UKIFIKA katika mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam utaanza kuhisi kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho ya wengi huanza kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba anayoishi msanii huyo.
Muda wote geti hilo limefungwa. Ili uweze kuingia
ndani itakulazimu ubonyeze kengele itakayoashiria kuwa kuna mgeni nje
anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi kupenya kirahisi ndani hadi
uulizwe shida yako na kama hauna miadi na mtu yeyote anayeishi ndani ya
nyumba hiyo haitakuwa rahisi kuingia.
Mapaparazi wetu walitinga
katika nyumba ya msanii huyo na kushuhudia ukimya wa hali ya juu ilhali
kuna watu ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na kupokewa
na Diamond aliyekuwa ameketi katika sebule iliyonakshiwa na mapambo
makini ukutani huku ikiwa na samani chache lakini za gharama kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika mahojiano na
Diamond ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na kujibu kwa
ufasaha na ufafanuzi mpana.
Mapaparazi wetu: Utendaji kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini katika kazi zangu.
Mambo yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo yanifikie mimi, mara
nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja kwa moja lazima apite huko na
hiyo ndiyo staili ya Diamond. Nimejipanga kuhakikisha nafanya kazi gani,
kwa wakati gani na sikurupuki tu, japo katika utengenezaji wa nyimbo
zangu naweza nikapata wazo basi hapo hapo nikatengeneza mistari.
Mapaparazi wetu: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia asubuhi hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi, nikishaamka kitu cha
kwanza ni kwenda ‘gym’, mara nyingi ni hapa nyumbani kama unavyoona hapo
nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu nyingine zilizopo ndani, mara
nyingi hutumia muda wa saa moja. Ifikapo saa sita na nusu huwa naanza
kufanya kazi zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo ndio
mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo napumzika kwa muda
fulani na baadaye jioni huendelea na kazi na mara nyingi kazi zangu huwa
nazimaliza usiku wa manane.
Mapaparazi wetu: Unalala saa ngapi? Na unalala kwa muda gani?
Diamond: Muda wangu wa kulala
mara nyingi ni saa kumi na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi nyingi
studio basi nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita
mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema kuamka ni saa tano
asubuhi ila itategemea na nini ninakifanya siku inayofuata na kama nina
kazi maalumu na ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mapaparazi wetu: Shughuli gani zinazokuchelewesha mara kwa mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati
mwingine shoo. Kwa wiki ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku
zote tatu nitalala alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa
manane kwa kuwa huwa nakuwa studio na sehemu nyingine ambazo hunilazimu
kufanya kazi kwa kipindi kirefu usiku.
Mapaparazi wetu: Kati ya usiku na mchana ni muda upi unaopenda kurekodi?
Diamond: Kazi zangu narekodi
usiku na ndiyo muda ninaopendelea zaidi. Mara nyingi napenda kurekodi
saa 7 usiku ili niwe na muda na saa nyingine ni kuepuka lawama kurekodi
mchana, kwasababu vijana wengi chipukizi wataona napendelewa. Unajua
ninapoingia studio napenda kufanya kazi kwa muda mrefu, hata hivyo iliyo
bora sifanyi bora liende na siwezi kufanya kazi na prodyuza
anayenipeleka tu, ni lazima na mimi nipime kama kazi niliyoifanya
inakwenda vile ninavyotaka au kama yeye anavyotaka ilimradi tufanye kazi
nzuri na iliyobora.
: Unatumia muda gani kurekodi singo moja na kwa upande wa video ni siku ngapi?
Diamond: Inategemea, inaweza kuwa
siku mbili au miezi sita lakini nyimbo nyingi zinatumia muda mwingi
kwasababu wakati mwingine naanza halafu napata shoo hivyo inanibidi
nipange muda mwingine wa kurekodi. Kuna nyimbo zangu ambazo nilizifanya
kwa muda mrefu sana hizo huwa sizisahau ikiwemo Ukimwona, Mbagala,
Nataka Kulewa na nyinginezo. Nakumbuka katika kazi nilizofanya kwa muda
mfupi ni My Number One nilioufanya kwa prodyuza Sheddy Clever kwa
kipindi kifupi sana pamoja na Mapenzi Basi sambamba na Binadamu hizi ni
baadhi ya kazi ambazo hazikunipasua sana kichwa kuzikamilisha.
Mapaparazi wetu: Una prodyuza wako maalumu au studio yako mwenyewe?
Diamond: Sina prodyuza maalumu kila kazi
nitakayotaka kuifanya ninatafuta prodyuza yule ninayemtaka hata kama
sijawahi kufanya naye kazi. Ninafanya hivi nikiwa na malengo maalumu kwa
kujiweka vizuri mimi kama msanii na hata kuwapa nafasi maprodyuza
mbalimbali kutia mkono kwenye kazi ya mikono yangu. Ninaogopa kuwa na
prodyuza maalumu kwa kuwa najua atanisumbua ikiwa atajua kwamba
namtegemea yeye pekee katika kazi zangu. Studio sina kwa sasa ila nina
mikakati ya kuwa na studio kwani nimeshanunua baadhi ya vifaa.
Mapaparazi wetu: Unadhani ndiyo sababu iliyokufanya ukagombana na Bob Junior au Manecky?
Diamond: Hapana haya mambo
yalishapita lakini nilijifunza mengi ndiyo maana niliamua kuja na staili
hii. Naogopa kubaki kuwa msanii ninayetegemea prodyuza fulani, bila
yeye siwezi kufanya muziki, lakini mimi ni Diamond ninaweza kufanya
muziki na prodyuza yeyote naye akaonyesha ufundi wake kupitia kazi
yangu.
Mapaparazi wetu: Shoo gani kubwa kuliko zote uliyowahi kufanya ambayo haijawahi kujirudia?
Diamond: Diamond Forever. Hii
ilikuwa kubwa sana ambayo sitakaa nikaisahau, ilihudhuriwa na watu
wakubwa na maarufu nchini Tanzania hata hivyo ilikuwa ya kipekee ambayo
haijafanana na yoyote ile. Ya pili ni ile ya Dar Live ambayo nilifanya
baada ya kushuka katika helikopta ile pia ilikuwa kubwa. Lakini kwa nje
ya nchi ni Mombasa na Comoro huko nilifanya shoo kubwa sana ambazo
siwezi kuzisahau.
: Ni shoo ipi iliyowahi kukuingizia pesa kubwa kuliko zote?
Diamond: Shoo ile ya Mlimani City
ya Diamond Forever, ile iliniingizia pesa kubwa sana na tangu pale
ndipo nilipoanza kufurahia matunda ya kazi yangu. Nilifanya shoo pia
Burundi, Mombasa na Congo shoo hizi ziliniingizia kiasi kikubwa sana cha
pesa siwezi kutaja ni shilingi ngapi lakini ni pesa nyingi ambazo
sitakaa nizisahau.
Mapaparazi wetu: Shoo ipi ilikuwa ya bei chee ambayo huwezi kuisahau
Diamond: Kwa kweli siwezi kusahau
nilipofanya shoo yangu ya kwanza kubwa mwaka 2009 kwenye Fiesta
iliyofanyika Dar es Salaam, ilikuwa ndiyo shoo yangu ya kwanza na kubwa
wakati huo nilikuwa natamba na wimbo Kamwambie, ilinichukua muda mrefu
sana kujiandaa mimi pamoja na madansa wangu wanne tulilipwa Sh 50,000
lakini sikukata tamaa kwani ilikuwa ndiyo mwanzo wangu wa kujuana na
watu wengi na wadau wakubwa wa muziki nchini humu ambao nilikutana nao
kwenye ile shoo.
Mapaparazi wetu: Kwa hivi sasa ni shoo gani ambayo unaweza kusema kwamba utafanya kwa bei ya chini na ni shilingi ngapi?
Diamond: Shoo ninayoweza kufanya
kwa bei ya chini kabisa ni Sh 10 milioni za Kitanzania na hii labda
nione anayeniomba nifanye shoo hiyo hayuko vizuri na pengine ni rafiki
yangu na hawezi kuninyonya, si hivyo tu itategemea pia ni kampuni gani
na ni watu wa aina gani ambao watanitaka nifanye nao kazi.
Mapaparazi wetu: Kwa kawaida Diamond ni msanii wa gharama gani kwa shoo moja ndani na nje ya nchi?
Diamond: Kwa kawaida shoo moja
ninafanya kuanzia Sh15 milioni mpaka Sh20 milioni kulingana na muda
nitakaofanya shoo. Pia zile za nje ninafanya kwa gharama ya Dola 20,000
mpaka 30,000 yaani ni Sh32 milioni mpaka 48 milioni hivi kwa fedha za
Tanzania na nikiwa huko nahakikisha ninafanya kazi vile inavyotakiwa.
Lakini hali ni tofauti inavyokuja shoo ile ya uwanjani yaani hapa
nazungumzia shoo kubwa zinazofanyika nje ya ukumbi, hizi natoza Dola
20,000 ambayo ni sawa na Sh32 milioni 32 kwa fedha ya Kitanzania.
Mapaparazi wetu: Kuhusu madansa wako unawachukuliaje?
Diamond: Ni kama kaka zangu na
ninawapenda sana kwani tumetoka nao mbali na wanajua kuwa tunafanya kazi
pamoja kutengeneza maisha hivyo ni kama ndugu zangu na tunasaidiana
kwenye kila jambo ukizingatia kuwa kile tunachokipata tunagawana. Kwa
kweli najitahidi sana kuwaambia hasa kuhusiana na masuala ya kimaisha,
nahusika katika maisha yao ya kila siku na nijuavyo mimi nikikosea tu
mmoja akapotea kundi langu litakuwa limeharibikiwa maana kila mtu
namtegemea kwa upande wake. Kwa sasa wamejenga nyumba zao na wanaendelea
vizuri kimaisha hilo ndilo sharti langu lazima wafanye mambo ya
maendeleo kwa kile tunachokipata.
Mapaparazi wetu: Umesafiri nao nchi ngapi, na kwanini unapenda kuambatana nao?
Diamond: Nimesafiri nao sehemu
mbalimbali kama Burundi, Comorro na sehemu nyinginezo ambako nimekwenda
kufanya shoo, sina tabia ya kusafiri peke yangu hata nikienda Ulaya na
hata Marekani lazima niwe nao. Ninapenda kuwa nao kwani ni sehemu ya
muziki wangu na imefika wakati nimekuwa nataka mapromota kuhakikisha
wanatulipia mimi na madansa wangu kwa ajili ya shoo hasa tutakapojua
kuwa shoo fulani itaingiza watu wengi au udhamini mkubwa.
Mapaparazi wetu: Kuna safari ambayo umewahi kusafiri peke yako?
Diamond: Ziko nyingi, nilienda
mwenyewe kutokana na ukubwa wa shoo, lakini ni miaka kadhaa nyuma,
baadaye nilijiwekea mikakati kwamba siwezi kusafiri mwenyewe wakati shoo
nahitaji kufanya na madansa wangu, awali mapromota walikuwa wagumu
kunielewa na wapo waliokataa. Niliachana nao na kuwataka wakishajipanga
na kuhakikisha kwamba wanaweza kunichukua mimi na madansa wangu
watafanya hivyo.
Mapaparazi wetu: Umewahi kuwatema madansa?
Diamond: Sijawahi kubadilisha
madansa kwa sababu wanajua kazi yao. Ingawa nilikuwa na madansa sita
nilipokuwa naanza muziki lakini niliachana na wawili kutokana na
utendaji wao wa kazi. Wawili hawa hawakuwa wabunifu kila siku walikuwa
na staili ileile, niliamua kuchagua vichwa ambavyo vikikaa na mimi
mwishowe tunatoka na kitu makini na chenye kueleweka. Kulikuwa na tatizo
pia la kukosea stepu wakati wa shoo hili lilikuwa likinishushia sana
hadhi yangu jukwaani, hapo ndipo nilipoamua kuwaondoa.
Mapaparazi wetu: Kwa upande wa malipo unawalipaje?
Diamond: Ninawalipa vizuri lakini
siwezi kutaja kiwango ila ingekuwa kwangu ningetaja, hiyo ni haki yao
wao wenyewe kutamka ila mimi siwezi kutaja. Malipo ninayowalipa yapo
machoni mwa watu wanaowazunguka, dansa kujenga nyumba kumiliki baadhi ya
biashara si jambo dogo, hivyo ninawalipa vizuri. Na hata gharama za
kusafiri ndani na nje ya nchi vyote ni juu yangu, malipo tunayoyapata
tunagawana.
Mapaparazi wetu: Unakumbana na changamoto zipi katika kazi yako?
Diamond: Nakumbana na mengi,
kwanza unapokuwa msanii unayeongoza lazima upate vikwazo vingi.
Nakumbana na watu wengi wanaonichukia na kunitusi bila sababu za msingi,
hata hivyo nasingiziwa vitu vingi ambavyo havipo nadhani hii ni
changamoto iliyotokana na kufanya vizuri katika muziki.
Wapo ambao wanamwona Diamond anafanya vizuri
kwenye muziki badala ya kukaa na kuangalia nimepita wapi na wapi anaanza
kutoa lawama kwamba ameibiwa na mengine ambayo kimsingi hayana maana.
Mapaparazi wetu: Siku za hivi karibuni
kuna maprodyuza na wasanii wasiofahamika ambao walijaribu kutengeneza
kazi yako ya My Number One na kukutusi kupitia wimbo huo na wapo
waliotunga mashairi mengine yaliyozungumzia maisha yako kabla hujawa
staa, ulijisikiaje? Na unachukua hatua gani?
Diamond: Awali niliumia sana
nilipoibiwa mashairi ya wimbo wangu wa Mbagala, iliniuma sana kwa muda
wa wiki nzima uchungu nilioupata siwezi kuuelezea. Lakini baadaye
nilikomaa, huwezi amini niliposikia zile nyimbo nilicheka sana kisha
nikawadharau sana watu waliofanya hivyo maana nipo kwenye hii tasnia
siwezi kuchukia watu wasiojua walitendalo kwani na wao wapo katika
kujitafutia riziki. Lakini hata hivyo sheria ya muziki bado haijawa
makini hapa nchini nitachukua hatua gani mwisho wa siku nitaacha kufanya
mambo yangu ya msingi na kushughulikia wezi wa kazi zangu ambao hata
hivyo hawatabanwa kwa lile walilolifanya.
Mapaparazi wetu: Msanii yupi hapa Tanzania anakutisha kama hayupo vipi huko nje ya nchi?
Diamond: Kwa hapa Tanzania
sijaona mwanamuziki anayenitisha, ila siwezi kujua mashabiki wao ndio
majaji, nafikiri kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake. Kati ya
wanamuziki ninaowahusudu mimi kwa nje ya nchi hasa Afrika ni P Square
pekee, hawa wapo katika nafasi kubwa sana kwenye ubongo wangu na
nafikiria ni lini ninaweza kuwafikia, hiyo ndiyo ndoto yangu daima.
Mapaparazi wetu: Unapokuwa juu ya jukwaa unakumbana na vishawishi vipi ukiwa kama msanii mkubwa?
+
Diamond: Ninapata vishawishi vingi sana
ninapokuwa jukwaani. Kwa kweli ninashawishiwa na wakinadada, mfano kuna
mwanamke mmoja ambaye alikuwa mmoja wa mapromota wa shoo nchini
Uingereza alitaka kunibusu mdomoni kwa lazima, kitendo kile
kilinifedhehesha sana na nilishindwa nifanyeje kwani nipo ugenini na
jukwaani ilikuwa ngumu sana kwangu. Wakati mwingine wanawake wanapanda
jukwaani ili wacheze na wewe mwisho wa siku wanaingiza mikono kwenye
suruali yaani sipendezwi kabisa na michezo ya namna hii.
Mapaparazi wetu: Umewahi kuibiwa ukiwa jukwaani?
Diamond: Nimeshaibiwa sana hasa
katika hizi shoo ndogo ndogo mara nyingi watu wanapanda jukwaani na
kuondoka na kitu chako. Nakumbuka nimeshawahi kuibiwa saa, pete ya
dhahabu na kuna mmoja alitoa kali ya mwaka yaani yeye alinivua nguo kwa
lazima.
Mapaparazi wetu: Inakuwaje nje ya muziki, unakumbana na changamoto zipi?
Diamond: Kitu ambacho ni
changamoto kubwa sana kwangu ni simu yangu ya mkononi. Kila baada ya
miezi sita au mitatu nalazimika kubadili namba yangu ya simu,
nasumbuliwa sana na watu ambao hata hivyo hawana la msingi la kuniambia.
Ni kweli kwamba mawasiliano ni kitu cha msingi na ninawapenda mashabiki
wangu lakini namba yangu inasambaa kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba
nashindwa kupokea simu za maana kwa kudhani kwamba na hao nao ni
wasumbufu.
Mapaparazi wetu: Ina maana milio yote ya simu hapo ni watu wanakupigia?
Diamond: Yap, unavyoona inalia
kila dakika watu wanapiga hapa. Muda mwingi hii simu ninaweka ‘silent’
yaani haitoi mlio wowote kwani inaita kila dakika.
Mapaparazi wetu: Tuzungumzie uhusiano wako. Mpenzi wako wa kwanza unamkumbuka? na je uliwahi kumpa shilingi ngapi?
Diamond: Mpenzi wangu wa kwanza
kabisa enzi hizo ninajifunza mambo haya sikumbuki vyema jina ila alikuwa
anaishi Tandale na mimi pia nilikuwa naishi huko na mama yangu.
Sikumbuki kama nimewahi kumhonga maana enzi hizo mimi nilikuwa napewa tu
na mama yangu pesa, sikuwa na hela yoyote ya kumpa na ilikuwa ni kwa
kipindi kifupi kama miezi minne hivi, hata hivyo tulikuwa tunaibana tu
kwa siri nilikuwa mdogo.
Mapaparazi wetu: Kwanini mliachana?
Diamond: Kwanza nilikuwa sijajua
mapenzi ni nini. Hata hivyo haikuwa rasmi na wala nilikuwa sijawa na
akili ya kupenda sana na nilikuwa na fikra kwamba ni mchezo tu hivyo
tuliachana mapema kwani hata yeye akili yake ilikuwa haijakomaa.
Mwanaspoti: Mpenzi wako uliyekuwa naye kabla ya kuwa staa nasikia uliachana naye baada ya kutoka kimuziki kwa nini?
Diamond: Nilimpenda sana lakini aliniacha kabla
ya kutoka. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa anaitwa Sarah Sadick,
sijawahi kumuhonga na ndiye mwanamke niliyewahi kumpenda sana. Wakati
huo Naseeb Abdul kabla sijawa Diamond nilikuwa nahaha kuhangaika ni vipi
nitatoka kimuziki. Msichana huyu ndiye aliyenipa hasira za kufanya
muziki kwa bidii zote baada ya kunitema na kuanza kuhangaika na wengine
na aliniita majina mengi yasiyo mazuri, kisa sina fedha. Si kwamba
nilimuacha bali yeye ndiye aliyeniacha kama zali baada ya wiki kadhaa
nikatoka na wimbo Kamwambie, taratibu nikaanza kuwa staa naye akaanza
kurudi ila nilishamuondoa moyoni mwangu.
Mapaparazi wetu: Kwa nini mliachana? Unadhani hakukufaa tena kwa kuwa ulishakuwa staa?
Diamond: Alinisumbua sana
kutokana na ugumu wa maisha niliokua nao kwa kipindi cha nyuma hadi
kufikia 2009. Nilimpenda sana huwezi amini nilikuwa silali usingizi kwa
ajili yake. Nahisi ilitokana na mimi kukosa kazi ndiyo maana ilifikia
hatua alinipotezea. Lakini baada ya kupata na kujulikana alinifuata
lakini sikutaka tena hata baada ya kuniomba msamaha.
Mapaparazi wetu: Umewahi kuwa na wanawake wangapi tangu uwe staa?
Diamond: Sikumbuki kwa kweli wapo
wengi mno, si unajua tena wapo walionitaka na kunilazimisha nifanye
hivyo, lakini idadi kamili siwezi kukumbuka na kila siku nasumbuliwa na
hawa wanawake.
Mapaparazi wetu: Ni wapenzi wangapi ambao umekuwa nao kipindi kirefu na kuwapenda kama wapenzi wako?
Diamond: Nimewahi kuwa na wapenzi
wanne katika kipindi chote cha ustaa wangu na sikupenda kubadili ovyo
ila wengi wao hawakuweza kutimiza haja ya moyo wangu.
Unaweza kuwataja majina?
Diamond: Ndiyo ila wawili
wanafahamika zaidi. Wa kwanza kabisa alikuwa anaitwa Sarah na wa pili
alikuwa anaitwa Hawa yule msichana niliyeimba naye katika wimbo
‘Nitarejea’, huyu alizidiwa ujanja na Wema Sepetu ambaye naye alikuja
kuondoka kwangu na baadaye nikawa na Penieli Mungilwa.
Mapaparazi wetu: Mwanamke yupi unahisi ulimpenda kuliko wote?
Diamond: Mwanamke wangu wa kwanza
Sarah Sadick huyu aliniingia sana moyoni sijajua ni kwanini. Lakini
nahisi huenda kwa kuwa awali alinipenda kweli kwa kuwa wakati huo sikuwa
na kitu. Hata hivyo nahisi ilitokana na mimi kutokuwa bize na wakati
huo sikufikiria lolote zaidi ya yeye ilitokana na kutokuwa na kazi ya
kufanya. Siku hizi sina mapenzi ya kivilee, nawaza zaidi pesa na
ninaihangaikia na zaidi ni muziki wangu, hili ndilo la kwanza kabisa
linalonifanya niwe bize mapenzi baadaye.
Mapaparazi wetu: Umeshawahi kutongozwa na wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna mmoja kati
ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye mwenyewe ndipo nikawa
naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza
kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi
mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa sana kwenye
mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp, Instagram na kwingineko na wapo
wasichana ambao wanatafuta namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mapaparazi wetu: Ni mwanamke wa aina gani unataka awe mkeo?
Diamond: Kwanza ninahitaji aijue
kazi yangu na ajue kwamba mimi ni mtu maarufu hivyo akubaliane na
changamoto mbalimbali atakazokumbana nazo kwa kipindi atakachokuwa ndani
ya ndoa, siyo siku mbili anafungasha virago. Pia ajue kwamba
nitamsikiliza mama yangu kwanza kabla ya yeye hilo naliweka wazi, yeye
ana nafasi yake katika maisha yangu lakini mama yangu nimempa
kipaumbele, tatu awe tayari kuishi na mama yangu. Nne awe na akili na
mwenye utambuzi na atakayeniongoza katika kazi zangu, sihitaji kuwa na
mwanamke golikipa kila siku ategemee kutoka kwangu. Tano awe mzuri,
nahitaji mke bwana…yule nitakayeweza kutoka naye out kwenye zulia
jekundu, nikapita naye bila tatizo lolote awe mzuri.
Itaendelea Jumatatu…
0 comments:
Toa Maoni yako
Tuambie Unafikilia Nini..!