WAKATI Manchester United ikionekana kukaribia kushinda mbio za
kumbakiza mshambuliaji wao tegemeo, Wayne Rooney imedaiwa kuwa mkewe,
Coleen Rooney ni sababu kubwa ya nyota huyo kuamua kubaki klabuni hapo.
Coleen amechangia kwa kiasi kikubwa mazungumzo ya
Rooney na Man United ambayo mwishowe yatamwona staa huyo akisaini
mkataba mpya wa miaka mitano huku akitarajiwa kulipwa kitita cha Pauni
300,000 kwa wiki.
Coleen anataka Rooney abaki Uingereza ili waweze
kuwalea vizuri watoto wao, Kai mwenye umri wa miaka minne na Klay mwenye
miezi minane.
Dili hilo lina thamani ya Pauni65 milioni na
litamfanya Rooney, 28, awe mwanasoka anayelipwa zaidi katika Ligi Kuu
England. Kwa sasa Rooney analipwa sawa na mshambuliaji mwenzake mahiri
wa Old Trafford, Robin Van Persie huku wote wawili wakichukua kiasi cha
Pauni 250,000 kwa wiki.
Rafiki wa Coleen ametoboa kuwa shoga yake huyo
ndiye chanzo cha Rooney kuachana na ndoto za kucheza Real Madrid ambayo
inapewa nafasi kubwa ya kumchukua kwa sababu Man United isingependa
kumwona akicheza timu nyingine ya Uingereza.
“Sababu kubwa ni kwamba Coleen hataki kuhama
kutoka Kaskazini Mashariki. Hilo pia ni muhimu kwa Wayne. Hana mpango wa
kuhama eneo hilo lakini pia pesa nyingi wanayotaka kutoa Man United ni
sababu pia,” alisema rafiki huyo wa Coleen.
“Coleen anaona ni muhimu kwa Kai na Klay kuwa
karibu na wanafamilia wengine. Hataki walelewe katika nchi nyingine au
eneo jingine la nchi hii. Lakini pia Coleen anafanya vizuri katika kazi
yake ya uanamitindo.”
Wapenzi hao wanaishi katika eneo la Prestbury,
Cheshire, na wazazi wa Coleen, Colette na Tony wanaishi maili 50 tu
kutoka hapo katika eneo la Formby, Merseyside, ambako ni karibu na
familia ya Rooney.
Hivi karibuni Coleen akizungumza na Gazeti la
Sunday Mirror alieleza namna ambavyo Rooney atapata wakati mgumu wa
kuishi bila ya msaada wa familia zao.
“Kutokana na asili ya kazi ya Rooney huwa haambiwi
kama kuna mapumziko mpaka baada ya mechi. Kwa hiyo inabidi tuzoee hali
hiyo kwa sasa. Na ndiyo maana wazazi wangu na wa Rooney wanasaidia sana
katika hali kama hii. Tusingeweza kufanikiwa bila ya msaada wa familia
zetu.”
Rooney na Coleen ambaye jina lake halisi ni Coleen
McLoughlin wamekulia pamoja katika kitongoji cha Jiji la Liverpool cha
Croxteth na walianza penzi lao katika mwaka wa mwisho wakiwa shule
wakati huo wakiwa na umri wa miaka 16 tu. Coleen alianza kujulikana
zaidi wakati Rooney alipoanza kuonyesha makali yake katika soka, Mei
2003 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji kinda zaidi kukipiga England.
Alikuwa na umri wa miaka 17.
Oktoba Mosi, 2003, Rooney alionyesha nia ya kumuoa
Coleen baada ya kumvalisha pete ya uchumba yenye madini ya almasi
ambayo ilikuwa na thamani ya Pauni 46,500.
Hata hivyo, Rooney alitia doa uchumba wao baada ya Agosti 2004
kukiri kwamba aliwahi kutembelea danguro la makahaba mnamo mwaka 2002
kitu ambacho kilimwacha Coleen katika mshtuko na mfadhaiko mkubwa.
“Sasa hivi inaonekana ni ujinga. Mara kadhaa
nilitembelea sehemu za makahaba. Ilikuwa ni wakati nipo mtoto na
sijapevuka,” alisema Rooney.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!