KIUNGO Mhispaniola Juan Mata kwa sasa ni
mchezaji wa Manchester United baada ya kukamilisha uhamisho wake wa
Pauni 37.1 milioni akitokea Chelsea.
Staa huyo wa kimataifa wa Hispania ametua Old
Trafford, lakini amekiri kwamba daima mashabiki wa Stamford Bridge
watabaki kuwa na nafasi kubwa moyoni mwake. Katika kulithibitisha hilo,
Mata aliwaandikia barua mashabiki wa Chelsea na kisha akaiweka kwenye
tovuti yake ili kila mmoja apate fursa ya kuisoma. Mata alianza kwa
kuwasalimia; Habari zenu. Kisha akaendelea kuwapasha mashabiki wa klabu
hiyo kuhusu uamuzi wake wa kuhamia Man United.
Mata anaanza...
Kama mnavyotambua hii ni siku muhimu
sana katika maisha yangu, kuhamia Man United. Ningependa mtambue hisia
zangu kila ninavyoendelea kuandika barua hii.
Ninachokieleza kwenye barua hii
kinatoka moyoni, kwanza ningependa kusema sitasahau mapenzi yenu kwangu
tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho. Kwani mapenzi yenu yamenisaidia
kupevuka kama mchezaji na kuwa mahiri ndani na nje ya uwanja. Siku zote
nitakuwa na hisia za kipekee kwenu. Daima. Maneno hayajitoshelezi
kuelezea vitu mlivyonipa.
Nimepita kwenye nyakati nzuri sana;
kutwaa ubingwa wa Kombe la FA, taji langu la kwanza nilipofika Chelsea,
pia nafurahi kuwa sehemu ya kihistoria kwa kuwamo kwenye kikosi
kilichotwaa kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe
la Europa League.
Kwa upande mwingine, nimekumbana na
mambo yenye utata mkubwa kwenye maisha binafsi hasa kwa miezi sita ya
hivi karibuni. Lakini, kwa meseji zenu mlizonitumia kwenye mitandao ya
kijamii, maneno mliyoniambia tulipokutana mitaani au kunisapoti pale
nilipokuwa uwanjani hilo lilinifariji na kujivunia sana kuwa na
mashabiki wa Chelsea.
Siwezi kusahau imani yenu juu yangu
wakati nilipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa Chelsea kwa misimu miwili
mfululizo. Najivunia sana na daima sitasahau siku zile, asanteni sana.
Natumai mnaelewa nyakati ngumu zilizonikabili kwa miezi michache ya hivi
karibuni, nadhani nimefanya chaguo bora zaidi katika kuendeleza soka
langu na kuufurahia mchezo huu.
Kabla ya kipindi cha usajili wa mwaka
jana, dhamira yangu ilikuwa kubaki Chelsea kwa miaka mingi, kuendelea
kutwaa mataji na klabu ya Chelsea. Hiyo ndiyo furaha niliyokuwa nayo
hapo mwanzo kwenye klabu na jiji. Lakini, kama mnavyofahamu, kila kitu
kilibadilika ghafla. Kutoka kwenye kujitambua mimi ni mchezaji muhimu
kikosini hadi kukumbana na nyakati ngumu na kushindwa kuisaidia timu
yangu kama ilivyokuwa awali.
Nilikaa kimya na kuheshimu hali
halisi. Niliamini soka ni mchezo wa kitimu hivyo si rahisi kucheza kila
mechi kwenye kikosi kizuri kama kile. Kwenye michezo unaweza kushinda au
kushindwa, lakini jambo muhimu ni kujitolea kwa kila hali. Nadhani
mnafahamu siku zote nilikuwa nafanya hilo. Kwenye kila mechi, kila
mazoezi bila kujali, nilijitolea kwa kila hali kwa ajili ya klabu yangu.
Napenda kuwashukuru pia wachezaji
wenzangu wa zamani kwa jinsi tulivyoishi tangu siku ya kwanza. Napenda
kumshukuru nahodha kwa msaada wake katika kuniweka sawa kwa sababu
aliguswa na kila kilichokuwa kikiendelea.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!