WACHEZAJI wa timu ya soka ya Mbeya City ya Tanzania,
wamepigwa marufuku kunyoa nywele za pembeni na kuziacha za katikati
‘kiduku’ na wameambiwa atakayejitosa kunyoa hivyo itakula kwake.
Mbali ya hilo, pia wamepigwa marufuku kufuga nywele na kuzisokota ‘rasta’.
Kauli ya marufuku hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi
wa timu hiyo, Maka Mwalwisi na kuungwa mkono na Katibu Mkuu, Emmanuel
Kimbe, waliosema wachezaji wa timu yao hawajafikia hatua ya kunyoa
nywele kwa mfumo huo kama wanavyofanya wachezaji wa timu nyingine.
Mwalwisi alisema kuwa wachezaji wa Kitanzania
wameiga mfumo huo kutoka kwa wachezaji wa nje jambo ambalo kwao imekuwa
ni vigumu kuhudumia nywele zao kutokana na kipato kidogo wanachokipata.
“Kilichoruhusiwa ni kunyoa upara, hayo mambo
mengine ya ‘kiduku’ na ‘dread’ kwetu hayana nafasi, kwanza uwezo wenyewe
wa kuzihudumia hawana maana wakiweka hizo ‘dread’ zao wanakuwa kama
wachafu,” alisema. “Nywele zinahitaji matunzo kama wanavyofanya
wachezaji wa nje pia muda wa kwenda kuzihudumia saluni, hapa Tanzania
hata hao wanaofuga na kunyoa viduku uwezo wao kifedha sio mkubwa,
tumewaambia atakayenyoa hivyo atapewa adhabu kwa mujibu wa taratibu
zetu.”
Alisema kuwa kwao nidhamu ya ndani na nje ya
uwanja ndiyo wanaipa kipaumbele kuliko mambo mengine yoyote, suala
ambalo liliungwa mkono na aliyekuwa mwamuzi wa soka, Othman Kazi.
Kazi alisema: “Tangu wapande daraja nimebahatika
kuangalia mechi zao ila sijawahi kuona timu yenye nidhamu kama Mbeya
City, ingawa siwezi kuzungumzia kiundani mechi yao na Yanga.
“Wachezaji wa Mbeya City hawana tabia ya kumzonga
mwamuzi pale anapotoa uamuzi wake na hiyo ndiyo nidhamu inayotakiwa kwa
wachezaji.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!