Kenya imesema haitatuma wanajeshi wake katika nchi jirani ya Sudan Kusini pamoja na kuwa Umoja wa Mataifa umeiomba ifanye hivyo.
Haye yamebainishwa jana na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Kenya Bi. Amina Mohammad ambaye amesema Umoja wa Mataifa
umeitaka Nairobi itume askari 5,500 ili kuzuia kuenea vita Sudan
Kusini. Amesema serikali ya Kenya itasaidia kurejesha amani nchini humo
kwa njia za kidiplomasia. Bi. Amina amedokeza kuwa Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa limeziomba nchi kadhaa zikiwemo Kenya na Rwanda
kuchangia kikosi cha askari 5,500 katika nchi hiyo iliyotumbukia vitani
tokea Desemba 15 mwaka jana. Akijibu madai kuwa uamuzi wa Uganda kutuma
wanajeshi wake Juba ni tishio kwa mazungumzo ya amani nchini humo, Bi.
Amina amesema uamuzi wa Kampala kutuma askari wake Juba umeidhinishwa na
serikali ya Sudan Kusini pamoja na jumuiya ya kieneo ya IGAD. Wakati
huo huo Katibu mkuu wa IGAD Mahboub Maalim amesema mazungumzo ya
upatanishi yanaendelea vizuri mjini Addis Ababa, Ethiopia. Umoja wa
Mataifa umetangaza kuwa watu karibu nusu milioni wamekimbia makazi yao
Sudan Kusini kutokana na mapigano makali ambayo yamegeuka kuwa ya
kikabila baina ya kabila kubwa zaidi la Dinka la Rais Salva Kiir na
kabila la Nuer la Riek Machar anayeongoza uasi.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!