UGONJWA wa mashabiki kumpenda sana staa mpya wa Barcelona na
timu ya taifa ya Brazil, Neymar, umekithiri na sasa kinda huyo mwenye
sura ya mvuto amewaomba mashabiki wake wasiingilie sana maisha yake
binafsi.
Ingawa ana tabia za kitoto, kiasi cha kutuma picha
zake kila mara katika mtandao wa Instagram, Neymar amenyoosha mikono
kwa mashabiki wake na kuwaomba wamuweke mbali. Hiyo ni kutokana na
kumsumbua mara kwa mara nje ya uwanja wa soka.
Mashabiki hao wanasadikiwa kuwa wa nchini kwake
Brazil ambako amekuwa akihusudiwa kuliko mchezaji mwingine yeyote nchini
humo huku wengi wakiweka matumaini ya kutwaa Kombe la Dunia nchini mwao
mwakani kupitia yeye.
Katika barua ya wazi aliyowaandikia mashabiki wake
wenye wazimu wa kumpenda unaojulikana kwa jina la Neymarzetes, Neymar
ameeleza jinsi anavyolazimika kubadilisha namba yake ya simu kila siku.
“Ninawapenda sana na sijui kama ningefika hapa
nilipofika bila ya wao,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ambayo aliituma
katika mtandao wa Instagram.
“Nimeshindwa kutunza namba yangu ya simu kwa walau
wiki mbili kwa sababu watu wanaojiita mashabiki-Neymarzetes – huwa
wananipigia simu mida ya asubuhi au kunitumia meseji. Mbaya zaidi
wanagundua pia namba za simu za watu wa familia yangu, rafiki yangu wa
kike, wanatunga stori nyingi na uongo na mwishowe naishia kubadilisha
namba yangu ya simu.”
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 kutoka katika
Jiji la Sao Paolo, hajapata matatizo katika kuizoea Ligi Kuu Hispania
lakini nje ya uwanja amekuwa na wakati mgumu wa kupata usingizi kutokana
na kusumbuliwa na mashabiki wa nyumbani kwao Brazil.
“Ninawaomba kwa moyo wangu wote kwamba kila
anayenipenda mimi na ambaye amekuwa na mimi tangu mwanzo, kama kuna mtu
anamjua anafanya hivi tafadhali amshauri aache tabia hiyo. Sijui kitu
kingine cha kufanya,” aliongeza.
Neymar amejitahidi kuishi maisha ya kawaida tangu
alipotua Barcelona akitokea Santos katika kipindi cha majira ya joto
kilichopita. Ameondoa staili yake ya nywele maarufu kwa jina la Mohican
na ameendelea kujaribu kuishi chini ya kivuli cha Messi.
Hata hivyo, mpaka sasa ameshindwa kabisa kuwadhibiti watu wanaoipata namba yake ya simu kwa njia za panya.
“Sijui nifanye kitu gani kingine. Hawa watu wananisababishia matatizo sana. tafadhali niacheni niishi kwa amani,” analalamika.
Kwa sasa Neymar amekuwa katika penzi zito na mrembo, Bruna
Marquezine, mwenye umri wa miaka 17. Mrembo huyo ambaye jina lake kamili
ni Bruna Maia Reis in Duque De Caxias, amekuwa staa wa tamthiliya za
televisheni nchini Brazil huku akifanya kazi za uanamitindo.
Tangu mwaka 2003, Bruna ameshinda tuzo 11 akiwa
ameanza kuigiza tangu akiwa na umri wa miaka minane. Alianza maisha ya
kazi hiyo akiwa kando ya mtangazaji maarufu wa Brazil, Xuxa.
Kwa kuwa na uhusiano na Neymar, Bruna, ambaye
alikuwapo uwanjani wakati Neymar akitambulishwa kuwa mchezaji wa
Barcelona, anakuwa na bahati ya kuwa katika penzi na mmoja kati ya
wanasoka wenye mvuto ndani na nje ya uwanja.
Neymar alisaini mikataba mingi akiwa na umri wa
miaka 17 tu wakati jina lake linachomoza kwa kasi Santos. Machi 2011,
alisaini mkataba wake wa kwanza na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike
akiwa na umri wa miaka 11 tu.
Katika mwezi huo huo alisaini mkataba wa miaka
miwili na kampuni ya Panasonic ambao ulikuwa na thamani ya Dola 2.4
milioni. Neymar pia alisaini mikataba na kampuni za Volkswagen, Tenys Pé
Baruel, Lupo, Ambev, Claro, Unilever na Santander.
Kwa mikataba yake yote hiyo, Neymar anakusanya
kiasi cha Euro 20 milioni kwa mwaka. Mei 2013, alitajwa kuwa
mwanamichezo mwenye soko zaidi duniani mbele ya Lionel Messi aliyeshika
nafasi ya pili na Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya nane.
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!