Rais Abd Rabbuh Mansour Hadi wa Yemen amelaani vikali uchokozi na
mashambulizi yanayofanywa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni wa Israel
dhidi ya wananchi wa Palestina na kusisitiza juu ya kuungwa mkono
juhudi za wananchi wa Palestina za kukabiliana na uchokozi na chokochoko
zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina. Akizungumza
kwa njia ya simu na Khalid Mash'al Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati
ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina 'Hamas', Rais Abd Rabbuh Mansour
Hadi amesisitiza kwamba serikali na wananchi wa Yemen wanaunga mkono
haki ya wananchi wa Palestina ya kuainisha mustakbali wao wa kuundwa
serikali huru kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwenye mazungumzo hayo,
Khalid Mash'al naye amezitaka nchi za Kiarabu kuchukua msimamo mmoja na
madhubuti wa kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel, ili urejeshe haki
za wananchi wa Palestina.
Kiongozi wa Hamas amesema kuwa, utawala wa
Israel unatekeleza jinai za kivita na zilizo dhidi ya binadamu siku hadi
siku na kukanyaga sheria za kimataifa. Mash'al amesema kuwa taasisi za
kimataifa zinapasa kuchukua hatua za kuwafungulia mashtaka viongozi wa
utawala huo ghasibu. Kiongozi wa Hamas amezitaka taasisi za kimataifa,
watetezi wa haki za binadamu kote duniani kuchukua msimamo thabiti wa
kukabiliana na uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Israel dhidi ya
wananchi wa Palestina.

0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!