BALLON d’Or siku zote inatajwa kuwa ni vita inayochezwa nje ya
uwanja kuwafanya wachezaji kutwaa tuzo binafsi za mafanikio ya vipaji
vyaowanavyovionyesha ndani ya uwanja.
Kwa misimu kadhaa, ulimwengu wa soka uligubikwa na
mjadala wa nani zaidi kati ya wanasoka wawili wanaotajwa kuwa na
upinzani mkubwa kwenye kusaka umaarufu, Cristiano Ronaldo na Lionel
Messi.
Kwa mwaka jana mjadala huo uliendelea na usiku wa
Jumatatu iliyopita jibu lilipatikana, Ronaldo akatajwa kuwa zaidi ya
Messi na kutwaa tuzo hiyo kwa kura 1,365 dhidi ya kura 1,205 za Messi.
Vita hiyo ilimhusisha pia Mfaransa Franck Ribery anayecheza Bayern Munich, ambaye aliambulia kura 1,127.
Asubuhi ya juzi Jumanne, Ronaldo alikwenda
mazoezini Real Madrid na kusherehekea na wachezaji wenzake akiwa
ameshika tuzo hiyo ambapo walipiga picha ya pamoja na kisha akaandika
kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Tuzo hii ni ya kila mtu. Kwa wote
wafanyakazi na mabosi na mashabiki wote!”
Alipotajwa mshindi Jumatatu, Ronaldo alimwaga
chozi kabla ya kufichua kwamba haikuwa rahisi kuinasa tuzo hiyo licha ya
kwamba ilikuwa ni mara yake ya pili.
Lakini, imefichuka kwamba si Ronaldo wala Messi
aliyempigia kura mwenzake kwenye kuwania tuzo hiyo. Wachezaji hao ambao
ni manahodha wa nchi zao, hawakupigiana kura.
Kama inavyoelezwa, kutwaa Ballon d’Or ni vita
inayochezwa nje ya uwanja, mashabiki na marafiki wa mastaa hao ndiyo
waliofanya kazi kubwa katika kuhamasisha upigaji wa kura za kumpata
mshindi.
Mfumo wa upigaji kura uliochukuliwa katika tovuti
ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) unafichua kwamba chaguo la
kwanza thamani yake ni alama tano, alama tatu kwa chaguo la pili na la
tatu ni alama moja.
Messi, Ronaldo wachuniana
Messi amekubali na kukiri kwamba Ronaldo
alistahili tuzo hiyo huku akidai alikuwa majeruhi muda mrefu na jambo
hilo lilimfaidisha mpinzani wake.
Ukiacha Fifa kuwaweka karibu ukumbini ambapo siti
zao zilitofautishwa na siti moja tu katikati, kushoto akiwa ameketi
Ronaldo na mpenzi wake mrembo Irina Shayk na kulia akiwa Messi na mkewe
Antonella Roccuzzo, wachezaji hao walikuwa kwenye presha kubwa kabla ya
kufichuka kwamba walichuana kwenye kupigiana kura.
Kati yao, hakuna aliyemtambua mwenzake kwamba ni bora. Kwa
mujibu wa kura hizo, Ronaldo hakuwa mchezaji bora wa Messi kwa mwaka
2013 sawa na ilivyokuwa kwa Mreno huyo ambaye hakumtambua staa huyo wa
Argentina kama ni bora kwa mwaka huo.
Kura zilikuwa zikipigwa na manahodha, makocha
waandishi maalumu ambao ni wajumbe wa Fifa. Kwa kuwa wawili hao wote ni
manahodha kwenye nchi zao, Messi wa Argentina na Ronaldo wa Ureno,
walikuwa na ruhusa ya kupiga kura, lakini hawakutakiwa kujichagua
wenyewe.
Messi awachagua Barca wenzake
Kwenye kura hizo, Messi aliwapigia nyota wenzake
wa Barcelona, Andres Iniesta akiwa chaguo lake la kwanza, kisha
akawapigia Xavi na Mbrazili Neymar.
Kwa kura hizo, inaonyesha Messi alikoshwa na
viwango vya nyota wenzake wa Barcelona kwa mwaka jana, huku akiwa
hajaona mchezaji yeyote mwenye kiwango kikubwa kuliko wakali hao kutoka
kwenye klabu nyingi ukimweka kando mpinzani wake, Ronaldo.
Kwenye kura hizo, Ronaldo alikuwa tofauti baada ya
chaguo lake la kwanza kuwa straika wa Colombia na klabu ya Monaco,
Radamel Falcao, wakati kwenye nafasi ya pili na tatu aliwapigia staa wa
Wales, Gareth Bale na Mjerumani wa Arsenal, Mesut Ozil.
Kura za Ronaldo zinaonyesha kwamba hakuwa mbinafsi
kwa maana ya kutazama wachezaji waliopo kwenye kikosi chake tu
anachochezea kama alivyofanya Messi, licha ya kwamba Ozil aliwahi
kucheza Real Madrid na Bale amejiunga na klabu hiyo ya Santiago Bernabeu
msimu huu.
Messi lazima atahitaji maelezo kutoka kwa kocha
wake wa timu ya taifa, Alejandro Sabella kwa nini alimpigia kura
Ronaldo, wakati alipomchagua kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Messi na
Ribery.
Kwa bahati mbaya, Ribery alishika nafasi ya tatu,
lakini akiwa amepata kura za kwanza kutoka kwa nahodha wake wa Ufaransa
Hugo Lloris na kocha wake, Didier Deschamps.
Ufaransa walimtosa Messi, wakati mwenzake Ronaldo alipata kura kutoka kwa Deschamps aliyekuwa chaguo lake la pili.
Kocha wa Ureno, Paulo Bento alipiga kura kiufundi, akimchagua
nyota wake, Ronaldo kwenye nafasi ya kwanza na kisha akawapa Falcao na
Arjen Robben ambao wote hawakuwamo kwenye tatu bora, huku akimweka kando
kabisa Messi.
England, kocha Roy Hodgson na nahodha wake, Steven
Gerrard wote walimchagua kwenye nafasi ya kwanza, kabla ya kutofautiana
kwa wachezaji wengine, wakati Hodgson aliwataja Zlatan Ibrahimovic na
Robin van Persie, Gerrard aliwachagua Messi na nyota mwenzake wa
Anfield, Luis Suarez.
Ibrahimovic, aliyetwaa tuzo ya Bao Bora la Mwaka
alilofunga kwa ‘tick-tack’ dhidi ya England, alimpigia Ribery, Messi na
Ronaldo licha ya kwamba staa huyo wa Sweden mara kadhaa aliripotiwa kuwa
na bifu na supastaa wa Argentina, Messi, huku kwa Afrika, nahodha wa
Cameroon, Samuel Eto’o na wa Ivory Coast, Didier Drogba walimpigia kura
Yaya Toure.
Italia, Gianluigi Buffon na kocha wake, Cesare Prandelli walimchagua mtu wao, kiungo Andrea Pirlo kwenye nafasi ya kwanza.
Baadhi ya kura za manahodha zilivyopigwa na
wachezaji waliowachagua kwenye mabano; Messi, Argentina (Iniesta, Xavi,
Neymar), Thiago Silva, Brazil (Messi, Ibrahimovic, Ronaldo), Gerrard,
England (Ronaldo, Messi, Suarez), Hugo Lloris, Ufaransa (Ribéry, Manuel
Neuer, Bale), Philipp Lahm, Ujerumani (Ribéry, Ronaldo, Messi).
Gianluigi Buffon, Italia (Pirlo, Ronaldo, Messi),
Robin van Persie, Uholanzi (Robben, Ibrahimovic, Ronaldo), Ronaldo,
Ureno (Falcao, Bale, Ozil), Iker Casillas, Hispania (Ronaldo, Ribery,
Robben), Ibrahimovic, Sweden (Ribery, Messi, Ronaldo).
Kura za makocha; Alejandro Sabella, Argentina
(Messi, Ribery, Ronaldo), Luiz Felipe Scolari, Brazil (Ronaldo, Messi,
Ibrahimovic), Roy Hodgson, England (Ronaldo, Ibrahimovic, Van Persie),
Didier Deschamps, Ufaransa (Ribery, Ronaldo, Ibrahimovic), Cesare
Prandelli, Italia (Pirlo, Philipp Lahm, Robert Lewandowski), Louis van
Gaal, Uholanzi (Ribery, Thomas Muller, Robben).
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!