SIMBA juzi Jumatano ilitoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar
katika mechi ya Ligi Kuu Bara lakini mshambuliaji wake, Amissi Tambwe
ameweka rekodi ya kipekee baada ya kuifungia Simba bao la kusawazisha na
hivyo kufikisha mabao 14.
Kwa kufunga bao hilo Tambwe anakuwa ameweka rekodi
kwani katika misimu ya hivi karibuni hakuna mchezaji ambaye ameweza
kufunga mabao 14 baada ya kucheza mechi tatu za mzunguko wa pili wa ligi
na kama akiendelea na kasi hiyo huenda akafanikiwa kuwa mfungaji bora
kwa mabao mengi.
Tambwe alifunga bao hilo la kusawazisha katika
mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro dakika 50 kwa
shuti kali la chini chini akipokea pasi ya Haruna Chanongo.
Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi 31 na
kupanda hadi nafasi ya tatu na kuishusha Mbeya City hadi nafasi ya nne.
Timu zote hizo zina pointi 31 lakini Simba inanufaika na mabao ya
kufunga. Ina mabao 31 wakati Mbeya City ina mabao 21
Mussa Hassan Mgosi ndiye aliyeanza kuifungia
Mtibwa Sugar bao dakika ya nane baada ya kupiga krosi kali kutoka wingi
ya kulia ambayo ilidakwa na kipa Ivo Mapunda lakini shuti hilo
lilimparaza kipa huyo kabla ya mpira kujaa wavuni.
Katika mchezo huo ambao Mtibwa Sugar walitawala
sana katika eneo la kiungo, kipindi cha kwanza ilishuhudiwa Amri Kiemba
akikosa bao la wazi akiwa yeye na kipa dakika ya 19 baada ya shuti lake
kupaa juu ya lango.
Dakika ya 21 Mgosi aliyewahi kuwika na Simba,
alijaribu tena kumchungulia kipa Ivo Mapunda lakini shuti lake lilipaa
nje kidogo ya lango.
Dakika ya 36 kocha wa Simba Zdravko Logalusic
alifanya mabadiliko baada ya kumtoa Awadh Juma na kumuingiza Ali Badru
mabadiliko ambayo hayakuzaa matunda kwani hadi timu zinakwenda mapumziko,
Mtibwa ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 huku Mgosi akiwa mwiba mchungu kwa
beki wa kati wa Simba, Donald Mosoti ambaye alikuwa na kazi kubwa
kumkaba mshambuliaji huyo.
Simba ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kuweza
kusawazisha bao dakika ya 50 kwa shuti la chini la Amissi Tambwe
lililomshinda kipa wa Mtibwa, Hussein Sharrif ‘Casillas’.
Simba ilifanya mabadiliko tena dakika ya 51 kwa
kumtoa Chanongo na kumuingiza Uhuru Seleman na Mtibwa nao wakamtoa Juma
Luizio na kumuingiza, Vicent Barnabas.
Dakika ya 69, nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaban
Nditi alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kutoa lugha chafu kwa
mwamuzi mwanamke, Jonesia Rukyaa wa Arusha.
Kadi hiyo ilikuja baada ya beki Salvatory Ntebe
kumchezea rafu Tambwe na ndipo Nditi alipoanza kumlalamikia mwamuzi kwa
lugha chafu na kuambulia kadi nyekundu.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola
alisema wanakubali matokeo ingawa alidai uwanja ulichangia matokeo hayo
kwani wachezaji walishindwa kucheza kwa uhuru.
“Mechi ilikuwa nzuri tunakubali matokeo ingawa
lengo letu ni kupata pointi tatu lakini hata hii pointi moja tuliyoipata
si mbaya kwani imetusogeza juu na kupunguza gepu la pointi na walio juu
yetu lakini pia uwanja ulikuwa kikwazo si mzuri”alisema Matola.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema
timu yake imejitahidi na wanajipanga kwa mechi ijayo ili waweze kupata
matokeo mazuri ingawa akamlalamikia mwamuzi kuwa hakuchezesha kwa haki.
Baada ya mechi ya jana, Simba itacheza na Mgambo
Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kufuatiwa na mechi
nyingine Februari 15 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine,
Mbeya.
Vikosi
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!