Jose Mourinho ana dharau sana. Ameidharau Arsenal baada ya kudai
kwamba wapinzani wao hao walikuwa ‘chamtoto’ walipoikabili timu yake
juzi Jumamosi na Mreno huyo anasema Chelsea ilimaliza mechi ndani ya
dakika saba tu.
Kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu England, Mourinho
aliiongoza Chelsea kuichapa Arsenal ya Arsene Wenger mabao 6-0 uwanjani
Stamford Bridge na hivyo kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi
hiyo.
Mourinho alisema aliwaagiza wachezaji wake
waivuruge Arsenal na staili yao ya uchezaji na hadi zilipotimia dakika
saba za mwanzo baada ya mabao ya Samuel Eto’o na Andre Schurrle mechi
ilikuwa imemalizika, kwa mujibu wa tambo zake.
“Nadhani tulianza vizuri sana, dakika saba tu tulikuwa mbele 2-0 na mechi iliishia pale,” alisema Mourinho.
“Tulianza mechi kwa nguvu sana na hatukutaka
kuwapa nafasi Arsenal. Tulijaribu kuwakaba na kuwashambulia kwa haraka.
Baada ya mabao yale mawili, ilikuja penalti na kadi nyekundu ambayo
ilikuwa mbaya sana kwao. Nadhani mechi nzima ilikwisha kila kitu ndani
ya dakika 10 za mwanzo.”
Kwenye mchezo huo, mwamuzi Andre Marriner alimtoa
kimakosa kwa kadi nyekundu beki Kieran Gibbs, licha ya kwamba Alex
Oxlade-Chamberlain ndiye aliyekuwa ametenda kosa wakati alipocheza kwa
mkono makusudi dhidi ya shuti la Eden Hazard.
Mourinho alisema: “Namwonea huruma refa. Kulikuwa
na watu wengi sana kwenye boksi na baada ya shuti la Hazard kulionekana
mchezaji ameruka kama kipa. Msaidizi wangu mmoja alisema alikuwa (Mikel)
Arteta, mwingine alisema Chamberlain na refa au msaidizi wake alisema
Gibbs. Yalikuwa maamuzi magumu. Kuhusu penalti ilikuwa penalti na kadi
nyekundu ilistahili. Bahati mbaya imetolewa kwa kijana asiyekuwa na
hatia.”
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!