Sheikh Ahmad Madobe, Rais wa eneo lililojitangazia mamlaka ya ndani la
Jubaland lililoko kusini mwa Somalia, ameyataka majeshi ya Ethiopia
yaendelee kubaki nchini humo. Mwaka uliopita, serikali ya Somalia
iliafiki kulipatia eneo la Jubaland mamlaka ya ndani, lakini hadi hivi
sasa bado haijatoa ruhusa hiyo kwa eneo la Somaliland. Majeshi ya
Ethiopia yakishirikiana na majeshi ya serikali ya Somalia na vikosi vya
kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, yanatekeleza operesheni za
pamoja dhidi ya kundi la al Shabaab kwa lengo la kulitokomeza kikamilifu
kundi hilo la kigaidi. Kabla ya hapo, serikali ya Ethiopia ilisisitiza
kuendelea kuyabakisha majeshi yake nchini Somalia. Viongozi wa Ethiopia
wamesisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya al Shabaab, na hasa kutokana
na hofu ya kusambaa mashambulizi ya kundi hilo kwenye mipaka ya pamoja
ya nchi hizo mbili. Wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa, wasiwasi wa
serikali ya Ethiopia ni wa kimantiki, kwani mpaka wa pamoja na nchi
hizo mbili unakaribia urefu wa kilomita 1,600. Imeelezwa kuwa, sababu ya
majeshi ya Kenya nayo kuingia ndani ya ardhi ya Somalia mwezi Oktoba
2011, ilitokana na hatari ya kiusalama iliyokuwepo nchini humo.
Kuongezeka harakati za kundi la al Shabab nje ya mipaka ya Somalia,
kumetishia mno usalama wa nchi za eneo la Mashariki mwa Afrika. Licha ya
hayo, mashambulio ya kundi hilo yamesababisha kupungua safari za
watalii wa kigeni nchini Kenya, ambapo uchumi na maisha ya wananchi wa
nchi hiyo yanategemea zaidi pato la sekta ya utalii. Kabla ya hapo,
viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kieneo ya IGAD walichukua
maamuzi ya kukomesha machafuko nchini Somalia, kwa kuimarisha
mashirikiano yao na serikali ya Mogadishu, sanjari na kupelekewa nchini
Somalia wanajeshi wa Ethiopia mwezi Novemba mwaka 2011. Hatua ya
viongozi wa IGAD ya kubariki kuingia majeshi ya Kenya na Ethiopia nchini
Somalia, imeandaa mazingira ya kushirikishwa nchi hizo mbili kwenye
operesheni za vikosi vya AMISOM. Umoja wa Afrika ambao ndio unaoongoza
vikosi vya kulinda amani nchini Somalia, unatarajia kupitisha rasmi
mpango wa kushirikishwa majeshi ya Kenya kwenye operesheni za AMISOM
mwezi Januari mwakani. Mwaka uliopita, majeshi ya Ethiopia
yaliunganishwa rasmi kwenye vikosi vya Umoja wa Afrika vya kulinda amani
nchini Somalia. Kundi la al Shabaab lilitoa radiamali na kufanya
shambulio katika jengo la maduka ya biashara Westgate jijini Nairobi
mwaka jana, na kutishia usalama wa nchi zote zinazopanga mikakati ya
kulitokomeza kundi hilo. Bila shaka, mwaka jana wanamgambo wa al Shabaab
walishindwa vibaya kwenye medani za mapigano na majeshi ya serikali ya
Somalia, Ethiopia na Kenya na hatimaye kupoteza udhibiti wa maeneo mengi
waliyokuwa wakiyadhibiti. Alaa kullihaal, wiki mbili zilizopita,
Msemaji wa al Shabaab alisema kwamba viongozi wa kundi hilo wameazimia
kuyateka tena maeneo yote waliyokuwa wakiyadhibiti mwaka 2013. Kwa
mtazamo wa kundi la al Shabaab, ardhi yote ya Somalia inafungamana na
kundi hilo, na serikali ya Somalia ambayo inaungwa mkono na Umoja wa
Mataifa na jamii ya kimataifa ni vamizi tu na majeshi yote yanapaswa
kuondoka nchini humo. Shambulio la hivi karibuni la kundi hilo dhidi ya
Ikulu ya Rais na mlipuko wa bomu uliotokea uwanja wa ndege wa Mogadishu,
yalifanyika kwa sababu hizohizo. Inaonekana kuwa, takwa la Sheikh Ahmad
Madobe kiongozi wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Jubaland la
kubakishwa majeshi ya Ethiopia nchini Somalia, linatokana na woga wa
kufanyika mashambulio mapya ya kundi la al Shabaab kwenye maeneo
liliyokuwa likiyadhibiti na ambayo sasa yanadhibitiwa na vikosi vya
AMISOM. Inafaa kuashiria hapa kuwa, sisitizo la Abdiweli Sheikh Ahmed
Waziri Mkuu wa Somalia la kutokomezwa kundi la al Shabaab hadi ifikapo
mwishoni mwa mwaka 2014, limelikasirisha kundi hilo na ndio maana
limeamua kuendeleza mashambulio dhidi ya majeshi ya serikali na
waitifaki wake. Hii ni katika hali ambayo, wananchi na serikali
zinazoiunga mkono Somalia, zinaunga mkono utekelezwaji wa operesheni za
kulitokomeza kundi hilo ambazo zitasaidia kurejeshwa amani na utulivu
kwenye nchi zao na eneo lote la Mashariki na Pembe ya Afrika.
Home »
siasa afrika
» MAJESHI YA ETHIOPIA YAOMBWA KUSALIA SOMALIA
MAJESHI YA ETHIOPIA YAOMBWA KUSALIA SOMALIA
Written By Unknown on Friday, 7 March 2014 | Friday, March 07, 2014
Labels:
siasa afrika
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!