UHUSIANO kati ya kocha wa Manchester United,
David Moyes na winga wake chipukizi, Wilfried Zaha umetajwa kuwa katika
hali mahututi na unaweza kufa muda wowote. Kuna mambo mengi yanaendelea
nyuma ya pazia baina ya wawili hao.
Zaha amekuwa katika wakati mgumu Manchester United
tangu aliposajiliwa na kocha aliyepita katika klabu hiyo, Sir Alex
Ferguson kwa dili la Pauni 15 Milioni akitokea Crystal Palace Januari
mwaka jana.
Hata hivyo, kitendo cha Ferguson kuamua kustaafu
soka bila hata kufundishwa naye kulivunja mipango yote ya Man United
dhidi yake kwa sababu kocha mpya aliyefuata hampi thamani hiyo.
Zaha azuiwa kuhama, afoka
Zaha amechukia vikali kuzuiwa kuhama Manchester
United kwenda klabu ya Cardiff City kwa mkopo na Moyes na sasa
anafikiria kuandika barua ya kuomba kuihama klabu hiyo.
Ilidaiwa kuwa Moyes alishakubaliana na kocha mpya
wa Cardiff City, Ole Gunnar Solskjaer lakini akabadili mawazo ghafla kwa
kile alichodai kuwa timu hiyo imeandamwa na majeruhi katika eneo la
winga wa pembeni ambapo Luis Nani na Ashley Young wote ni majeruhi.
Alhamisi Zaha alipigiwa simu kufahamishwa kuhusu
kukwama kwa dili lake la kwenda kucheza kwa mkopo Cardiff ambapo
kulikuwa na majadiliano makali ya simu kati ya wawakilishi wake na
Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward.
Hata hivyo Zaha mwenyewe alisikika akifoka na baadaye simu hiyo ilikatwa bila ya kuwepo mwafaka baina ya pande hizo mbili.
Wakati hali ikiwa hivyo tayari Moyes amemwambia
Zaha kuwa uhamisho wake wa mkopo atauangalia tena mara baada ya pambano
la marudiano dhidi ya Sunderland katika michuano ya Kombe la Ligi au
Capital One.
Agoma kusafiri mechi ya Chelsea
Moyes anaamini kuwa benchi lake la ufundi lina
hoja nzuri katika kumzuia Zaha kutolewa kwa mkopo, lakini Zaha amekerwa
na kitendo hicho ambacho kinaikera nafsi yake hasa ukizingatia kwamba
hata akibaki bado anasugua benchi.
Kutokana na kukerwa huko, inadaiwa Zaha aliamua
kubaki nyumbani kwake katika Jiji la Manchester badala ya kwenda London
kushuhudia pambano la timu yake dhidi ya Chelsea jana Jumapili katika
uwanja wa Stamford Bridge.
Nyota huyo anayekipiga katika timu ya taifa ya England chini ya
umri wa miaka 21, huku akilipwa na Man United mshahara wa Pauni 30,000
kwa wiki, bado hajaanza mechi hata moja chini ya Moyes huku akiwa
ameachwa nyuma katika nafasi yake na Adnan Januzaj, Antonio Valencia,
Nani, Young na Danny Welbeck.
Adai anaonewa na Moyes mazoezini
Inadaiwa kuwa Zaha anaamini Moyes anamwonea katika
mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika Uwanja wa Carrington jijini
Manchester na tayari alishapokea barua ya kurasa nne kutoka kwa kocha
huyo akimbwatukia.
Zaha anaamini kuwa Moyes amekuwa akimwandama kwa
chuki binafsi mazoezini na katika tukio moja lisilo la kawaida alifokewa
sana wakati alipopiga pasi iliyonaswa na maji yaliyokuwepo uwanjani.
Hata hivyo, sekunde chache baadaye kiungo Mjapani,
Shinji Kagawa alifanya kosa hilo hilo lakini Moyes hakumfokea wala
kuonyesha kukerwa.
Chini ya utawala wa Moyes, Zaha amecheza dakika
167 tu na nyingi kati ya hizo amecheza katika michuano ya Kombe la Ligi.
Hata hivyo kocha wa timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, Gareth
Southgate ameendelea kumchagua katika kikosi hicho.
Zaha anaamini kuwa alitengwa mno wakati stori
zilipoibuka mitandaoni kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto wa
Moyes aitwaye Lauren Moyes.
Alikerwa zaidi baada ya klabu hiyo kushindwa kutoa
taarifa za kukanusha habari hiyo hali iliyomlazimu yeye mwenyewe
akanushe katika mtandao wake wa Twitter.
Katika taarifa hiyo Zaha alisikika akisema:
“Sijawahi kuwa na uhusiano wa mapenzi wala kukutana na binti wa David
Moyes kwa hiyo nadhani hiyo si sababu ya mimi kutokucheza. Ningependa
kuzuia uvumi huu wa uongo.”
Binti huyo wa Moyes alilazimika kuiondoa hewani
akaunti yake ya Twitter katika tukio la Oktoba mwaka jana huku wengi
wakiamini kuwa wameipata sababu halisi ya Moyes kumwacha nje katika
kikosi cha kwanza Zaha.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!