Straika namba moja wa Simba mwenye asili ya Burundi, Amissi
Tambwe ametoa ya moyoni baada ya kutamka hadharani kwamba anatamani
angekuwa anacheza na mawinga wenye kasi na ubora kama wa Yanga kwani
makipa na mabeki wangemtambua.
Tambwe mwenyewe amesisitiza
kwamba angekuwa na wachezaji hao mpaka sasa angekuwa amepachika mabao
mengi na kazi yake ingekuwa rahisi zaidi tofauti na sasa ambapo amekuwa
akitumia nguvu nyingi zaidi Simba kutokana na aina ya uchezeshaji.
Yanga mara nyingi inawachezesha mawinga wenye kasi
ambao ni Simon Msuva, Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi huku washambuliaji
wa kati wakisimama Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa wakati mwingine Said
Bahanuzi ambaye hana uhakika wa namba kikosini.
Tambwe alisisitiza licha ya upinzani wa Simba na
Yanga lakini mtu akifanya kitu kizuri kiuanamichezo husifiwa, alisema
kuwa mawinga wa Yanga wana uwezo mkubwa wa kupiga krosi na kutengeneza
pasi nzuri za kufunga mabao.
“Ujue siku zote katika mechi zetu, mara nyingi
utanikuta nipo katika eneo la 18 nikisubiria pasi na krosi kutoka kwa
mawinga na viungo wenye jukumu la kunichezesha ikiwemo kunipa pasi na
krosi nzuri za kufunga mabao.
“Vitu ambavyo sivipati kwa ubora unaostahili
Simba, ninaamini kama timu yangu ingekuwa na mawinga wazuri kama wa
Yanga wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi na pasi nzuri za kufunga, basi
ningefunga mabao mengi hadi sasa katika Ligi Kuu.
“Kiukweli kabisa tuweke pembeni upinzani wetu,
ninaipenda sana kombinesheni na aina ya uchezaji wanayoitumia Yanga
ndani ya uwanja, ujue mimi kazi yangu kufunga mabao, hivyo ni lazima
nipewe mipira mizuri ya kufunga,”alisema Tambwe ambaye habari za ndani
zinadai kwamba baadhi ya vigogo wa Kundi la Friends of Simba wanajipanga
kumtumia kama chambo kwenye kampeni za uchaguzi wa Simba mwezi ujao.
Mchezaji huyo ana mkataba wa miaka miwili na
Simba, lakini wamekubaliana msimu wa kwanza ukimaliza watakaa chini
kujadiliana jinsi ya kuendelea na mwaka wa pili.
Habari zinadai kwamba vigogo hao wamepanga kumlipa
fedha za mkataba wa mwaka wa pili na kumhakikishia maisha mazuri Simba
na watatumia upenyo huo kama sehemu ya kampeni za uchaguzi wa mwezi
ujao.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!