Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kupambana na Mihadarati
nchini Kenya (NACADA), Bw. John Mututho, amesema idadi ya watu
waliopoteza maisha kutokana na unywaji wa pombe yenye sumu wamepindukia
90. Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya simu, Mututho amesema watu
wengine zaidi ya 200 wamelazwa hospitalini kutokana na kunywa pombe
hiyo. Mkuu huyo wa Nakada amesema hatua kali zitachukuliwa kwa
waliotengeneza, kusambaza na kuuza pombe hiyo yenye sumu ambayo
imesababisha maafa katika kaunti 6 za nchini Kenya.
Huku hayo yakijiri, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya
ametangaza kuwafuta kazi maafisa 52 wa serikali kutokana na tukio hilo.
Joseph Ole Lenku amesema waliofutwa kazi ni pamoja na maafisa waandamizi
katika jeshi la polisi, Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA na mwenzake wa
kitengo cha kutathmini ubora wa bidhaa (ACA) pamoja na maafisa katika
Mamlaka ya Ushuru.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!