ACHANA na vita ya Barcelona na Real Madrid, mchuano wa tuzo ya Ballon d’Or (mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa) na umahiri wa ndani ya uwanja. Wanasoka Lionel Messi na Cristiano Ronaldo vita yao ya sasa ni kufukuzia rekodi ya Raul kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pamoja na kuwapo mchuano huyo, wako wanasayansi wanaosema kwamba, Messi staa wa Barcelona ataendelea kutamba.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi hao kutoka
kwenye vyuo vikuu tofauti duniani umebainisha siri kubwa inayomfanya
Messi azidi kumfunika Ronaldo kwa ujuzi wa ndani ya uwanja na jambo hilo
ndilo linalomfanya staa wa Ureno (Ronaldo) awe wa kushika nafasi ya
pili nyuma ya Muargentina huyo.
Madai ya wanasayansi
Wataalamu hao wamefanya utafiti wao na kufichua
kwamba wachezaji wanaotumia mguu wa kushoto wana uwezo mkubwa kiakili na
ndio maana Messi amemzidi uwezo Ronaldo.
Utafiti huo uliofanyika katika vyuo vikuu vya
Oxford, St. Andrews na Bristol, unasema kwa kuwa Messi anatumia mguu wa
kushoto, ubongo wake unafanya kazi kubwa sana anapokuwa ndani ya uwanja
pengine mara mbili zaidi ya Ronaldo.
Wachezaji wanaotumia mguu wa kushoto ubongo wao
unafanya kazi kwa haraka sana na kufanya mambo yasiyotarajiwa tofauti na
ilivyo kwa wanaotumia mguu wa kulia.
Baadhi ya wachezaji waliotajwa kwenye utafiti huo
wanaotumia mguu wa kushoto na kufanya mambo makubwa ndani ya uwanja ni
pamoja na David Silva, Messi, Gareth Bale, Diego Maradona, Mesut Ozil na Ryan Giggs na kupitia nyota hao wachache, unaweza kutambua umakini na viwango vyao wanapokuwa uwanjani.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hiyo ndio sababu
inayomfanya Ronaldo ashindwe kumfunika Messi kwa ujuzi na ubunifu wa
ndani ya uwanja, licha ya wawili hao kutajwa kuwa ndio wanasoka walio
kwenye ubora mkubwa wanaotamba duniani kwa sasa.
Kufukuzia rekodi ya Raul
Wakati wanasubiri Ballon d’Or Januari mwakani,
Ronaldo na Messi kwa sasa wapo kwenye vita mpya ya kufukuzia rekodi ya
mabao iliyowekwa na Mhispaniola, Raul Gonzalez Blanco, kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Staa huyo amefunga mabao 71 kwenye michuano hiyo mikubwa na alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 33 kabla hajastaafu soka.
Mabao yake yamebaki kuwa rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa, ilimchukua mechi 144 staa huyo wa zamani wa Real Madrid na Hispania kuweka alama zake katika michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi za klabu barani Ulaya.
Wakati akiwa ameondoka zake kwenye soka, nyuma ameacha vita ya mafahari wawili wanaoshindania kuifukuzia rekodi yake. Watu hawa ni mahasimu wakubwa, Messi na Ronaldo.
Nani ataifikia rekodi ya Raul?
Msimu huu, Messi anacheza akiwa na umri wa miaka 26, wakati mpinzani wake ana miaka 28.
Mastaa hawa wana nafasi kubwa ya kuifikia rekodi ya Raul tena wakiwa pungufu kwa karibu mechi 50.
Achana na mbio za kuwania Mpira wa Dhahabu, vita
hii ya Messi na Ronaldo kwenye kumfukuzia Raul haitakuwa na pointi za
kupigiwa kura, bali ni idadi ya mabao watakayofunga katika michuano hiyo
mikubwa ili kumpiku Mhispaniola huyo.
Msimamo wa mabao ulivyo
Messi ameshika usukani kwa kufikisha mabao 65,
sita tu kuifikia rekodi hiyo ya Raul wakati Ronaldo anafuatia kwenye
nafasi ya pili na mabao yake 59.
Kwenye 10 bora
ya wenye mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Ronaldo na Messi
tu ndio pekee wanaoendelea kucheza michuano hiyo hadi sasa.
Wakali wengine wenye mabao mengi ni Mdachi Ruud van Nistelrooy
(56), Thierry Henry (50), Alfredo Di Stefano (49), Andriy Shevchenko
(48), Eusebio (46), Philippo Inzaghi (46) na Didier Drogba (42).
Vita yao inavyokwenda
Ronaldo amefikisha mabao 59 katika mechi 96, wakati Messi mabao
yake amefunga baada ya kucheza mechi 82. Kama Ronaldo ataendeleza rekodi
yake ya wastani wa mabao anaofunga kwenye kikosi cha Real Madrid na akicheza kila mechi hadi fainali, atakuwa na mabao tisa zaidi.
Rekodi za sasa zinaonyesha amefunga mabao manane
katika mechi nne, sawa na wastani wa mabao mawili kwa kila mechi.
Akiendelea kufanya hivyo anaweza kufunga mabao 18 zaidi na jambo hilo litamfanya kufikisha mabao 77.
Ni jambo linaloonekana gumu kiuhalisia, lakini kwa
Ronaldo kitu kama hicho kinawezekana. Akifanikiwa hilo atakuwa amefunga
mabao 222 katika mechi 215 kwenye kikosi hicho cha Real Madrid.
Lakini, kwa Ronaldo kumfikia Raul ni lazima ampiku
kwanza Messi. Staa huyo wa Barcelona alifunga mabao mawili Jumatano
iliyopita kwenye mechi dhidi ya AC Milan na rekodi yake ni kwamba amefunga mabao sita katika mechi tatu msimu huu.
Kwa kuendelea na rekodi hiyo na akioongoza Barcelona hadi fainali, Muargentina huyo atakuwa amefikisha mabao 83.
Wawili hao wote wanayo nafasi ya kuivunja rekodi
ya mabao ya Raul ambaye bao lake la mwisho la Ligi ya Mabingwa Ulaya
alilifunga kwenye robo fainali miaka miwili iliyopita akiwa na kikosi
cha Schalke 04.
Kwa hali ilivyo kwa sasa, kama rekodi hiyo ya Raul itashindwa kuvunjwa msimu huu, basi
mwakani atakuwa Messi au Ronaldo watakaoandika majina yao katika kurasa
za kihistoria, lakini jambo hilo haliwezi kufika mwakani mechi bado
nyingi msimu huu na wakali hao wanatarajiwa kuendelea kutikisa nyavu.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!