi kwenye jimbo hilo kuwalinda wananchi dhidi ya mashambulizi mengine yanayopangwa kufanywa na wapiganaji hao.
Shambulio hili limetekelezwa kwenye kambi ambayo maelfu ya wananchi wa Sudan Kusini wa kabila la Dinka wamekimbilia kupata hifadhi kuhofia kuuawa kutokana na machafuko yanayoendelea kati ya wanajeshi walioasi na wale wa Serikali.
Rais Salva Kiir anamtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwa kuchangia kutokea kwa mapigano hayo kwa kile anachodai amekuwa akipandikiza chuki baiana ya vikosi vya Serikali kwa misingi ya kikabila tuhuma ambazo Machar mwenyewe amekanusha akiwa kusikojulikana.
Hapo jana rais Kiir alitarajiwa kuwa na mazungumzo na mawaziri wa mambo ya kigeni saba toka mataifa ya Afrika walioko nchini humo kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umelikumba taifa hili jipya kabisa barani Afrika.
Vikosi vya Marekani kwa kushirikiana na vile vya Umoja wa Mataifa vimeimarisha usalama kwenye uwanja wa ndege wa Juba kulinda usalama wa ndege zinazotua na kuondoka kwenye uwanja huo kufuatia hofu ya kuwepo kwa njama za kutekelezwa kwa shambulio kwenye uwanja huo.
Wakati huohuo maelfu ya wananchi ambao sio rais wa Sudan Kusini na wale ambao ni raia wameendelea kuikimbia nchi yao kufuatia tangazo la nchi zao kuwataka kuondoka nchini humo kwa usalama wao kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo.
Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Philip Aguer amethibitisha vikosi vya Serikali kuupoteza mji wa Bor kwa vikosi vya Riek Machar.
Mapigano haya yalianza siku ya Jumatatu ya juma hili ambapo rais Salva Kiir alitangaza Serikali yake kubaini mpango wa kutaka kufanyika mapinduzi ya kuipindua Serikali yake, mpango ambao amedai ulikuwa umepangwa na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!