KWA wanaomtambua tangu utoto wake,
alichokifanya Jumatatu iliyopita hakikuwa kigeni kwao. Kulialia.
Cristiano Ronaldo alidondosha chozi aliponyakua tuzo yake ya pili ya
Mwanasoka Bora wa Dunia, lakini kitendo cha kulia na kutokwa machozi ni
kitu alichokifanya sana utotoni kutokana na kukabiliwa na ugumu wa
maisha.
Akiwa amezaliwa katika mji wa kimasikini sana,
Madeira huko Funchal, Ureno alikuwa na sifa moja ya kulia kila mambo
yake yalipokwama, lakini kwenye tukio lile la wiki iliyopita, Ronaldo
alidondosha chozi la furaha baada ya kutajwa mshindi wa Ballon d’Or tuzo
ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa mbele ya Lionel Messi na Franck
Ribery.
Ronaldo utotoni
Alikulia katika mji wa milima mingi kisiwani
kwenye eneo lililoitwa Santo Antonio, utotoni Ronaldo alikuwa mtoto wa
mama (legelege). Akiwa wa nne kwenye familia ya Dolores na Dinis, mimba
ya Ronaldo ilikuwa ya bahati mbaya.
Mama yake alikuwa mpishi na baba yake alikuwa
mtunza bustani wa manispaa, ambaye alikuwa ameathirika sana kwa ulevi
kabla ya kufariki 2005.
Misosi ilikuwa adimu sana nyumbani kwa kina Ronaldo.
Alipozaliwa mama yake alimpa jina la Cristiano,
baba yake akampa Ronaldo ikiwa ni jina la Ronald Reagan (Mwigizaji
filamu na rais wa zamani wa Marekani, ambaye Dinis alikuwa kipenzi
chake).
Baada ya kuandamana na baba yake kwenda kwenye
klabu ya kijijini kwao, Andorinha, Ronaldo akaanza kuwa na mapenzi ya
soka na kipindi hicho alikuwa akicheza na binamu yake, Nuno. Alipoanza
soka, Ronaldo hakurudi tena nyuma.
Aanza kucheza beki
Francisco Afonso, mwalimu wa shula ya msingi,
ambaye alikuwa kocha wa kwanza kumnoa Ronaldo, alifichua ukweli kuhusu
staa huyo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno baada ya kudai
mwanzoni fowadi huyo alianzia kucheza beki. “Alionekana kuwa na kitu
tangu utoto wake, alikuwa na mwili mdogo sana, lakini alihitaji kufanya
kitu,” anasema.
“Alianza kucheza beki kabla ya kuamua kupanda
mbele kwa sababu alitaka kushiriki kila kitu. Alikuwa mahiri kwenye
miguu yote na alikuwa na kasi sana kitu ambacho aliendelea kukifanyia
mazoezi muda wote na kuwa bora zaidi. Soka ikawa ndiyo kila kitu kwake,
asipocheza alikuwa kama mgonjwa.”
Rafiki wa utotoni afichua
Rui Alves, rafiki kipenzi wa Ronaldo utotoni, ambaye bado
wanaendeleza urafiki wao hadi sasa, anasema kitu pekee Ronaldo
alichokuwa akikitaka utotoni ni kucheza soka tu.
“Tulikuwa tunakwenda kucheza siku nzima, lakini Cristiano muda wote alikuwa akipiga mpira wake,” anasema.
“Nilijaribu kumfanya acheze michezo mingine,
lakini yeye alichohitaji ni soka tu. Kila jioni tulikuwa tukienda
kununua mikate, lakini Ronaldo kila alipokuwa akienda lazima awe na
mpira wake mkononi.” Kwenye klabu ya Andorinha, ndipo Ronaldo alipoanza
kuweka alama zake. Ricardo, aliyekuwa mchezaji mwenzake kwenye timu
hiyo, ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye baa ya klabu hiyo,
anamkumbuka Ronaldo kwa kupenda ushindani.
“Mtaani alikuwa akitaka kuwa yeye zaidi. Tangu
alipokuwa mdogo, alitaka mpira muda wote uwe kwake, alipoukosa basi
alichukia sana na wakati mwingine alikuwa akilia,” anasema Ricardo.
Kwenye mechi moja, Cristiano aliifungia Andorinha ‘hat-trick’ (mabao
matatu) kwenye kipindi cha kwanza na kuifanya timu yake kwenda mapumziko
ikiwa mbele 3-0. Kipindi cha pili kilipoanza, Ronaldo aliumia kichwani
na kukimbizwa hospitali kupata matibabu kabla ya kurudi uwanjani akiwa
na bandeji kichwani na kuchukia zaidi kwa sababu kwa muda huo ambao yeye
hakuwapo uwanjani, Andorinha ilipoteza uongozi wake wa 3-0 na kufungwa
4-3.
Kuhamia timu kubwa
Baada ya kuonyesha kuwa na kipaji, akiwa na umri
wa miaka 12, hakimu wa mji wa Madeira, Joao Marques de Freitas alimpigia
simu skauti wa klabu ya Sporting Lisbon, Aurelio Pereira, kujadili
uwezekano wa Ronaldo kwenda kufanya majaribio kwenye klabu hiyo ya bara.
“Nilikutana na Ronaldo alikuwa na umri wa miaka
11,” anasema De Freitas. “Baba yake wa ubatizo alinitambulisha kwake na
kusema ni mchezaji mzuri sana. Alikuwa mdogo sana na mwembamba sana.
“Nilichofanya niliwasiliana na mtu wa Sporting na
nilimwambia: ‘Kuna mtoto hapa wanasema ni mzuri sana.’ Lakini, yeye
alinijibu: ‘Huyo ni mtoto sana’ kisha akaniambia kwamba tusimpeleke
mtoto mdogo kama huyo Lisbon.
“Hivyo nilizungumza na mama yake Cristiano, ambaye
alikuwa mtu safi, alikubali. Hivyo tulimnunulia tiketi Ronaldo ya
kwenda Lisbon na tulimfunga mfano wa kibao shingoni kilichokuwa
kimeandikwa jina lake. Aurelio alikuwa stendi kumsubiri na alikaa Lisbon
kwa siku nne.”
Kuna siri imefichuliwa kwamba Nacional klabu
inayodai kumtengeneza Ronaldo inaidai Sporting Euro 25,000, licha ya
kwamba uhamisho wake ulionekana kuwa bure. Hilo lilikuwa dau kubwa sana
kwa mchezaji wa umri wa miaka 12, lakini viongozi wa klabu hizo mbili
walikubaliana kufanya siri.
Atua Sporting
Hatimaye Ronaldo alitua Sporting na kujiunga na
shule ya klabu hiyo inayosifika kwa kutengeneza mawingi wengi wenye
viwango vya juu sana akiwamo Luis Figo.
Mama yake Ronaldo, alikuwa shabiki mkubwa sana wa Figo na pia
anaishabikia Sporting, hivyo kitendo cha mwanaye kujiunga na timu hiyo
kilimfanya kuwa na furaha isiyo kifani.
Mwanzoni maisha yalikuwa magumu sana kwa Ronaldo
kwa sababu ya utoto wake, alikuwa akilia mara kwa mara kukumbuka
nyumbani ambapo wenzake walikuwa wakimcheka sana.
Rafiki yake wa utoto, Rui anasema: “Watu hawamjui
Ronaldo. Wanajifanya wanamjua, lakini ukweli ndio huo. Ronaldo ni mtu
mwenye misimamo sana. Siku hizi haji Santo Antonio kwa sababu kuna watu
wengi sana hawana kazi, anapokuja wanamuomba pesa tu, hivyo anaamua
kukaa nao mbali. Lakini, bado hilo halimfanyi kuwa mtu mbaya.
“Bado tunawasiliana naye na baadhi ya siku
tumekuwa tukifurahia maisha pamoja naye,” anasema Rui kabla ya rafiki
mwingine, Ricardo kuongeza: “Inafurahisha sana, nilipokuwa mdogo
nilikuwa namtazama Pauleta, aliyekuwa akitokea Azores (visiwa vingine)
akichezea Ureno na nilikuwa nikiwaza kwanini na sisi kwetu Madeira
kusitokee mchezaji kama wao? Kwa bahati nzuri, kwetu ametokea aliyebora
zaidi.
“Ronaldo amekiweka kisiwa chetu kwenye ramani ya
dunia na hakika tunashukuru kwa hilo na siku zote tutamheshimu kwa
alichotufanyia.”
Kwa chozi lile alilodondosha Ronaldo mjini, Zurich
haikuwa pekee tu kwake, walidondosha wengi huko Madeira kutokana na
ushindi wake, eneo ambalo supastaa huyo alikua kwa umasikini mkubwa na
kulialia sana kabla ya sasa kuwa mchezaji maarufu duniani.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!