UJIO wa Juan Mata katika klabu cha Manchester United umeleta
utata mkali mno hasa kutoka kwa kocha wa Arsenal, ‘Profesa’ Arsene
Wenger ambaye kwa hakika amechukizwa na biashara ambayo Man United
ilifanya na Chelsea.
Mata nikimchambua kwa undani kiasi namkumbuka kuwa
ni kiungo hatari mno. Ni mchezaji ambaye amekuwa ndani ya kikosi cha
timu ya taifa ya Hispania kwa muda mrefu tangu mwaka 2009.
Katika soka duniani kote, Mata ni kati ya viungo
hatari, Chelsea kwa misimu miwili Mata alikuwepo pale Stamford Bridge
aliweza kupiga pasi za uhakika na kufunga mabao 18.
Alikuwa mchezaji bora wa Chelsea kwa misimu miwili
mtawalia. Duniani kiungo kupiga mabao18 si jambo dogo, inadhihirisha
uwezo alionao si tu katika kutengeneza pasi za kuzalisha mabao bali hata
kufunga inapobidi.
Kuna baadhi ya washambuliaji katika hizi klabu za juu ambao hata kufikisha mabao 10 pekeee kwa msimu mmoja inakuwa shida kubwa.
Tukirejea suala la Wenger kulalamikia biashara ya
Chelsea na Man United, swali langu ni hili hapa. Je Jose Mourinho na
Chelsea yake wangekuwa hawajacheza na Man United mzunguko wa pili
wangemuuza Mata?
Jibu langu ni la. Sijui wewe lakini Mourinho
amekuwa na mbinu chafu na anatafuta njia zozote za kulitwaa taji.
Anaihami Man United. Kumbuka Man United bado hawajakabiliana na Man
City, Liverpool na Arsenal.
Wenger anamfahamu Mata vilivyo hata akafikia hatua
ya kumtaka Emirates, matumaini ya Wenger msimu huu ni kuhakikisha
analibeba taji la Ligi Kuu England (EPL) ni matumaini ambayo yapo juu
mno.
Kutokana na mpango wake huo ndiyo maana anaziona
mbinu chafu zinazofanywa na Jose Mourinho za kumsimamisha katika mbio za
kulitwaa taji la EPL.
Mbinu za Jose Mourinho za kushinda mechi ni chafu,
kuanzia kwa kejeli na mambo mengine. Itakumbukwa Mourinho na Chelsea
yake walikuwa wameshaapa kwamba hawatomuuza Mata kwa Man United. Na hapa
ndipo unapojiuliza kulikoni kubadilika na mwisho wa siku kuamua
kuwauzia Man United mchezaji huyo?
Mata ni mchezaji hodari mno. Hadi sasa mechi mbili
ambazo amecheza ametoa pasi mbili za uhakika za mwisho. Ni kiungo
ambaye yupo kila mahali katika eneo husika pia ana chenga za maudhi.
Mourinho amepiga hesabu kuwa akiihami Man United
na silaha hatari kama Mata ataweza kupunguza makali ya Man City na
Arsenal. Man United haipo katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu
lakini inaweza na ina kila sababu za kutoa upinzani kwa Man City na
Arsenal na Mata na ushupavu wake anaweza kuwa sababu ya kutoa mwelekeo
wa mechi yoyote ile.
Kumbuka inahitaji ujasiri wa mchezaji mmoja tu kubadilisha timu
yoyote ile. Kumbuka ujio wa Robin Van Persie katika klabu ya Man United,
msimu mmoja tu ulibadilisha ligi na Man United waliweza kulitwaa taji.
Kwa wakati huu kiungo Mesut Ozil wa Arsenal ndiye
tegemeo kubwa katika klabu hiyo na ujio wake pale Emirates umebadili
mengi mno, pasi anazopiga za uhakika na za ukweli zinaifanya Arsenal
kuwa juu ya jedwali.
Anavyowatafuta washambuliaji ndugu zangu acha tuu.
Hadi natamani kurejea uwanjani. Arsenal kuwa kileleni ni juu ya
mchezaji mmoja tu, naye ni Ozil, angalia wakati Ozil hayupo uwanjani,
inakuwa ni wakati mgumu kwa Wenger na kikosi chake kuweza kuzikabili
timu pinzani.
Kwa hivyo Wenger akiteta kuhusu mauzo ya Mata
kwenda Man United inaeleweka, ana hoja ya msingi katika jambo hilo,
hapaswi kubezwa.
Mourinho mara nyingi ni aina ya kocha ambaye mbinu
zake ni chafu na za kihuni. Kumbuka anavyocheza mechi zake na timu
kubwa, atawapanga walinzi zaidi ya saba uwanjani. Na mshambuliaji mmoja
tu.
Kuna wakati mmoja akicheza na Barcelona, kwa
sababu anajua Barca ni timu ya kupiga pasi za haraka haraka alichofanya
ni kama kuharibu uwanja ambao uligeuka mfano wa uwanja wa farasi au
ng’ombe ambao walikuwa katika mbio za kuelekea malishoni na mwisho wa
siku Barca walilemewa kucheza soka pale.
Kwa hivyo mbinu za Jose Mourinho za kulitwaa taji
la msimu huu mojawapo ni kuihami Man United, hata kuipa silaha za
kuingamiza Man City na Arsenal.
Hata hivyo haitakuwa rahisi, Mourinho hatofanikiwa
katika mbinu zake hizo kwani Man City na makali yao ndugu zanguni
itakuwa kazi kubwa kuwasimamisha. Wakati Arsenal wakienda sare ya mabao
2-2 na Southampton, Man City waliiadhibu vikali Tottenham Hotspurs kwa
mabao 5-1, tena nyumbani kwao White Heart lane.
Nayo Chelsea ikapoteza mwelekeo walipoenda sare ya kutofungana na West Ham Utd nyumbani kwao Stamford Bridge.
Kocha wa Man City, Manuel Pellegrini hana tatizo,
karata zake anazicheza polepole, ameapa kutwa mataji yote manne msimu
huu. Capital One, FA, EPL pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hadi sasa EPL inazidi kunoga. Je ni Man City, Arsenal, Chelsea au Liverpool watalitwaa taji la msimu huu?
Bado zaidi ya mechi 15 kwa kila klabu kucheza. Hizo ni pointi 45. Ukweli atakayeteleza kwa sasa, Watetezi wa ligi hiyo Man United washatolewa. Kupoteza mechi dhidi ya
Stock City Jumamosi iliyopita ilikuwa dhahiri kwao kwamba ligi ya msimu
huu si yao, na hata kumaliza nne bora itakuwa ni ishu kubwa.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!