Siku kama ya leo miaka 98
iliyopita makubaliano ya kihistoria ya Sykes-Picot yalitiwa saini na
wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja
wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi
ya Bolshevik. Serikali za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za
Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania, kwa mujibu
wa makubaliano hayo. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya
udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa.
***************************************************************
Miaka 361 iliyopita katika
siku kama hii ya leo kazi ya kujenga jengo la Taj Mahal ambalo
linahesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja
kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India
ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza
baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa Kimogholi wa India
huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani
iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani.
Kwa upande wa nje, jengo la
Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake
zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu.
Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe,
Nur Jahan.
***************************************************************
Na tarehe 9 Rajab mwaka 963
Hijria alifariki dunia Izzuddin Sayyid Hussein ambaye alikuwa miongoni
mwa maulamaa wakubwa wa karne ya 10 wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 906
Hijria katika kijiji kimoja cha Jabal Amil nchini Lebanon na kupata
elimu katika eneo hilo. Izzuddin Sayyid Hussein alifikia daraja za juu
za kielimu ya kiirfani. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alifariki dunia
katika siku kama hii ya leo kwa kupewa sumu katika mji wa Saida
(Sidon).
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!