Ligi Kuu ya soka ya nchini England inaelekea ukingoni na ndoto
za mabingwa watetezi, Manchester United za kuendelea kubaki na kombe
hilo zimepeperuka baada ya kushuhudia vipigo vingi, hasa nyumbani kwao,
Old Trafford.
Huu ni uwanja ambao katika miaka mingi ya kocha
Sir Alex Ferguson ilikuwa ngome inayoogopwa na wachezaji na makocha wa
timu pinzani, lakini tangu msimu huu umeanza wakiwa chini ya David
Moyes, mambo yamegeuka.
Man United imekuwa timu ya kubezwa, ambayo
imefungwa na timu nyingi ndogo, baadhi ikiwa ni mara ya kwanza katika
historia zao kuwafunga Mashetani Wekundu, mfano Swansea.
Rekodi nyingi zimewekwa na kuvunjwa, lakini kwa
upande hasi kwa United ambao sasa wanajaribu kujitutumua ili walau
wacheze Ligi ya Europa japokuwa vigingi mbele yao bado ni vingi kwa
jinsi timu nyingine zinavyowawekea kauzibe.
Athari za matokeo hayo kisaikolojia zinamuumiza
zaidi kocha ambaye aliona ni heshima kubwa sana kupata nafasi ya
kuwafundisha mabingwa hao na moja ya klabu zinazoheshimika zaidi
duniani.
Lakini matokeo haya naathiri pia chapa ya Ligi Kuu
ya England (EPL) machoni pa ulimwengu wa michezo, kwa sababu kimsingi
kutetereka huko kunashusha kwa namna fulani hadhi ya ligi yenyewe.
Hii ni kwa sababu za anguko la Manchester United
haziishii ndani tu, bali pia nje ya nchi, kwa sababu kwa mfano kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) licha ya kufika hatua ya robo fainali,
ilikuwa bahati zaidi kuliko uwezo.
Tunakumbuka bado jinsi Olympiakos walivyowaadhiri
kwenye mchezo wa kwanza na kuwafunga 2-0, timu ambayo ni ndogo
ikilinganishwa na United.
Lakini pia mchezo dhidi ya Bayern Munich ambapo United walilazimisha sare, ‘waliegesha basi’ ndiyo maana winga wa Wajerumani hao, Arjen Robben akasema ilikuwa kana kwamba United wanajihami kwenye mpira wa mikono.
Lakini pia mchezo dhidi ya Bayern Munich ambapo United walilazimisha sare, ‘waliegesha basi’ ndiyo maana winga wa Wajerumani hao, Arjen Robben akasema ilikuwa kana kwamba United wanajihami kwenye mpira wa mikono.
Mtaalamu wa masuala ya soka na biashara kuhusiana
na chapa na matangazo, Evans Brighton anasema kwamba hii ni sawa na
panga lenye kukata kuwili kwa sababu klabu kubwa kama hii inapoanza
kufanya mambo ya ovyo, inapunguza washabiki kwenye ligi husika na
kidogokidogo mapato.
Hii ni timu iliyopata kutwaa ubingwa wa England
mara 20, ikawa na kocha aliyesifika kote duniani na kuna watu waliokuwa
wakiweka fedha zao kwenye ligi hii kwa sababu ya timu, kocha wake, aina
ya wachezaji waliopo au hata wamiliki kwa maana ya uhakika wa kufanya
vyema.
Lakini moja ya klabu kubwa kama hii inapodondoka
tafsiri yake kimataifa ni kwamba na utamu wa ligi unaweza pia kuwa na
tatizo, watu wakaamua kuelekeza macho yao kwenye ligi nyingine.
Ikumbukwe kwamba Ligi Kuu England ndiyo sasa
maarufu zaidi kote duniani, lakini kadiri miaka inavyokwenda watu
wanakuja na hoja kinzani, wakianza kutupia macho Bundesliga (Ligi Kuu
Ujerumani), La Liga (Ligi Kuu Hispania) na hata Ligue 1 (Ligi Kuu
Ufaransa).
Katika viwango vya klabu 20 bora duniani vilivyotolewa hivi
karibuni na wataalamu wanaochambua masuala ya soka, Manchester United
imetupwa nje. Walau kubaki kwa Chelsea kwenye timu nne zilizoingia nusu
fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kunaweza kuisaidia nchi hii, lakini
nao pia walipita kana kwamba kwa bahati, kwenye timu ambayo kocha
anawabeza washambuliaji wake kila uchao.
Kwa hiyo unahitajika uwiano fulani kuhakikisha
kwamba timu zina nguvu, zinashindana kweli kweli na si kushiriki tu.
Kuanzia mwaka jana hadi 2016, kwa dili lililoingiwa na Bodi ya Ligi Kuu
na wadau, vituo vya televisheni vya ng’ambo viliingizia EPL kitita cha
Pauni 3 bilioni kwa mwaka jana tu.
Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha na wakati dili
linasukwa na vituo hivyo kwa ajili ya kudaka na kurusha matangazo ya Sky
na BT Manchester United ndio walikuwa mabingwa, lakini sasa upepo
umebadilika.
Man U hawatakuwa tena kwenye Ligi ya Mabingwa
Ulaya, watatakiwa kusubiri labda hadi Septemba 2015, kama watakuwa
wamejijenga ili kuingia humo tena.
Ni kitu ambacho washabiki wa United hawakuwa
wamezoea, kwani kila mwaka, tangu miaka 19 iliyopita, wengi wao walikuwa
na uhakika wa kama si ubingwa basi nafasi ya pili au ya tatu na hivyo
ndivyo timu inasuka mashabiki na ligi kupendwa hivyo pesa kumwagwa
kutoka kila kona ya dunia.
Athari nyingine za hali hii, japokuwa Kocha Moyes
anapinga, ni kukosa saini za wachezaji muhimu. Ni wazi kwamba United
wanatakiwa kupangua vijeba wengi waliomo pamoja na wachezaji wasioonesha
ama uwezo au kujituma.
Licha ya kuwa nilishaandika mara nyingi juu ya
ajabu ya mabadiliko haya wakati wachezaji ni walewale waliotwaa ubingwa
msimu uliopita, ni wazi baadhi watajiondoa wenyewe, wengine wapelekwe
kwa mkopo kwingine na baadhi kuuzwa kabisa.
Inaelezwa kwamba mamilioni yametengwa kwa ajili ya
usajili wa haja na kwamba washabiki hawatakiwi kuwa na wasiwasi kwa
vile matatizo haya ni ya msimu huu tu. Lakini lazima waelewe kwamba
wachezaji nyota wanapenda timu iliyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na
United hawamo humo.
Ni wakati huu mahasimu wakubwa wa kitaifa wa
United, Liverpool wanafanya vizuri pia msimu uliopita United walimaliza
ligi wakiwazidi The Reds kwa pointi 38! Msimu huu wapo nyuma yao kwa
pointi 17!
Pia watani wa jadi katika Jiji la Manchester,
yaani Manchester City nao wanang’ara sana. Washabiki wa Mashetani
Wekundu wanajiuliza; maisha bila Ligi ya Mabingwa Ulaya yatakuwaje?
Wengine wanahoji iwapo ndio mwanzo wa kuanguka kwa ufalme wa Old Trafford au ni kuteleza tu.
Kazi kubwa iliyo mbele ya Moyes, ambaye inaelekea
Makamu Mwneyekiti, Edward Woodward na wamiliki Familia ya Glazer bado
wana imani na Moyes na watampa kitita ili atafute wachezaji. Msimu
uliopita alipewa fedha nyingi lakini alifanikiwa kumnasa mchezaji mmoja
tu tena siku ya mwisho, naye ni mchezaji wake wa zamani pale Everton,
Marouane Fellaini ambaye hajawasaidia sana United zaidi ya kupewa kadi
za njano na nyekundu na wakati mwingine kuhurumiwa na waamuzi tu
kutokana na mchezo wake wa rafu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!