MAPEMA mwezi huu, kocha David Moyes aliketi kitako na maskauti
wake wote Manchester United wanaofanya kazi Ulaya, akihitaji kupata
mastaa wapya kikosini kwake Manchester United.
Kikao hicho kilifanyika kwenye uwanja wa mazoezi
wa klabu hiyo, Carrington na hapo Moyes akataka kufahamu mipango ya
maskauti wake kwa mwezi huu na uwezekano wa kupata nyota wapya.
Moyes akawasikiliza, hakuridhika na hivyo kuamua kuingia mwenyewe mtaani kusaka nyota wa kuwasajili kwenye usajili wa mwezi huu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na maskauti 16 makini
kwa taarifa zilizopatikana na hapo akataja sehemu ambazo akienda
watarudi na majibu mazuri ya kuwapata mastaa wenye hadhi ya kuvaa jezi
za Man United.
Kikao kilikamilika na wote wakatawanyika sehemu
mbalimbali Ulaya, hasa kwenye nchi sita zinazotajwa kuwa na vipaji vya
maana; Croatia, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Ureno na Hispania. Mwanzo
mbaya wa msimu wa mabingwa hao wa Ligi Kuu
England umemtibua Moyes na kuona kuwapo kwa haja
ya kufanya usajili wa nguvu kikosini kufuatia kufanya vibaya kwenye
ligi, huku kikosi chake kikiwa kimetupwa nje pia kwenye Kombe la FA.
Hilo lilimsukuma Moyes kupanda ndege na kuingia
mwenyewe msituni kusaka wakali wa kuwaongeza kwenye kikosi chake ili
kukifanya kuwa bora na kushirikiana na maskauti wake wamefanikiwa
kutazama zaidi ya mechi 10 ikiwa katika mchakato wa kubashiri nani
atafaa kutinga uzi wa wababe hao wa Old Trafford.
Kuona hatari ya kukosa michuano ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya msimu ujao, kitu ambacho kitamgharimu sana kwenye kupata
wachezaji makini, Moyes ameona ni heri akafanya usajili kwenye mwezi huu
ili apate wachezaji wa kukipigania kikosi ili kiwemo ndani ya nne bora
mwishoni mwa msimu.
Makala hii inazungumzia jitihada za Moyes na mechi
alizohudhuria mwezi huu kwa lengo la kusaka wachezaji sambamba na
msaidizi wake, Phil Neville na mkuu wa maskauti wa klabu hiyo, Jim
Lawlor. Lakini, wachezaji waliokwenda kuwatazama kwenye mechi hizo.
Phil azitazama Getafe v Vallecano
Kocha msaidizi wa Man United, Phil Neville,
Jumapili iliyopita alikuwa nchini Hispania akizishuhudia Getafe na Rayo
Vallecano zikimenyana kwenye Ligi Kuu ya Hispania.
Mchezo huo ulimalizika kwa Rayo kushinda bao 1-0
uwanjani Coliseum Alfonso Perez, shukrani kwa bao la Alberto Bueno
kwenye dakika 29. Lakini, uwanjani hapo,
Neville alikuwa na kazi moja tu kumtaka kiungo wa Franjirrojos, Saul Niguez, aliyekuwa ndani ya uwanja akionyesha ufundi wake.
Niguez mwenye umri wa miaka 19, kwenye mchezo huo
alicheza kwenye safu ya kiungo mkabaji, nafasi ambayo Manchester United
ina tatizo kwenye kikosi chao.
Kiwango cha Niguez kilikuwa cha kuvutia sana na
Man United inataka huduma ya kinda huyo wa Atletico Madrid, anayechezea
Rayo Vallecano kwa mkopo.
Aibukia Atletico Madrid v Valencia
Phil Neville alihusika pia kwenye mchezo huo wa
Kombe la Mfalme uliofanyika Jumanne iliyopita, uliozikutanisha Atletico
Madrid na Valencia.
Kwenye mchezo huo, Neville alikwenda kuwatazama nyota wawili, kiungo Koke na straika hatari, Diego Costa.
Diego Costa alicheza kwa dakika zote tisini,
lakini hakufunga bao kwenye mchezo ambao klabu yake ya Atletico Madrid
ilishinda mabao 2-0.
Nyota mwingine, ambaye Neville alipewa kazi ya kumtazama,
Koke alicheza kwa dakika 58 tu na nafasi yake
kuchukuliwa na Jose Sosa wakati huo kikosi hicho kikiwa kinaongoza kwa
bao 1-0. Baada ya mechi, Neville aliandika ripoti yake na kumpelekea
Moyes kwa ajili ya kuchukua hatua za mwisho.
Lawlor azitazama Benfica v Porto
Benfica iliichapa FC Porto 2-0 kwenye mchezo huo
wa nguvu kabisa wa Ligi Kuu ya Ureno Jumapili iliyopita. Lakini,
jukwaani skauti mkuu wa Man United, Jim Lawlor aliketi kwa makini kabisa
akimtazama staa wa FC Porto, Eliaquim Mangala.
Mangala, mwenye umri wa miaka 22, ni mchezaji
makini, ambaye aliwahi kuisaidia Standard Liege kutwaa ubingwa wa
Ubelgiji kabla ya kuhamia FC Porto, mahali ambapo umahiri wake umesaidia
timu hiyo kunyakua ubingwa mfululizo.
Beki huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 2 amekuwa makini
kwenye nafasi yake na sifa yake kubwa nyingine ni kupiga pasi sahihi
anapokuwa uwanjani. Mangala alicheza soka la kimataifa kwa mara ya
kwanza kwenye kikosi cha Ufaransa wakati timu ilipocheza mechi ya
kirafiki na Uruguay mwaka jana.
Moyes jukwaani Cagliari v Juventus
Mechi hii ilimhusisha bosi mwenyewe, David Moyes
aliyeamua kwenda kumtazama mwenyewe mchezaji au wachezaji wa kuongeza
kikosini kwake.
Jumapili iliyopita kwenye mechi ya Serie A iliyofanyika
Sardinia, Cagliari walikuwa nyumbani kuwakaribisha
Juventus. Jukwaani, Moyes alikuwa na wakati mzuri wa kuwatazama
wachezaji anaowataka na kwenye orodha ya kuwindwa na Man United ni
Davide Astori, Claudio Marchisio na Paul Pogba.
Marchisio alianzia benchi kwenye mchezo huo,
lakini alipoingia tu kuchukua nafasi ya mkongwe Andrea Pirlo aliifungia
bao Juventus na kumfanya Moyes kuamini staa huyo anamfaa zaidi kwenye
kikosi chake ambacho kwa sasa viungo wanaonekana kuwa ni tatizo.
Aonekana Bordeaux v Paris SG
Baada ya kumaliza mchakato wa Italia, Moyes
aliibukia nchini Ufaransa na kuonekana kwenye mechi kati ya Bordeaux na
Paris Saint-Germain Jumanne iliyopita kwenye Kombe la Ufaransa uwanjani
Stade Chaban Delmas.
Akiwa na dhamira kubwa ya kusaka viungo, Moyes
kazi yake ya kwanza kwenye mchezo huo ni kumtazama Blaise Matuidi, licha
ya kwamba staa huyo wa kimataifa wa
Ufaransa aliingia uwanjani kwenye dakika 79 kuchukua nafasi ya Marco Verratti.
Lakini, licha ya kwamba aliingia dakika hizo, bado staa huyo alitikisa nyavu akiunganisha kona ya Adrien Rabiot.
Mechi za Jumatano
Ripoti zilizopatikana ni kwamba skauti mkuu, Lawlor alikuwa na
kazi ya kumtazama tena Eliaquim Mangala kwenye mchezo wa FC Porto na
Penafiel kwenye Kombe la Ureno, wakati Moyes alirudi Italia kwenye mechi
ya Napoli ili kumtazama kiungo staa wa timu hiyo, Marek Hamsik.
Misafara hiyo ya kocha Moyes na msaidizi wake
Neville kuliifanya Man United kama kuupuza mchezo wao wa Ligi Kuu
England dhidi ya Chelsea uliotarajia kufanyika jana Jumapili uwanjani
Stamford Bridge.
Kabla ya mchezo huo, Man United ilikuwa nyuma kwa
pointi 14 dhidi ya vinara Arsenal na hivyo inakabiliwa na mtihani mzito
wa kupunguza pengo hilo ili kuwamo kwenye nafasi za juu zitakazowapa
tiketi ya kucheza Ulaya msimu ujao.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!